AITAKA SERIKALI IMTHIBITISHE HADHARANI MTU ANAYEITWA RAMADHAN
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amefufua upya sakata la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, akitaka serikali ithibitishe hadharani mtu anayetajwa kuhusika na tukio hilo.
Akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara mjini Ifakara, Morogoro jana, ikiwa ni sehemu ya Operesheni Sangara awamu ya pili, Dk. Slaa aliyeambatana na viongozi wakuu wa chama hicho, akiwemo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, alisema kuwa Serikali ya CCM imekuwa na kiburi cha kuwatisha wanaotaka kutetea maslahi ya wananchi.
Alisema kuwa imefikia hata hatua ya wengine kutishiwa vifo, huku akitolea mfano wa kutekwa, kupigwa na kisha kuumizwa Dk.Ulimboka, aliyetendewa unyama huo usiku wa kuamkia Juni 26 katika msitu wa Mabwepande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
“Serikali ina nguvu ya kuvifungia vyombo vya habari kwa sheria dhalimu ya magazeti ya mwaka 1977, lakini haitaweza kuzuia midomo ya watu kujadili suala zima la kutekwa huko kwa Dk. Ulimboka,” alisema.
Dk. Slaa ambaye alikuwa akishangiliwa kwa nguvu, aliongeza kuwa, kuanzia sasa CHADEMA itaanzisha mapambano kwa ajili ya kutaka kupata ukweli juu ya aliyemteka Dk. Ulimboka.
Alisema kuwa miongoni mwa simu zilizowasiliana na Dk. Ulimboka ni Ramadhan Ingondhur, aliyetajwa kama mtu wa mwisho kabla ya kutekwa pamoja na namba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Mabwepande, aliyemtaja kwa jina la Abdallah Punja.
“Serikali na Usalama wa Taifa wanapaswa kusimama hadharani na kuuambia umma Ramadhan ni nani na kwanini anahusika na Idara ya Usalama wa Taifa.
“Mimi ni muumini wa Usalama wa Taifa na wala siwaondolei hadhi, lakini kwa mwendo huu ni wao wenyewe ndio wanajiondolea hadhi yao, na sasa wamekaa kufuatilia mikutano ya vyama vya siasa, hususan CHADEMA,” alisema Dk Slaa.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbowe alisema umati uliokusanyika unaonesha namna wakazi wa Kilombero walivyomthamini aliyekuwa mbunge wa viti maalumu, marehemu Regia Mtema.
Mbowe aliomba jina la uwanja wa Ifakara libadilishwe na kuitwa Uwanja wa Ukombozi, na kwamba hali hiyo iwe chimbuko la ukombozi kwa Mkoa wa Morogoro.
Aliwataka wakazi wa Kilombero kuacha kulalamika na badala yake wachukue hatua kwa kuachana na CCM na kujinga na CHADEMA.
“Ndugu zangu kila mmoja ana wajibu wa kujiuliza kafanya nini kwa ajili ya nchi yake, watoto wake na anawaandalia nini siku zijazo. Tambueni tupo katika utwala usiowajali na hili jukumu lenu ninyi wananchi kujiondoa katika hali hii na si kazi ya Dk Slaa, Mbowe au Lissu,” alisema.
Mbali na Dk. Slaa na Mbowe, viongozi wengine waliokuwa katika msafara huo ni Joshua Nassar (Arumeru Mashariki), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Hamad Yusuph (Naibu Katibu Mkuu Zanzibar), Suzan Kiwanga (Viti Maalumu), Joyce Mukya (Viti Maalumu) na wengine wa makao makuu.
Naye Lissu, alisema baada ya kupita kuanzia Mikumi hadi Ifakara, hajui ni kwanini bado wakazi wa wilaya hiyo wanaendelea kuikumbatia CCM huku akishangazwa na kitendo cha wananchi hao kuendelea kutozwa ushuru wa mazao ambao serikali ilikwishaupiga marufuku.
Alisema ufike wakati wananchi wawakatae viongozi wasiochaguliwa kuwa wawakilishi wao kwani wanasimamia masilahi ya waliowateua kama inavyotokea sasa katika maeneo mbalimbali.
Mbunge wa Mbeya Mjini, Mbilinyi alijibu kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuwa wapinzani wanapinga maendeleo, akisema kwamba si kweli, kwani wao wanapingana na mipango inayowapa fursa mafisadi kujineemesha, huku wananchi wakiendelea kuogelea katika umasikini.
No comments:
Post a Comment