MBUNGE wa Maswa Mashariki, Sylvester Kasulumbai (CHADEMA), na kada wa chama hicho, Robert William, wamehukumiwa kifungo cha miezi saba jela au kulipa faini ya sh 250,000 baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili ya jinai.
Adhabu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Tabora, Thomas Simba, muda mfupi baada ya kumwachilia huru mbunge wa Viti Maalum wa chama hicho, Suzan Kiwanga, na mwanachama mwingine, Anwaryn Kashaga.
Kasulumbai na mwenzake walifungwa pingu na kupelekwa katika mahabusu ya mahakama kitendo ambacho kililalamikiwa na wakili Mbogolo kwamba ni cha udhalilishaji na uvunjaji wa haki za binadamu.
“Unakifurahia kitendo unachokifanya? Alisikika Kasulumbai akimuuliza askari polisi aliyemvika pingu mara baada ya hukumu hiyo kutolewa.
Akisoma hukumu ya kesi hiyo, hakimu Simba alisema kuwa hii ni sawa na kesi nyingine zinazowakabili watu wengine kwamba mbunge huyo atakwenda jela miezi mitatu kwa kutoa lugha ya matusi au kulipa faini ya sh 50,000.
Pia aliwahukumu washtakiwa hao kwenda jela miezi minne au kulipa faini ya sh 100,000 baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la shambulio liletalo madhara mwilini.
Hakimu Simba vile vile aliwataka washtakiwa hao kumlipa fidia ya sh 2,000,000 mlalamikaji Fatuma Kimario, ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga.
Washtakiwa wote walilipa faini hiyo na kuachiliwa huru huku wakibaki kusubiri kulipa fidia hiyo ya sh milioni moja kila mmoja.
Awali upande wa mashtaka ulidai kuwa washtakiwa wote walitenda makosa hayo Septamba 15 mwaka jana, katika Kijiji cha Isakamaliwa wilaya ya Igunga.
Mara baada ya kuachiliwa huru, Kiwanga na Kashaga walitoka nje na kutimua mbio jambo lililowafanya watu waliokuwepo mahakamani hapo kuwashangaa.
Mapema wakili wa utetezi, Edson Mbogolo, aliiomba mahakama itoe adhabu ndogo kwa wateja wake kwa vile ni wakosaji wa mara ya kwanza na kwamba Kasulumbai (62) ana watoto 27 na wake watatu wanaomtegemea.
“Mahakama izingatie kwamba Kasulumbai ni mwakilishi wa wananchi na endapo akipewa adhabu ya kifungo, jimbo lake litakuwa wazi na hivyo litaigharimu serikali kuitisha upya uchaguzi,” alisema Mbogolo.
Makosa mengine yaliyokuwa yakiwakabili washtakiwa hao ni kumweka chini ya ulinzi isivyo halali kwa mujibu wa sheria Mkuu huyo wa Wilaya, huku kosa la nne ni wizi kutoka maungoni ambalo halikuweza kuthibitishwa na hivyo kufutwa na mahakama.
Wakati huo huo, mshauri wa chama hicho ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitila Mkumbo, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya mjini Singida akikabiliwa na tuhuma za kutoa lugha ya matusi kwa mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM).
Dk. Mkumbo ameunganishwa katika kesi hiyo pamoja na ofisa wa sera na utafiti wa CHADEMA Mwita Mwikwabe (37) ambaye alisomewa pia shitaka hilo Julai 16mwaka huu.
Awali Mwanasheria wa serikali, Maria Mudulugu alidai kwamba Julai 14 mwaka huu, saa 10 jioni, mshtakiwa huyo alitoa lugha ya matusi kwa Mwigulu kuwa ni malaya na mzinzi huku akijua wazi kwamba kitendo hicho ni kinyume cha sheria.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Ruth Masamu, mwanasheria huyo alidai kuwa mshtakiwa alitoa lugha hiyo ya matusi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya kituo cha mabasi Kijiji cha Nguvumali, Kata ya Ndago.
Dk. Mkumbo alikana shitaka hiko na yupo nje kwa dhamana hadi Julai 30 mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.
Nao wakazi wawili wa Kijiji cha Nguvumali, Kata ya Ndago, Paulo Nashokigwa (27) na Emanuel Shila (24), wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya mjini hapa wakikabiliwa na tuhuma za kushiriki kumuuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Yohana Mpinga (30).
Mwanasheria huyo wa serikali alidai kuwa Julai 14 mwaka huu, saa 10 alasiri katika Kijiji cha Nguvumali, Kata ya Ndago, washtakiwa wote kwa pamoja wakitumia fimbo na mawe, walimpiga Yohana na kumsababishia kifo.
Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa vile Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji. Na wameunganishwa na washtakiwa wengine 12 waliosomewa shitaka lao la mauaji Julai 16 mwaka huu, kesi hiyo itatajwa Julai 30 mwaka huu.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment