Friday, August 10, 2012

Lissu: Ma-RC, DC watimuliwe bungeni


MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lisu (CHADEMA), ameibana serikali na kuitaka kuwatimua bungeni wabunge ambao ni wakuu wa wilaya na mikoa kwa kuwa wapo kinyume na Katiba.
Lisu alitoa kauli hiyo bungeni jana alipokuwa akiuliza swali la papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na kuongeza kuwa wakuu wa wilaya (DC) na wakuu wa mikoa (RC) ni maofisa waandamizi wa serikali, hivyo hawapaswi kuwapo bungeni.
Alisema Katiba ilivyo sasa inakataza ofisa mwandamizi wa serikali kuwa mbunge na kuhoji ni kwa nini serikali inaendelea kuwaruhusu watu wa aina hiyo kuwapo bungeni.
“Kuna wabunge wameteuliwa kuwa wakuu wa wilaya na mikoa, hivyo wamenyang’anywa haki yao ya kuwa wabunge, kwa nini serikali inaendelea kuwaruhusu watu wa aina hii kuwapo bungeni wakati ni maofisa waandamizi wa srerikali?” alihoji.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu, alisema kwa jinsi anavyofahamu utaratibu huo unamhusu mtumishi wa serikali (Public Servant) lakini DC na RC ni watendaji wa kisiasa, si moja kwa moja maofisa wa serikali, hivyo anaamini kuwa hawajakosea.
Katika swali la nyongeza, Lisu alisema katika Katiba ya mwaka 1965 ilieleza kuwa DC na RC si maofisa waandamizi wa serikali, hivyo waliruhusiwa kuingia bungeni, lakini baada ya kufanyiwa marekebisho mwaka 1992 suala hilo liliondolewa, hivyo kuwaomba wataalamu wa sheria waliopo serikalini kulifanyia kazi suala hilo.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu alisema kuwa tafsiri inayotolewa na mbunge huyo si kama wao wanavyoitumia na kusisitiza kuwa suala hilo watalifanyia kazi, ili ukweli upatikane na baadaye serikali kulitoea kauli.
“Vingunge wenzio wanaojua madudu haya watalifanyia kazi na tutalitolea tamko, lakini bado naamini Waziri Mkuu hajakosea sana.”
Wakati huohuo, serikali imesema inapitia upya mikataba ya wawekezaji mbalimbali na watakaobainika kushindwa kufuata mikataba wataivunja, ili wapewe watu wengine.
Pinda alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM), aliyehoji serikali inatoa tamko gani kwa wawekezaji wasiozingatia mikataba.
Alisema hakuna mwekezaji anayeruhusiwa kuingia moja kwa moja katika maeneo ya vijini kama hakuna ridhaa ngazi ya taifa.
“Utaona katika maeneo ya ardhi hilo halifanyiki, labda kama umepita katika mkondo tulioridhika ambao utawanufaisha wananchi, pengine kuna kupuuzwa kwa agizo hili. Tutafuatilia suala hili,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, alisema kipengele cha dini kimeondolewa katika sensa kwa kuwa hakina tija kwa maendeleo ya nchi.
Alisema miaka ya nyuma kipengele hicho kilikuwapo, lakini kiliondolewa, ili kuondoa hofu ya kutokea mgogoro.
Pinda alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu swali la mbunge wa viti maalum, Susan Lyimo, aliyehoji kwa nini serikali imeondoa kipengele cha dini.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment