Saturday, July 28, 2012

Upinzani wamtaka DPP kumchunguza Mhando


KAMBI ya Upinzani bungeni imemtaka Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) kuruhusu uchunguzi wa kijinai ufanyike dhidi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shrika la Umeme (TANESCO) William Mhando kuhusu tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.
Msimamo wa kambi hiyo ulitolewa bungeni mjini Dodoma jana na Msemaji wa Wizara Kivuli ya Nishati na Madini John Mnyika wakati akiwasilisha maoni ya kambi na kusema Mhando ambaye kwa sasa amesimamishwa kupisha uchunguzi amepoteza sifa za maadili ya utumishi wa umma.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (CHADEMA) aliweka bayana kuwa kambi yao inamtaka kila mbunge wa chama chochote cha siasa chenye uwakilishi ndani ya Bunge anayefuata imani yoyote ya dini amkatae mkurugenzi huyo.
Akifafanua tuhuma hizo zinazomkabili Mhando, Mnyika alisema mipango kwa ajili ya kufua umeme ilitumika kama mwanya wa ufisadi na kuzalisha ‘Richmond nyigine’.
Alisema kuwa katika siku za karibuni kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa wazabuni ambao wamekosa zabuni ya kuiuzia TANESCO mafuta ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya IPTL kutokana na uamuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, wa kuipatia zabuni kampuni ya PUMA Energy (Tz) Ltd zamani BP ambayo inamilikiwa na serikali kwa asilimia 50.
Mnyika alibainisha kuwa licha ya malalamiko ya wazabuni hao, wanafahamu kwamba kuna kampeni kubwa imefanywa na inaendelea kufanywa ndani na nje ya Bunge ili uamuzi huu wa Maswi ubatilishwe kwa maslahi ya makampuni hayo na wapambe wake wa ndani na nje.
“Wanaoendesha kampeni hiyo wanashinikiza Katibu Mkuu Maswi ajiuzulu kwa kile kinachoitwa kitendo chake cha kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma,” alisema.
Mnyika alisema kuwa Juni 10 mwaka jana, Mhando alimwandikia Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufilisi, Vizazi na Vifo (RITA) – iliyokuwa inasimamia ufilisi wa IPTL – kumtaka aendeshe mitambo ya IPTL ili kufua MW 100 za umeme ili kuweza kuondoa mgawo wa umeme uliokuwa unaendelea sehemu mbalimbali nchini.
Mara baada ya kupata barua hiyo, Juni 24 mwaka huo, Mtendaji Mkuu wa RITA alimwandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) akimwomba mwongozo na ushauri juu ya utaratibu wa manunuzi ya mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL kwa dharura.
“Mkurugenzi Mkuu wa PPRA alitoa mwongozo kwa RITA kwa barua yake ya June 28, 2011 ambapo aliielekeza RITA itumie mamlaka yake chini ya kanuni ya 42 ya Kanuni za Manunuzi ya Umma zinazohusu Bidhaa, Kazi na Huduma zisizokuwa na Ushauri Elekezi na Mauzo ya Mali za Umma kwa Tenda,” alisema Mnyika.
Mnyika alisema kuwa baada ya kupata mwongozo huo wa PPRA, Mtendaji Mkuu wa RITA alimwandikia Maswi barua kumweleza kwamba katika makampuni matano yaliyoonyesha nia ya kuiuzia IPTL tani 500 za mafuta kwa siku zilizokuwa zinahitajika kuendeshea mitambo yake kwa Julai, 2011, OilCom na Shell hazikuwa na akiba ya mafuta.
Kampuni ya Mogas ilikuwa na lita 330,000 kwa upande mwingine, kampuni ya Oryx ilikuwa na tani 6,000 lakini ilikuwa inauza mafuta hayo kwa sh 1,668,456.02 kwa tani.
Aidha kampuni ya BP (sasa Puma Energy) ilikuwa na tani 9,000 na ilikuwa tayari kuuza mafuta hayo kwa sh 1,405,864.77 kwa tani.
“Kwa kuzingatia maelezo hayo, Katibu Mkuu Maswi alitoa ridhaa kwa RITA kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL kutoka kwa kampuni ya BP kwa bei iliyotajwa hapo juu,” alisema.
Aliongeza kuwa licha ya ukweli kwamba mafuta ya BP yalikuwa na bei ndogo ikilinganishwa na bei ya Oryx, Septemba 27 mwaka jana, Mhando alisaini mkataba wa kununua mafuta kutoka Oryx kwa bei ya sh 1,501,707.60 kwa tani.
Mnyika alibainisha kuwa wiki moja kabla ya hapo, Mhando alikwishasaini mkataba mwingine na kampuni ya Camel Oil kwa bei ya sh 1,466,488.80 kwa tani kwamba licha ya mikataba yote miwili kuwa na gharama kubwa zaidi kwa tani kuliko bei ya BP, bado mkataba wa BP ulikatishwa na TANESCO ikaanza kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL kutoka makampuni ya Oryx na Camel Oil.
“Kitu cha ajabu ni kwamba licha ya mikataba ya makampuni ya Oryx na Camel Oil kuonyesha bei za sh 1,501.70. na sh 1,466.49 kwa lita, TANESCO ilianza kununua mafuta ya makampuni hayo kwa sh 1,850 kwa lita,” alisema.
Mnyika aliongeza kuwa kwa maana hiyo, kwa mikataba ya kununua jumla ya lita 16,110,000 kwa mwezi kutoka kwenye makampuni hayo, TANESCO ilikuwa inayalipa sh bilioni 29.8 kwa mwezi. Kwa ulinganisho, mafuta yaliyouzwa na BP kwa mkataba na RITA yaliigharimu Serikali sh bilioni 13.1 kwa bei ya sh 1,460 kwa lita.
“Hii ndio kusema kwamba kama TANESCO ingeendeleza mkataba na BP badala ya kuuvunja, gharama ya mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL ingekuwa sh bilioni 23.5 na hivyo TANESCO ingeliokolea taifa sh bilioni 6.3 kila mwezi,” alisema Mnyika.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment