Friday, July 20, 2012

Mnyika kuwa shahidi kesi ya mauji

MBUNGE wa jimbo la Ubungo, John Mnyika atakuwa ni mmoja wa mashahidi wa Serikali watakaoithibitishia mahakama namna walivyohusika washtakiwa wanaotuhumiwa kumuua Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Kata ya Ndago, Yohana Mpinga (30).

Jeshi la Polisi mkoani Singida, limemefikia azimio hilo baada ya kumhoji Mnyika kwa saa tatu juzi usiku, kuhusiana na tukio hilo la mauaji lililotokea baada ya mkutano wake wa hadhara uliofanyika Julai 14 mwaka huu, majira ya jioni.

Mahojiano hayo yaliyoanza saa 11.53 jioni na kumalizika saa 3:15 usiku, yaliendeshwa chini ya kikosi maalum cha askari wa upelelezi kutoka jijini Dar es Salaam kwenye ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoani hapa.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana zilithibitisha kwamba Jeshi la Polisi lilimtaka Mnyika awe tayari kuitwa wakati wowote ili kusaidia kwenye kesi hiyo ya mauaji.

Tayari watu 18 wametiwa mbaroni, miongoni wakiwemo wanachama wa Chadema, kwa tuhuma za kuhusika kwenye mauaji ya kijana huyo wa CCM.


Mnyika alihojiwa huku akiwa na wakili wa Chadema na mbunge wa jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Mauaji hayo ya mwenyekiti wa UVCCM yalifanyika Julai 14 mwaka huu saa 10 jioni huko katika kijiji cha Nguvumali kata ya Ndago jimbo la Iramba magharibi.

Mauaji hayo yanadaiwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na vurugu zilizotokea kwenye mkutano wa hadhara ambao Mnyika alikuwa mgeni rasmi.

Katika hatua nyingine, mshauri na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Kitila Mkumbo, ambaye alikuwa ameambatana na Mnyika, alitarajiwa pia kuhojiwa kuhusiana na mauaji hayo jana.



Mwananchi

No comments:

Post a Comment