Monday, July 9, 2012
Tume ya Katiba yatoa ufafanuzi wa malalamiko
TUME ya Mabadiliko ya Katiba, imetoa ufafanuzi kuhusu malalamiko ya baadhi ya wananchi kuwa imeweka ukomo wa idadi ya wananchi wanaotoa maoni katika mikutano yake inayoendelea katika mikoa minane nchini.
Pia imewasihi wananchi waendelee kujitokeza kwa wingi katika mikutano inayoitishwa na tume na kutoa maoni yao kwa uhuru na uwazi.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu wa Tume hiyo,Assaa Rashid, ambaye alisema tume haiwezi kuweka ukomo wa idadi ya watu wanaotoa maoni kwa sababu yenyewe inahitaji maoni kutoka kwa kila mwananchi.
Ufafanuzi huo unafuatia taarifa zilizochapishwa na baadhi ya vyombo vya habari zikiwanukuu baadhi ya wananchi, wakidai kuwa tume hiyo imeweka kikomo cha idadi ya na watu na maswali katika kutoa maoni.
Taarifa hizo zilidai kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, imekuwa ikitoa nafasi kumi tu kwa wananchi wanaopaswa kuuliza maswali yasiyozidi kumi katika kila mkutano na kwamba hayo yametokea katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Biharamulo, mkoani Kagera.
Inadaiwa kuwa katika wilaya hiyo, tume imezifikia kata sita u kati ya kata 15.Lakini katika taarifa yake, Rashid alipingana na madai hayo na kusisitiza kuwa katika baadhi ya maeneo, tume imeongeza muda wa mikutano.
“Katika baadhi ya wilaya, kama Kusini Unguja na Bahi mkoni Dodoma, tume imelazimika kuongeza muda wa kupokea maoni ya wananchi na wakati mwingine kuongeza idadi ya mikutano hadi kufikia mitatu badala ya miwili kwa siku. Hatua hizi zinalenga kutoa fursa zaidi kwa wananchi kutoa maoni yao,” alisema Assaa katika taarifa yake kwa vyombo habari.
Kuhusu mikutano iliyofanyika wilayani Biharamulo, Assaa amesema tume ilipanga na imefanya mikutano sita katika kipindi cha kati ya Julai 2 na 4 mwaka huu na kwamba jumla ya wananchi 267 walitoa maoni yao kwa mdomo na wengine 265 walifanya hivyo kwa njia ya maandishi.
Kwa mujibu wa katibu huyo, vituo ambavyo mikutano hiyo ilifanyika ni Kelenge, Movata, Nyamigogo, Runazi, Nyakanazi na Biharamulo mjini.
“Katika mikutano hiyo na mingine, tume haikuweka na haitaweka ukomo wa idadi ya wananchi wanaopaswa kutoa maoni,” alifafanua Assaa na kuongeza kuwa tume inatambua kuwa wananchi wana shauku kubwa ya kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya.
Hata hivyo, Katibu huyo alisema kuwa ingawa tume ingependa kumfikia kila mmoja mahali alipo, jiografia ya nchi na muda ambao tume imepewa, haiwezi kukidhi azma hiyo.
Kuhusu madai kuwa kuwa baadhi ya kata hazitafikiwa, Rashid alisema tume haikupanga ratiba ya mikutano ya kukusanya maoni kwa kuzingatia kata na kwamba imepangwa kwa kuzingatia eneo ambalo linaweza kujumuisha wananchi kutoka zaidi ya kata moja.
Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment