Neville Meena na Florence Majani, Dodoma
MBUNGE wa Ubungo (Chadema), John Mnyika jana alimrushia kombora Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba akimtaja kwamba ni mmoja wa watuhumiwa wa wizi wa Sh133 bilioni za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), uliotokea ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).Kombora hilo dhidi ya Nchemba ambaye pia ni Mweka Hazina wa CCM, lilisababisha mabishano ya hoja kwa dakika 20.
Mnyika alirusha kombora hilo baada ya Nchemba kuchambua bajeti kivuli ya upinzani kuhusu Ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Uhusiano) na kukosoa baadhi ya maneno, ikiwamo kusema walimu wanafanya biashara shuleni na wahadhiri wanafundisha madarasa ya pembeni, kitu alichosema ni udhalilishaji kwa wanataaluma hao kwa kuwa si wote wanaofanya hivyo.
Nchemba alisema kuwa, hotuba ya wapinzani ni ya uchochezi akinukuu katika ukurasa wake wa 27 inasema: “Walimu wote wa shule za msingi hufanya biashara shuleni wakati wa masomo na wahadhiri katika vyuo vikuu vya umma hufanya kazi za muda katika vyuo vingine tofauti na kule walikoajiriwa.”
“Kiti chako Mheshimiwa Mwenyekiti na kwa heshima ya Bunge hili, kitoe maelekezo, agizo au ushauri kwenye baadhi ya maneno yaliyopo katika hotuba ya kambi ya upinzani yaliyojaa uchochezi na udhalilishaji kwa baadhi ya kada za Watanzania,” Alisema.
Alisema hotuba hiyo imewadhalilisha watu wa kada hizo na kuwa si kuwa walimu wote hufanya kazi hizo na badala yake hotuba hiyo ingesema baadhi ya walimu.
Wakati Nchemba akiendelea kuchangia Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Sabreena Sungura alisimama na kuomba kutoa taarifa kwa mujibu wa Kanuni 64(1), akisema kuwa taarifa za Nchemba hazikuwa za kweli: “Mzungumzaji aliyepita amezungumza maneno yasiyo ya kweli kwani hotuba hiyo haijasema walimu wote, bali imesema kwa mfano na akitaka kupewa data basi atapewa.”
Baada ya taarifa hiyo ya Sungura, Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama alimtaka Nchemba athibitishe maneno yake hayo ambayo alikuwa ameyatoa katika bajeti hiyo kivuli.
Hata hivyo, Nchemba aliposimama tena alisema: “Namuomba Mbunge (Sungura) arudi darasa la kwanza akajifunze kusoma maana mimi nimenukuu kitabu cha wapinzani.”
Maneno hayo ya Mwigulu yalimwamsha kwenye kiti Mnyika ambaye aliomba mwongozo kupitia Kanuni namba 64 (Vifungu vya A, F na G), ambavyo haviruhusu mchangiaji kusema maneno yasiyo na ukweli na kutumia lugha ya kuudhi.
Mnyika alisema kwamba, kipengele hicho kinamkataza mchangiaji kumsema vibaya mbunge na amevunja kanuni nyingine kwa kutumia lugha ya kuudhi kwa kumwambia arudi darasa la kwanza.
Baada ya Mnyika kuomba mwongozo, Mwenyekiti Mhagama alimtaka Mwigulu afute kauli hiyo. Alifanya hivyo na kuendelea kuchangia hoja.
Wakati akiendelea kuchangia, Nchemba aligeukia kipengele kingine cha hotuba hiyo kivuli hususan kilichozungumzia kutokuwa na ufanisi kwa Idara ya Usalama wa Taifa na kusema hotuba hiyo imeidhalilisha idara hiyo: “Usalama wa Taifa ni eneo nyeti katika nchi hii na hautakiwi kufanya kazi kama trafiki.”
Kauli hiyo ilisababisha Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema) , Mchungaji Peter Msigwa kusimama na kuomba mwongozo na kumtaka Nchemba asome aya nzima kuhusu suala hilo badala ya kusoma kipengele kimoja kwa lengo la kupotosha.
“Ninamuomba mchangiaji aangalie ‘context’ badala ya kuangalia sentensi moja katika aya yenye mambo lukuki. Anajaribu kuupotosha umma kwa kutoka nje ya muktadha. Nina shaka na elimu yake na uelewa wake,” alisema Msigwa.
Hata hivyo, Mhagama alikataa kutoa mwongozo kwa hoja ya Msigwa kwa maelezo kwamba katika kuuliza kwake hakuzingatia kanuni husika: “Tunachogombana mimi na wewe Mheshimiwa Msigwa ni matumizi ya kanuni tu.”
Baadaye Mnyika alipata nafasi nyingine, ndipo aliporusha kombora hilo akisema Nchemba anajua mantiki ya kilichoandikwa katika hotuba ya kambi ya upinzani kuhusu idara hiyo na wala haijadhalilishwa isipokuwa imeshindwa kuzuia ufisadi kama wa EPA ndani ya BoT.
Mnyika alisema Nchemba ni miongoni mwa watuhumiwa wa wizi huo wa EPA kwani aliwahi kuwa mfanyakazi wa BoT wakati ukitokea na kusisitiza: “Wewe mwenyewe (Nchemba) ni mtuhumiwa wa EPA.”
Alisema watumishi wa Usalama wa Taifa wanatoa taarifa lakini, wakubwa wao hawazifanyii kazi... “Ninamuomba Mbunge aache propaganda kwani na yeye ni mmoja wa watuhumiwa,” alisema Mnyika.
Kombora hilo la Mnyika lilimsimamisha kitini Mwenyekiti Mhagama ambaye alimtaka atoe uthibitisho wa madai yake hayo bungeni katika muda wa siku saba kuanzia jana. Mnyika aliahidi kufanya hivyo akisema ataorodhesha tuhuma zote zinazomhusu.
Pia wakati Nchemba akiendelea kuchangia alisema kuwa, ameingia BoT mwaka 2006 na kwamba wakati wizi huo ukitokea alikuwa chuoni.
“Kwa taarifa ya utangulizi tu ni kwamba, wakati hayo yakitokea nilikuwa niko chuoni na nilikuwa sijaujua mlango wa Benki Kuu na nimeingia mwaka 2006 wakati wizi huo umetokea mwaka 2005,” alisema.
Simbachawene ampa somo Mhagama
Kuendelea kwa mivutano ndani ya Bunge, jana kulimfanya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene kusimama na kumweleza Mwenyekiti Mhagama kuwa kanuni anazozisimamia zinavunjwa na kusababisha wabunge kuhama kwenye mjadala.
Simbachawene ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri alikuwa Mwenyekiti wa Bunge, alisimama kwa kutumia Kanuni ya 65 na kusema kuwa, Kanuni za Bunge tangu juzi zimekuwa zikivunjwa kiasi cha kufanya mjadala uhame na kunafanya Bunge lisiwe la viwango.
“Mwenyekiti hili suala la mtu kusimama kila wakati linafanya Bunge lako kushuka viwango. Naomba utumie kanuni kusimamisha hilo,” alisema Simbachawene. Baada ya kumaliza Mhagama alikubaliana na hoja hiyo na kusema kwa kutumia Kanuni ya 5(1) anafunga mijadala yote.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment