Friday, August 10, 2012

HARAMBEE YA M4C


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeman Mbowe, leo anatarajia kuongoza harambee ya kukusanya fedha kwa ajili ya kufanikisha mkakati wa vuguvugu la mabadiliko (M4C) katika jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam, mjumbe wa Kamati Kuu na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alisema harambee hiyo itafanyika kuanzia majira ya saa 1:00 usiku katika Hoteli ya Serena kwa lengo la kuwakutanisha wanamabadiliko wa daraja la kati.
Alisema katika harakati za vuguvugu la mabadiliko wana lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni tano kwa upande wa Dar es Salaam, wanatakiwa kukusanya asilimia kumi ya fedha hizo.
“Tulienda Mwanza pamoja na mwenyekiti na tulifanya hivyo, kuna dalili za mafanikio makubwa na kama watu watakuwa makini, basi kutakuwa na mafanikio na lengo la fedha hizo ni kununulia magari kwa ajili ya kuendesha kampeni nchi nzima,” alisema Lema.
Naye Mwenyekiti wa M4C mkoa wa Dar es Salaam, Alex Mayunga, alisema wameandaa chakula cha jioni ambapo watu 500 kutoka katika kada tofauti tofauti, wamealikwa.
Alisema lengo lingine ni kukusanya rasilimali watu, fedha na vifaa vya kazi kwa lengo la kueneza chama katika vitongoji na mitaa ambako ndiko kunakoakisi maisha halizi ya Watanzania.
Alitaja lengo lingine kuwa ni kuweka mkakati wa kuendeleza mshikamano na umoja miongoni mwa wana-mabadiliko wa daraja la kati ili kutoa mchango kwa mabadiliko ya katika jamii.
Alisema, wanahakikisha chama kinakusanya rasilimali fedha kwa lengo la kununua vitendea kazi kulipa gharama za kupata rasilimali kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014 na uchaguzi mkuu mwaka 2015.



No comments:

Post a Comment