CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Mbeya kimeendelea kukitesa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kujinyakulia makada wake wanane maarufu katika mtaa wa Soko Mwanjelwa Kata ya Ruanda, akiwemo Katibu mwenezi wa CCM wa kata hiyo, Baraka Mwakyabula.
Makada hao walikabidhi kadi zao za CCM jana kwa Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija, maarufu kama Mzee wa Upako, ambaye pia aliwakabidhi kadi mpya za CHADEMA.
Mbali na Mwakyabula kuwa Katibu Mwenezi CCM Kata ya Ruanda pia alikuwa Katibu wa Hamasa wa Kata, Mjumbe wa Kamati ya siasa tawi la Ruanda, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wilaya ya Mbeya na Mjumbe wa Mbaraza la Wazazi wilaya pamoja na Mwenyekiti wa Mtaa wa Soko Mwanjelwa.
Makada wengine waliorejesha kadi za CCM na kukabidhiwa kadi za CHADEMA ni mabalozi saba waliotoka katika mtaa huo wa soko Mwanjelwa aliokuwa akiuongoza Mwakyabula ambao baadhi yao ni Chifu Adam Makatobe, Maneno Mwakabinga na Chifu Edward Mwakalukwa.
Akikabidhi kadi yake kwa Mzee wa Upako, Mwakyabula alisema kabla ya kuchukua uamuzi huo aliamua kujiuzulu nyadhifa zake zote za ndani ya CCM na serikalini kwa kuandika barua alizozipeleka kwa viongozi wa CCM na Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
“Nimemwandikia barua Ofisa Mtendaji wa Kata ya kujiudhuru, lakini pia viongozi wa CCM wilaya nao nimekwishawapelekea barua ya kujiudhuru nyadhifa nilizokuwa nazo ndani ya chama,” alisema.
Akiwapokea wanachama hao wapya, Mzee wa Upako alisema kupokelewa kwa Mwakyabula ni kusajili timu nzuri katika mapambano ya kisiasa jijini Mbeya na kuwa sasa ndoto za CCM za kutaka kulirejesha jimbo la Mbeya Mjini kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 ambalo kwa sasa linaongozwa na CHADEMA zimeyeyuka.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment