Tuesday, July 3, 2012

TUME YA KATIBA YAANZA KUKUSANYA MAONI


MCHAKATO wa kukukusanya maoni ya Katiba mpya nchini umeanza huku wananchi wakiwa na mawazo tofauti, na baadhi yao wakipendekeza Zanzibar iwe na mamlaka kamili.

Maoni hayo yalitolewa jana katika eneo la Mzuri Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja, ambako pia ilipendekezwa Muungano kati ya Tanzania uwe wa mkataba.

Pia baadhi ya wananchi waliwaeleza wajumbe wa Tume ya Katiba chini ya Mohamed Yussuf, wakitaka ziwepo Serikali mbili kama zilivyo sasa, huku wengine wakitaka Serikali tatu, yaani Tanganyika, Unguja na ya Kisiwa cha Pemba.

Mmoja wa wananchi hao alitaka Zanzibar iwe na mamlaka ndani na nje ya nchi, na iwe na uwezo wa kujiamulia mambo yake inavyotaka, huku akitoa mfano kuwa nchi hiyo imezuiwa kujiunga na Jumuiya ya Kislamu  (OIC) na Shirikisho la Soka la Dunia (Fifa)

“Zanzibar ikiwa na Serikali yake na Tanganyika  Serikali yake, nchi mbili hizi kila moja itakuwa peke yake wala hazitaingiliana, na Muungano wetu utakuwa wa mkataba," alisema mwananchi huyo.

wajumbe 16 waliotoa maoni yao walitaka mfumo uliopo sasa uendelee lakini wakisisitiza kero za Muungano zitatuliwe.

Kwa upande wao, Hasan Ali Othnam na Matona Masoud Issa, mbali na kutaka ziwepo Serikali za Tanganyika na Unguja, pia walieleza Pemba iwe na Serikali yake, na Muungao uwe kati ya Unguja na Tanganyika.

Pia baadhi ya wananchi walitaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania achaguliwe kwa awamu kwa kuachiana nafasi baina ya Bara na Visiwani.

Vile vile wapo waliopendekeza Rais aendelee kuwa na mamlaka ya kuteuwa mawaziri, wakuu wa wilaya ,wakuu wa mikoa na kutaka kati ya viongozi wakuu wa kitaifa, yaani Rais, Waziri Mkuu na Makamu wa Rais mmoja wao awe mwanamke.

Baadhi ya watoa maoni walitaka kuwepo kwa makamu wawili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, moja awe Rais wa Zanzibar, kama ilivyowahi kuwa zamani.

Wajumbe wengine wa Tume ya Katiba waliopo Zanzibar ni Dk Salim Ahmed Salim, Dk Sengendo Mvungi, Kibibi Mwinyi Hasan na Richard  Lyimo
.


Mwananchi

No comments:

Post a Comment