Friday, July 20, 2012

Kigogo mwingine Chadema mahakamani leo


Kiongozi mwingine wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amehojiwa na Polisi juu ya vurugu zilizotokea katika mkutano wa chama hicho na kusababisha Mwenyekiti UVCCM Kata Ndago, wilayani Iramba, Mkoani Singida, Yohana Mpinga kupoteza maisha.

Aliyehojiwa na kuachiwa kwa dhamana ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC), Mkumbo Kitila na alitakiwa kurejea Polisi leo asubuhi, kwa ajili ya kupelekwa mahakamani.

Kamanda wa Polisi Mkoa Singida, Linus Sinzumwa, alisema jana kuwa Kitilah atapandishwa kizimbani kwa kosa la kutoa lugha ya matusi kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika Jumamosi iliyopita.

“Kitila tumehoji na yupo nje kwa dhamana na tunatarajia kumfikisha kesho (leo) mahakamani…anakabiliwa na tuhuma hizo hizo za kutoa lugha ya matusi,” alisema Sinzumwa.

Juzi jeshi hilo lilimhoji mkurugenzi Habari na Uenezi wa Chadema ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo John Mnyika kwa saa tatu, kuanzia saa 12 jioni, kabla ya kumwachia huru.

Kuhusu kuhojiwa kwa Mnyika, Kamanda Sinzumwa alisema aliachiwa huru baada ya kuridhika na maelezo yake, lakini wakimhitaji watamwita tena, kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Kiongozi wa kwanza kuhojiwa kuhusiana na vurugu hizo alikuwa Ofisa Sera na Uratibu wa Chadema, Mwita Waitara, ambaye ameshafikishwa mahakamani kwa kosa la kutoa lugha ya matusi dhidi ya Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba.

Kutokana na hali hiyo, Kitila ataunganishwa katika kesi hiyo, kuhusiana na vurugu zilizotokea Mkutano wa Chadema uliofanyika Ndago, Iramba Mkoani Singida.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

  1. Ni lini MH Lusinde mbunge wa Mtera atafikishwa Mahakamani kwa kosa la kutukana matusi ya nguoni wakati wa kampeni huko Arumeru?

    Ni lini MH Mwigulu Nchemba muweka hazina wa CCM na mbunge atafikishwa mahakmani kwa kosa la kutoa lugha ya matusi katika kampeni Igunga na Arumeru?

    Kwa nini Serikali ya CCM kupitia Jeshi lake la Polisi imeweza kuwachulia hatua viongozi wa CHADEMA wakati huo huo haiwafungulii mashitaka viongozi wa CCM kwa makosa hayo hayo?

    ReplyDelete