KUFUATIA Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kumvua ubunge aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Igunga, Dalali Kafumu, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, leo anatarajia kunguruma mjini Igunga katika mkutano wa hadhara kwa ajili ya kuwashukuru wakazi wa mji huo.
Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene, jana ilieleza kuwa Dk. Slaa atafuatana na Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Tabora, Kansa Mbaruku, pamoja na baadhi ya maofisa wa chama hicho walio katika Operesheni Sangara (M4C) inayoendelea mkoani Tabora.
Makene alisema baada ya mkutano huo wa Igunga, Dk. Slaa na timu yake watarejea mkoani Morogoro kwa ajili ya kuhitimisha opersheni ya mkoa huo katika mkutano wa hadhara utakaofanyika kesho kutwa katika mji wa Morogoro.
“Ni kweli kuna umuhimu wa kuwashukuru wakazi wa mji wa Igunga ndiyo maana Dk. Slaa ameamua kuchukua jukumu hilo kwa ajili ya kuonesha thamani ya wakazi wa mji huo katika kupigania mabadiliko ya kweli kwa ajili yao na vizazi vyao,” alisema Makene.
Hivi karibuni Mahakama Kuu Kanda ya Tabora ilimvua ubunge Peter Dalali Kafumu baada ya kuridhika pasipo shaka kuwa uchaguzi mdogo uliomuingiza madarakani ulikiuka taratibu nyingi.
Mlalamikaji katika kesi hiyo alikuwa, Joseph Kashindye, ambaye alikuwa mgombea wa kiti hicho kupitia CHADEMA, alifungua kesi dhidi ya Kafumu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo.
Taratibu zilizokiukwa ni pamoja na matukio yaliyojitokeza wakati wa kampeni za uchaguzi huo ikiwa ni pamoja na kutolewa kwa ahadi ya kutojengwa daraja la Mbutu kama Dalali atachaguliwa.
Aidha, Jaji Mary Shangali aliyehukumu kesi hiyo alisema kulikuwa na ukiukwaji wa sheria, kwa kitendo kilichofanywa na upande wa walalamikiwa kwenda kutembelea hospitali na kutoa misaada mbalimbali.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment