Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kuwa kimesikitishwa uamuzi wa Mahakama kusitisha mgomo wa walimu na kusema kuwa madai ya walimu yanalipika.
Mgomo huo uliodumu kwa siku nne kuanzia Julai 30 hadi Agosti 2, mwaka huu ilikuwa na lengo la kuishinikiza serikali kuwalipa walimu madai mbalimbali, ikiwemo nyongeza ya mishahara.
Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kufafanua kuwa uamuzi huo siyo sahihi kwa kuwa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kilifuata kanuni za kisheria kabla ya kuanza mgomo huo na kwamba madai hayo yanalipika.
Profesa Lipumba alisema siyo kweli kwamba nyongeza ya mishahara kwa walimu haiwezekani kama Rais Jakaya Kikwete alivyoeleza wiki iliyopita kwa sababu serikali imekuwa ikifanya matumizi mengi ya fedha yasiyo ya lazima na hivyo akaishauri serikali kupunguza matumizi hayo, “Sisi tunaamini malipo ya walimu yanalipika serikali inachotakiwa kufanya ni kurekebisha namna ya upangaji wa bajeti yake kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kama vile safari zisizo za lazima, ununuzi wa magari ya kifahari na matumizi makubwa ya kiutawala,” alisema.
Aidha, mwenyekiti huyo aliiomba serikali kuonyesha nia ya kuwasaidia walimu kwa kuwalipa madai yao ya nyongeza ya mishahara angalau kwa sehemu kwa kuweka wazi kuwa ni asilimia ngapi watakayoweza kuwaongezea kama nyongeza ya asilimia 100 imeshindikana, “Pamoja na mgomo huo kusitishwa na Mahakama ya kazi, lakini bado serikali haijaweka wazi kuwa ni mipango gani waliyonayo ya kutatua tatizo la madai ya walimu ambayo yamedumu kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, waweke wazi ni asilimia ngapi inayoweza kulipika kama hiyo 100 wanayotaka imeshindikana,” alisema Profesa Lipumba na kuhoji kuwa mbona wabunge wanaongezewa posho kila siku?
Profesa Lipumba alisema kuwa kama nchi inayoendelea ni lazima kuwekeza kwenye sekta ya elimu kwa kuboresha miundombinu ikiwa ni pamoja na kuwapa motisha walimu ili kuwa na maendeleo endelevu.
Hata hivyo, aliiomba serikali kuweka mazingira ya kutatua matatizo ya wafanyakazi katika kada mbalimbali nchini kabla ya kufikia katika hatua za migomo kwani migomo katika nchi zinazoendelea inasababisha kurudi nyuma kimaendeleo.
Nipashe
No comments:
Post a Comment