Thursday, July 5, 2012

MZEE Mustafa Jaffer Sabodo achangia tena M4C (CHADEMA) na ahadi zingine za miradi


MFANYABIASHARA maarufu na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mustafa Jaffer Sabodo amekichangia tena Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), sh. milioni 10, huku akitoa ahadi nyingine mpya ya kukipatia chama hicho mradi wa kukiingizia mapato na kuchimba visima kwa majimbo ya chama hicho kwa miaka 10.
Amesema kuwa kazi inayofanywa na chama hicho kutoa elimu ya uraia hadi vijijini, huku kikizidi kuimarisha mtandao wake kwenye ngazi za vitongoji na mitaa kikidhamiria kuendelea kupigania na kutetea haki za wananchi, inapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania mpenda maendeleo.
Mfanyabiashara huyo ambaye amekuwa akijitokeza waziwazi bila uoga kukichangia chama hicho cha upinzani, akisema anafurahishwa na kazi ambayo kinafanya ya kutetea maslahi na rasilimali za Watanzania kutengeneza fursa za maendeleo, ameongeza kuwa amefurahishwa na Operesheni Okoa Kusini, ambayo chama hicho kilifanya karibuni mikoa ya Lindi na Mtwara.
Akizungumza jana nyumbani kwake ambako alikutana na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa kwa ajili ya kuzungumzia mchakato wa utekelezaji wa ahadi alizotoa kwa chama hicho, Mzee Sabodo aliahidi kuwa baada ya kukamilika kwa jengo la kuegesha magari linalojengwa katikati ya Jiji la Dar es Salaam, sehemu ya mapato yatatumika kuchimba visima kwa miaka 10.
Mbali ya sehemu ya mapato kutoka katika jengo hilo la kuegesha magari ambalo linajengwa na Taasisi ya Khoja Shia Ithnasheri Jamaat (KSIJAMAAT), pia Mzee Sabodo alisema kuwa sehemu ya chini ya jengo hilo ambayo itakuwa na maduka, CHADEMA itapatiwa duka moja kama mmoja wa miradi ya kukipatia mapato.
“Mtapata sehemu ya mapato ili kuchimba visima kwenye majimbo yenu kwa miaka kumi…pia mtapata duka pale ili mpate mradi wa mapato. Ili kuharakisha utekelezaji wa ahadi ya visima vile vingine fanyeni survey ninyi wenyewe na mpate mkandarasi, itakuwa sehemu ya gharama ya uchimbaji…hizi milioni 10 mtapata hundi hapa mkafanye kazi za wananchi,” alisema Mzee Sabodo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Slaa, mbali ya kumshukuru na kumpongeza Mzee Sabodo kwa ujasiri wake wa kuendelea kujitoa kusaidia harakati za kupigania haki za wananchi, mabadiliko ya kiutawala na kimfumo nchini, aliahidi kuwa chama hicho kitaendelea kutimiza wajibu wake kwa maslahi ya Watanzania.
“Umekuwa mtu wa msaada mkubwa kwetu, umeendelea kuwatia moyo Watanzania wote wa kila namna kuacha uoga wa kuchangia harakati hizi, kwani lengo letu ni kuwatumikia Watanzania katika kila fursa tunayoipata, ambapo kwa sasa tutaendelea kuisimamia na kuiwajibisha serikali ya CCM ambayo ni dhahiri ielekea mwisho na wananchi wameichoka.
“Nasi tunawaahidi Watanzania wote kuwa tutaendelea kuwatumikia na hatutawaangusha, tunatambua kuwa katika mparanganyiko huu mkubwa, kama ugumu wa maisha, hali mbaya ya uchumi, siasa zinazoyumba, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma na migogoro katika makundi mbalimbali ya kijamii kwa sababu ya uongozi mbovu, CHADEMA linabaki kuwa ndiyo tumaini pekee kwa Watanzania,” alisema Dkt. Slaa.
Dkt. Slaa aliyeambatana na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa CHADEMA, Antony Komu, aliongeza kuwa visima vya ahadi hii mpya kutokana na mapato ya jengo la maegesho ambayo ni tofauti na ahadi za visima vingine alizowahi kutoa mwaka jana na mapema mwaka huu, vitachimbwa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania yenye kero kubwa za maji.
Mbali ya ahadi hizo mpya za jana, Mzee Sabodo na Dkt. Slaa walizungumzia juu ya mchakato wa utekelezaji wa ahadi mbalimbali zingine za mfanyabiashara huyo na kada wa CCM, ambazo amekuwa akitoa kwa CHADEMA mara kadhaa tangu mwaka 2010, zikiwemo za ujenzi wa chuo, uchimbaji wa visima, ofisi za makao makuu ya chama hicho na baiskeli 100 za walemavu.

Tumaini Makene

No comments:

Post a Comment