Tuesday, July 17, 2012

CHADEMA yaonya vurugu za CCM Singida


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeeleza kukerwa na vurugu za Chama cha Mapinduzi (CCM) za kuvamia mikutano yao ya hadhara mkoani hapa.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CHADEMA ambaye pia ni mbunge wa Ubungo, John Mnyika, wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Ndago jimboni Iramba Magharibi, akisema kuwa kamwe hawatavumilia mbinu hiyo chafu ya CCM.
Alisema mbinu hiyo ya CCM kuwapiga watu mawe kwenye mkutano wa CHADEMA haivumiki na badala yake inachochea zaidi harakati ili kuikomboa nchi ambayo inakabiliwa na matatizo mengi ya kutisha yaliyochangiwa na udhaifu wa chama tawala.
Alisema wakati wowote kuanzia sasa, viongozi wa ngazi za juu wa CHADEMA watafanya ziara ya nguvu kwenye kata zote za mkoa wa Singida.
“Mmetuchokoza, hatutakubaliana na viongozi wasanii na wachumi wanaopanga mambo ya kipuuzi kama haya ya kupiga watu mawe wasio na hatia yoyote.  Jiandaeni na kusanyeni mawe mengi ya kutosha, tunakuja na tutakaba kila kona,” alifafanua.
Mnyika alisema amefarijika kufika kwenye jimbo hilo linaloongozwa na Mwigulu Mchemba (CCM) kwa madai kuwa amekuwa ‘akichonga’ sana propoganda bungeni wakati hakuna chochote cha maendeleo amekifanya.
Kauli ya Mnyika ilikuja baada ya kutokea vurugu za watu kupigwa mawe kwenye mkutano huo wa hadhara na CHADEMA wamekana kuhusika na vurugu hizo zilizosababisha kifo cha mfuasi wa CCM.
Afisa wa sera na utafiti wa CHADEMA,Waitara Mwita, alisema kuwa  katika mkutano huo halali, baada ya kuona hali sio nzuri za wafuasi wa CCM kuvamia mkutano huo kwa kurusha mawe na maneno ya kejeli alimpigia siku Kamanda wa Polisi kuomba ulinzi katika eneo hilo.
“Nashukuru RPC aliwasiliana na OCD na mara moja gari la polisi lilifika na askari, lakini licha ya hali kuendelea takriban mara tatu, ilitulazimu kufungua jalada polisi NDG/RB/190/2012 na tulitaja baadhi ya majina ya vijana 12, lakini OCD hakuweza kuwadhibiti vijana waliokuwa wakifanya vurugu hizo,” alisistiza Mwita.
Hata hivyo mara baada ya Waitara kuzungumza na waandishi wa habari, alifika OCD wa Wilaya ya Singida, na kumtaka kufika kwa RPC kwa mahojiano zaidi juu ya tukio hilo.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment