Thursday, July 5, 2012

Mnyika akata rufaa mgomo wa madaktari


MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amekataa rufaa dhidi ya maamuzi ya Spika, Naibu Spika na wenyeviti ya kukataa kuruhusu Bunge kutumia uhuru na mamlaka yake kwa mujibu wa Katiba ya nchi; sheria ya haki, kinga na madaraka ya Bunge na kanuni nyingine za Kanuni za Kudumu za Bunge kuhusiana na mgomo mkubwa wa madaktari.
Mnyika alisema amelazimika kufanya hivyo, baada ya kutojibiwa kwa barua zake mbili alizomwandikia Spika ili arekebishe miongozo iliyotolewa awali kuliwezesha Bunge kujadili hali ya huduma za afya nchini, jaribio la mauaji ya Dk. Ulimboka Steven na kushughulikia chanzo cha mgogoro unaoendelea kati ya serikali na madaktari wenye athari kwa nchi na maisha ya wananchi.
“Ikumbukwe kwamba tarehe 27, 28, na 29 Juni 2012, na tarehe 2, 3 na 4 Julai 2012 kwa nyakati mbalimbali kumetolewa miongozo, maamuzi, majibu na Mheshimiwa Spika Anne Makinda, Mheshimiwa Naibu Spika Job Ndugai na Waheshimiwa wenyeviti wa Bunge Sylvester Mabumba na Jenister Mhagama kwamba suala la madai ya madaktari na mgogoro uliotokana na madai hayo hayapaswi kujadiliwa bungeni kwa kuwa kanuni ya 64 (1) (c) ya kanuni za Bunge toleo 2007 inamkataza mbunge kuzungumzia jambo lolote ambalo linasubiri uamuzi wa mahakama,” alisema.
Mbunge huyo alisema sababu kubwa zilizomsukuma kukata rufaa ni kuonesha kuwa kesi iliyopo mahakamani imefunguliwa dhidi ya Chama Cha Madaktari (MAT) na si Jumuiya ya Madaktari nchini pamoja na vyama vingine vya watumishi na wataalamu katika sekta ya afya na masuala mengine ya sekta husika.
“Aidha, ukiondoa suala la madai ya madaktari ambayo ni kati ya hoja zilizo mahakamani masuala mengine yanayoendelea si sehemu ya madai yaliyopo mahakamani, mathalani hali ya hivi sasa ya kudorora kwa huduma katika hospitali za umma nchini na jaribio la mauaji ya Dk. Ulimboka Steven. Hivyo, Spika kukataza masuala husika ni kinyume na kanuni 5 (1) na ni kuingilia masharti ya ibara ya 100 ya katiba ya nchi yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika Bunge.
“Waziri Mkuu alilieleza Bunge kuwa Serikali imejipanga kuziba pengo kwa kupeleka madaktari kwenye hospitali za rufaa kutoka wizarani, kurejesha madaktari wastaafu,  kupeleka wagonjwa wa rufaa katika hospitali za Jeshi na kupunguza idadi ya wagonjwa wa rufaa kutoka hospitali za wilaya na mikoa’ alisema.
Alisema hata kitendo cha Rais Kikwete kuzungumzia suala hilo katika hotuba yake kwa taifa ya 30 Juni 30, 2012 , na kauli ya viongozi wa madaktari ikiwemo madaktari bingwa kwamba Rais alipotoshwa na timu aliyoituma kufanya majadiliano na madaktari, zinaashiria kwamba bado mgogoro huo unaendelea.
Aliongeza kuwa masuala yanayosubiri uamuzi wa mahakama ambayo yamewekewa masharti kwa mujibu wa kanuni 64 (1) (c) yanaweza kuruhusiwa kujadiliwa bungeni kwa muongozo na utaratibu utakaowezesha majadiliano kufanyika bila kuingilia uhuru wa mahakama kwa kuzingatia kanuni ya 5 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.
“Nimemjulisha Katibu wa Bunge kuwa niko tayari kuwasilisha maelezo na vielelezo zaidi wakati malalamiko yatakapokuwa yanajadiliwa na kikao cha Kamati ya Kanuni, hata hivyo kwa maelezo ya awali nimeiomba kamati irejee nyaraka toka maktaba ya Bunge la Uingereza ambalo lina utaratibu kama wetu wa kibunge,” alisema.
Kuhusiana na jaribio la mauaji ya Dk. Ulimboka Steven, mbunge huyo alisema uchunguzi unaofanywa na jopo lililoundwa na askari polisi pekee hauwezi kuaminika na hivyo Bunge kujadili na kupitisha maazimio ya kuweza kusuluhisha pande mbili za mgogoro badala ya mahakama ambayo mchakato wake utachukua muda mrefu kukamilika huku wananchi wakiendelea kuathirika.
Uamuzi wa kurejea mahakamani unapaswa kuwa wa mwisho baada ya hatua nyingine kushindikana.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment