Friday, June 29, 2012

Wananchi, wasomi walaani kujeruhiwa Dk. Ulimboka


Wasomi na wananchi wameishauri serikali kutumia busara badala ya mabavu kutatua mgogoro kati yake na madaktari ili kuepusha uwezekano wa watu wengi kupoteza maisha kwa kukosa matibabu.

Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti jana jijini Dar es Salaam, walisema mvutano unaoendelea kati ya serikali na madaktari unapaswa kutatuliwa mapema ili kunusuru maisha ya Watanzania.

Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alipendekeza serikali iyafanyie kazi mahitaji muhimu ya madaktari kuliko kuendelea na mvutano.
“Hakuna haki ya mtu iliyo kubwa zaidi kuliko haki ya kuishi, serikali na madaktari wanapaswa kutimiza wajibu wao kunusuru maisha na afya za Watanzania,” alisema Dk. Bana. 

Alisema haki iendane na wajibu wa kila mfanyakazi, hivyo madaktari wadai haki zao huku wakiendelea kutoa huduma kwa wagonjwa.

Naye Mhadhiri Msaidizi katika Idara ya Historia chuoni hapo, Iddy Magoti, alishauri serikali kutafuta mbinu za kutatua tatizo hilo badala ya kukimbilia kulizima kwa kutoa vitisho.

“Huwezi kutatua tatizo kubwa kama hili kwa vitisho vya kuwafukuza kazi madaktari ilhali ukitambua huna wataalam wa kutosha wa kuziba nafasi zitakazoachwa wazi,” alisema Magoti.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa shahada ya kwanza chuoni hapo, Jovin Jonathan, alisema serikali na madaktari wazungumze ili kumaliza tatizo hilo mapema maana wanaoteseka kwa kukosa huduma za afya ni wananchi wenye kipato cha chini.

Wakati huo huo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimelitaka Jeshi la Polisi nchini kutofungamana na upande wowote katika utatuzi wa mgogoro huo.

Kituo hicho pia kimewaomba wataalamu wa afya nchini kuendelea kufuatilia haki zao kwa utaratibu wa kisheria.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment