ASKARI WASHANGAZWA NA NGUVU ILIYOTUMIKA
NGUVU ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), katika mikutano ya hadhara na maandamano inayofanya mara kwa mara hivi sasa yaelekea kutishia uhai wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kiasi cha kulazimika kuvitumia vyombo vya dola kuidhibiti, Tanzania Daima Jumapili limedokezwa.
Miongoni mwa mbinu hizo ni kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano yaliyopangwa kufanywa kwa siku 10 kuanzia jana katika Mkoa wa Morogoro kwa kulitumia Jeshi la Polisi.
Jeshi la Polisi lilizuia mikutano hiyo na maandamano ya CHADEMA kwa madai kadhaa yakiwamo uchache wa askari, sherehe za Sikukuu ya wakulima (Nanenane), mgomo wa walimu uliozuiwa siku tatu zilizopita na maeneo husika kutumiwa na CCM katika mikutano ya hadhara.
Kinyume cha kauli ya Jeshi la Polisi mkoani humo kuwa lina uchache wa askari, jana idadi kubwa ilionekana ikijiandaa kukabiliana na maandamano na mikutano ya CHADEMA kama ingefanyika.
Baadhi ya askari waliowekwa tayari kukabiliana na CHADEMA, walieleza kushangazwa kwao na nguvu kubwa iliyotumika kuwazuia CHADEMA badala ya nguvu hiyo ingeelekezwa kuwalinda.
Polisi wapigwa jua
Taarifa kutoka mkoani Morogoro zinaeleza kuwa askari kutoka katika mikoa ya Iringa, Dar es Salaam na Dodoma waliokusanyika mkoani humo kwa ajili ya kuongeza nguvu ya kukabiliana na mikutano ya CHADEMA kama ingefanyika hiyo jana, walijikuta wakishinda juani bila kazi.
Kushinda juani huko kwa askari hao kunatokana na uamuzi wa viongozi wa CHADEMA kuamua kusitisha maandamano na mikutano hiyo hadi Agosti 8, mwaka huu ambapo itaanzia katika eneo la Mikumi (Kilosa).
Baadhi ya askari waliozungumza na Tanzania Daima Jumapili kwa sharti la kuhifadhiwa majina yao walisema kwa namna ulinzi ulivyoimarishwa isingekuwa rahisi kwa maandamano na mikutano ya CHADEMA kufanyika.
“Logic (mantiki) iko wapi kama nguvu hii iliyoandaliwa kwa ajili ya kuyazuia maandamano ya CHADEMA ingetumika kuyalinda, si kila kitu kingekuwa sawa na yangeenda vizuri tu, sijui ni wapi tunaelekea katika hali hii,” alisema mmoja wa askari.
Alisema kimsingi wao kama askari wa ngazi ya chini hawana tatizo na CHADEMA isipokuwa wanalazimika kupokea amri kwa kuwa ndiyo kazi waliyochagua kufanya na kusema kama watendaji wa serikali hawataacha siasa katika kazi kuna hatari ya kuipeleka nchi pabaya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, alipoulizwa kuhusu hali hiyo alikiri kuwapo kwa askari wengi mkoani Morogoro na kusema ni gharama zimetumika licha ya kukataa kutaja maeneo waliyotoka.
Kuhusu askari wa ngazi ya chini kulaani maandalizi makubwa ya kuzuia mikutano ya CHADEMA badala ya kulinda, Kamanda Shilogile alisema hakuna askari anayeweza kutamka kauli hiyo na kwamba hawatumiki kwa masilahi ya kisiasa.
“Unaniuliza askari wametoka wapi, hilo si swali la msingi, wewe jua gharama zimetumika kwa ajili ya suala hili na huku kusema askari wamesikitishwa na maandalizi ya kuzuia mikutano badala ya kuilinda mbona hawajaniuliza mimi? Hiyo ni wewe mwandishi umetengeneza stori,” alisema Shilogile
CHADEMA yasogeza mbele Sangara
Uongozi wa CHADEMA jana ulitangaza kusogeza mbele mikutano yake na maandamano hayo (Operesheni Sangara) ili kuepuka maafa ambayo yangeweza kutokea baina ya wafuasi wake na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro iliyozuia operesheni hiyo.
Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, walisema zuio hilo la polisi limelenga kukisaidia chama tawala (CCM) ambayo hivi sasa ina hali mbaya kiutawala.
Mbowe alisema CCM imetishwa na matokeo ya ziara za CHADEMA zilizofanyika hivi karibuni katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Mbowe alisema baada ya ziara ya mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa na mafanikio makubwa wabunge wa CCM walitishika kwa kiasi kikubwa hata kufikia baadhi yao kuomba mikutano hiyo ipigwe marufuku ili isiwaondolee uhalali wa kuitwa wabunge licha ya kuzembea katika majukumu yao.
“Tunapaswa kujua kuwa haya ni mapambano baina ya haki na batili, siku zote dhalimu hawezi akaruhusu kirahisi kuondolewa katika udhalimu wake…na atatumia njia mbali mbali ya kujihalalisha, kwa hiyo katika hili tunapaswa kuwa wavumilivu na wenye busara ya hali ya juu katika kukabiliana nao,” alisema Mbowe.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linapaswa kutambua kuwa kuminya haki za msingi za wananchi kwa manufaa ya wachache ni suala lisiloweza kukubalika mbele ya jamii na kwamba hali hiyo ya kuchagua watu wa kuwatumikia itasababisha watu kujenga usugu dhidi ya jeshi hilo.
Naye Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema baada ya majadiliano ya muda mrefu na Jeshi la Polisi walikubaliana kuahirisha uzinduzi wa ziara hiyo iliyokuwa ifanyike jana na badala yake itafanyika Agosti 8, katika Jimbo la Mikumi na kufuatiwa na ratiba nyingine ya mikutano katika Mkoa wa Morogoro.
“Jana (juzi) hatukulala tulikuwa katika mawasiliano na Jeshi la Polisi hata kufikia IGP kushindwa kupokea simu yangu, mwenyekiti alimtafuta na amempata leo asubuhi (jana), tumemfahamisha hoja zetu na mapendekezo yetu naye akatushauri turudi kwa RPC wa Morogoro kwa ajili ya mapendekezo hayo,” alisema.
Alibainisha kuwa katika mapendekezo yao ni pamoja na kumueleza kuwa hoja ya CCM kufanya mikutano pamoja na CHADEMA haina nguvu, kwa kuwa CCM waliomba kwa ajili ya Agosti 4, mwaka huu tu, na maonesho ya Nanenane mkoani Morogoro yanafikia kilele Agosti 8, mwaka huu na mgomo wa walimu umesitishwa na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
Alisema Jeshi la Polisi linapaswa kufahamu dhana ya siasa ya vyama vingi ni kutoa uhuru wa wananchi kuchagua sehemu ya kwenda hivyo kuweka visingizio kuwa kuna mikutano miwili katika wilaya moja ni kuua demokrasia.
Aidha, Dk. Slaa aliongeza kuwa hata kitendo cha jeshi hilo kuchukua magari kutoka sehemu tofauti za nchi kwa ajili ya kuwadhibiti CHADEMA mkoani Morogoro ni matumizi mabaya ya rasilimali za umma na badala yake gharama zilizotumiwa zingeweza kusaidia kuboresha hali ya maisha ya wafanyakazi wa jeshi hilo.
“Tunaionya serikali hii iwe mara ya mwisho na tumekubali hivi kwa sababu sisi si watu wa fujo, ila hatutaweza kuvumilia hasara ya namna hii, kwa kuwa hizi fedha tunazotumia ni za ruzuku zinazotolewa na serikali kwa vyama, sasa hasara hii iweje wabebeshwe wananchi kizembe zembe kwa ajili ya kuminya demokrasia?” alihoji.
Alisema Jeshi la Polisi linatumia sheria zilizowekwa na wakoloni katika kuendesha nchi huku likifahamu fika wakoloni walitumia fursa hiyo kwa ajili ya kuwaminya wapigania uhuru.
“Katika PGO ya Polisi ni mambo machache ndiyo yameboreshwa na zilizobaki ni zile za kikoloni, hivyo watambue sasa ni wakati wa siasa huru na si vita baina ya wenye nchi na wakoloni katika kudai uhuru,” aliongeza Dk. Slaa.
Agosti mosi, mwaka huu, Jeshi la Polisi mkoani Morogoro lilizuia mikutano na maandamano ya CHADEMA kufanyika mkoani humo na kutoa sababu mbalimbali ikiwamo kutokuwa na askari wa kutosha kuilinda mikutano hiyo.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment