Wednesday, July 4, 2012

Mnyika ataka ufafanuzi juu ya wabunge kudhalilishwa


Mbunge wa Ubungo, (Chadema) John Mnyika, ameomba mwongozo wa Spika, akitaka aelezwe hatua gani atahuchukuliwa Mwenyekiti wa Bunge, Sylivester Mabumba, kwa kitendo cha kuwadhalilisha wabunge wawili alipokuwa akiendesha kikao juzi jioni.
Mnyika aliomba mwongozo huo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama, mara baada ya kipindi cha maswali na majibu mjini Dodoma jana.
Akitumia kanuni ya tano (1) kwamba juzi katika mkutano wa Bunge, Mwenyekiti wa Bunge,  Mabumba (Mbunge wa Dole-CCM), alitoa maneno ya kuwadhalilisha wabunge wawili.
Alimtaja Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, ambaye aliambiwa kuwa anadandia hoja na anajitafutia umaarufu.
Alisema pia Mabumba, alitoa maneno kuwa yeye (Mnyika), ameshindwa kujibu taarifa, jambo ambalo halikuwa ni kweli kwasababu hakupewa nafasi ya kujibu.
Alisema jambo jingine, Mabumba alimwambia kuwa `anawashwa washwa’, na kwamba hayo maneno yameleta hasira sana kutoka kwa wananchi wake wa jimbo la Ubungo kwa kuwa wameona kuwa wamekashfiwa wao.
Alisema na wananchi wa Kasulu Mjini, nao wanaona kuwa wamekashfiwa wao kwa kitendo cha Mbunge wao kutolewa maneno ya udhalilishaji.
Alisema kanuni 64 (2) inatoa nafasi kutoa utaratibu kwa mambo yanayomhusu mbunge mwingine.
Mnyika alisema pia maneno hayo yanakiuka ibara ya sita ya sheria ya maadili ya umma.
Aliomba mwongozo wa Spika, wabunge hao wachukue hatua gani kwa jambo kama hilo.
Kuhusu suala la Mnyika, Mhagama alisema suala hilo atalitolea maamuzi baadaye ama siku atakayoona inafaa.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment