Thursday, August 9, 2012

Mdee ataka mkataba wa kampuni ufutwe


JIBU LA SWALI LA MBUNGE KAWE
MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), ameishauri tume iliyoundwa kuchunguza uhalali wa kampuni ya uwindaji wanyama,kupangisha kitalu chake kwa kampuni ya uchimbaji madini ya urani wilayani Namtumbo, kusitisha mkataba huo na kuhakikisha fedha zinawanufaisha wanakijjiji badala ya mwekezaji.
Akizungumza kwa njia ya simu juzi, Mdee alisema mkataba uliosainiwa kati ya kampuni ya uwindaji wa Game Frontiers na kampuni ya uchimbaji urani katika kijiji cha Mbaranga’andu kilichopo ndani ya pori la hifadhi ya Selous, unapaswa kumnufaisha mwananchi.
Awali, kijiji hicho kiliingia mkataba na kampuni ya uwindaji , ambapo walikubaliana kuwinda wanyama pekee.
“Ninaelewa kuwa katika mkataba huu wa pili kijiji kilipata dola 10,000 tu kati ya milioni sita ambazo kampuni ya uwindaji iliingia mkataba na kampuni ya uchimbaji madini katika kijiji hicho, hii si sawa,” alisema.
Alisisitiza tume iliyoundwa na Wizara ya Madini na Nishati kuchunguza uhalali huo itachukua hatua na kuona kuwa wanakijiji wanapata fedha wanazostahili.
“Tuwape muda tume ya uchunguzi na kuangalia mapendekezo yao, lakini suala kubwa hapa ni kuona kuwa wanakijiji wananufaika kutokana na mkataba huo uliosainiwa kinyume na sheria,” aliongeza.
Aliongeza kuwa mkataba huo umekiuka sheria kwani hakuna mwekezaji wa vitalu anayeruhusiwa kuchimba madini ndani ya pori hilo.
Hata hivyo, mbunge huyo alisema wakati kampuni hiyo ya uwindaji ikiingia mkataba huo wa siri, sheria ya zamani ya uhifadhi wa wanyamapori ya mwaka 1974 na sheria mpya namba 5 ya mwaka 2009, zinamruhusu mtu aliye na leseni ya uwindaji kuwinda wanyama tu, siyo vinginevyo.
Akiwasilisha bajeti ya kambi ya upinzani hivi karibuni mjini Dodoma, Mdee ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi, alifichua ufisadi mkubwa wa mamilioni ya dola za Marekani.
Mamilioni hayo ya fedha yangeibwa kupitia mkataba wa siri uliofikiwa baina ya kampuni moja ya uwindaji ya Kitanzania na kampuni mbili za kigeni kwa ajili ya kufanya utafiti wa uchimbaji wa madini ya urani kinyume cha sheria ya matumizi ya ardhi.
Kwa upande wao wadau wa masuala ya nishati wameipongeza hatua ya serikali na kusema itaokoa fedha za kigeni zinazopotea kwa njia ya mikataba mibovu.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment