MADIWANI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilayani Arusha wamechafua hali ya hewa kwa kususia uchaguzi wa Naibu Meya Halmashauri ya Manispaa ya Arusha, kitendo kilichosababisha uchaguzi huo kukwama kwa mara nyingine.
Hatahivyo, katika hali isiyo ya kawaida baadhi ya maofisa wa Usalama wa Taifa pamoja na askari wa Jeshi la Polisi wakiwa na magari yao, jana walionekana kwa wingi wakirandaranda nje na ndani ya ofisi hizo kitendo kilichoibua maswali mengi.
Akifungua kikao cha Baraza la Madiwani kabla ya kuanza kujadili ajenda mbalimbali za kikao hicho, Meya wa Jiji hilo, Gaudence Lyimo alisema anashangaa ni kwa nini madiwani wa Chadema wasusie kikao hicho wakati walikubali mwafaka na kumtambua yeye kama meya.
Pia, alisema awali madiwani hao walikubali mwafaka ili wawaletee
maendeleo wananchi lakini alihoji watu hao hao waliokubali mwafaka leo hii kususia vikao na kumtishia maisha huku wengine wakisema hawamtambui yeye kama meya.
Lyimo, alisema kuwa kikao hicho kilikuwa na ajenda tatu muhimu ambazo ni kuchagua wenyeviti wa kamati mbalimbali, kupitia taarifa za mapato na matumizi pamoja na uchaguzi wa Naibu Meya, ambaye alitakiwa kutoka Chadema, lakini cha ajabu chama hicho hawajaleta jina wala kuhudhuria kikao hicho.
Alisema kutokana na madiwani wa Chadema ambao ni saba kususia kikao hicho walikubaliana na madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuachana na ajenda hiyo mpaka kikao cha dharura kitakapoitwa kujadili suala hilo.
“Kikao hiki kina washiriki 23 ambapo watano kati yao ni wabunge na 18 ni madiwani, ila kwa leo wapo madiwani 12, tumefika nusu ya kolamu, ila madiwani wa Chadema wameandika barua na kueleza sababu zao za msingi za kususia kikao hiki kuwa wanataka uchaguzi wa Meya ufanyike tena na kuitaka Serikali kukubali uchaguzi urudiwe ili apatikane Meya halali ndipo wao washiriki,” alisema Lyimo.
Alisema barua hiyo waliyoandika Chadema na kuipeleka kwa
Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha, pia ilikuwa na ikitishia maisha watu iwapo hawatafanya uchaguzi wa Meya, jambo ambalo siyo halali.
Alisema kuwa, anakishangaa chama hicho, iwapo kama wameona
hawakutendewa haki, mahakama ndiyo sehemu ya kukimbilia, ambako hawataki kwenda badala yake wanagoma na kuwatishia watu maisha na kusisitiza ni Mungu pekee ndiye anayekuwa mlinzi wa watu aliyewaumba.
Lyimo alisema, anakumbuka walifanya kikao Juni 20 mwaka jana 2011 na pande hizo mbili na kukubaliana mwafaka na kuwapa nafasi ya Naibu Meya Chadema, ila anashangaa kuona wamegeuka makubaliano hayo.
Alisema kikubwa kilichopo ni kuwaletea wananchi maendeleo na siyo kulumbana, kwa sababu hawakuchaguliwa kuendesha malumbano.
Upande wa madiwani wa CCM, wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Olasiti, Ismail Katamboi alisema kuwa, kwa sababu Chadema wamekataa kuleta jina la Naibu Meya wamevunja kanuni na maazimio ya mwafaka wao ambao walikaa na kupongezana basi iwekwe katika kikao kijacho kama ajenda na watoe uamuzi wao.
Hali hiyo ilimlazimu, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Omary
Mkombole kusimama na kuingilia kati na kuwataka madiwani kuacha kujadili suala hilo kwani siyo kikao cha kujadili suala la mwafaka na kushauri madiwani hao kujadili suala hilo kikao kijacho kitakachoitwa kwa dharura.
Naye mwenyekiti wa Madiwani wa Chadema, Isaya Doita, alitoa tamko kwa niaba ya madiwani wenzake saba kuwa hawatashiriki uchaguzi wa Naibu Meya kwa kuwa uongozi wa chama hicho ngazi ya Wilaya ya Arusha uliandika barua Julai 14 mwaka huu, yenye kumbukumbu nambari MD/E40/10/VOL 11 kwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo wakimtaarifu kutoshiriki uchaguzi huo na kumtaka aitishe kikao cha uchaguzi wa Meya wa Arusha.
Alisema Chadema hawawezi kuteua mtu kwa nafasi ya Naibu Meya wakati hawatambui na kutaka uchaguzi wa meya ufanyike kwa kuwa manispaa hiyo haina meya kwa sababu aliyepo alichaguliwa kinyume cha sheria.
Doita alisema, baada ya kupeleka barua hiyo Ofisi ya Mkurugenzi Arusha ilipokewa na Julai 16 mwaka huu, ilijibiwa na Kaimu Mkurugenzi, Mkombole ambaye alisema kuwa kuhusu marudio ya uchaguzi hayuko tayari kwa sababu ofisi yake inatambua kuwapo kwa meya aliyechaguliwa kihalali kwa kufuata taratibu zote za kuendesha vikao.
Alieleza kwamba, barua hiyo ilisema uchaguzi wa meya ulifanyika Desemba 17 na 18 mwaka 2010 ulifuata sheria na kanuni zote za manispaa na hivyo meya aliyepo kwa sasa ni halali.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment