JUMLA ya madaktari 83 wamefukuzwa kazi katika Hospitali ya Rufaa Mbeya na ile ya mkoa wa Dodoma kwa madai ya kukaidi agizo la Mahakamu Kuu lililowataka wasitishe mgomo wao.
Mkoani Mbeya, Kaimu Mkuu wa Mkoa huo Nomani Sigala alitangaza kufukuzwa kwa madaktari 72, ambao wamekuwa katika mgomo huo licha ya agizo la serikali na amri ya mahakama ya kusitisha mgomo huo hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa maamuzi.
Katika tamko lake kwa waandishi wa habari jana, Sigala alisema bodi ya wakurugenzi wa hospitali hiyo, imeamua kuchukua uamuzi huo kutokana na kukaidi kwa madaktari hao.
Kati ya madaktari waliofukuzwa, 18 ni wa ajira ya kudumu, huku 54 wakiwa ni walioko katika mafunzo.
Sigala alisema kuwa Juni 23 mwaka huu madaktari 15 tu walikuwa zamu na Juni 24 wafanyakazi 19 kati yao 15 wa mafunzo na wanne wa ajira hawakufika hospitalini na hapo ukawa mwanzo wa mgomo.
Alidai kuwa madaktari hao walikataa kukutana hata na mwenyekiti wa bodi kwa ajili ya majadiliano.
Alisema kuwa baada ya kuona madaktari hao wamekataa kuitikia wito wa kukaa na kusitisha mgomo kutokana na amri ya mahakama, bodi imeamua kuwarudisha madaktari wote 54 wa vitendo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili kuchukua hatua zaidi na usitishaji huo ulianza jana.
Kwa madaktari 18 walioajiriwa, Kaimu Mkuu huyo wa mkoa alisema wameshawaandikia barua za kusimamishwa kazi kwao katika hospitali ya Rufaa Mbeya na kurudishwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa hatua zaidi za kinidhamu.
Kuthibitisha Tanzania Daima ilifika katika hospitali na kukuta madaktari wa mafunzo wakifungasha mizigo yao tayari kwa kuondoka katika hosteli za hospitali huku askari kanzu wakiwasimamia.
Mkoani Dodoma serikali imewasimamisha madaktari 11 wa mafunzo na vitendo kutokana na kuendelea na mgomo.
Mwenyekiti wa Kamati Jumuiya ya Madaktari Mkoa humo Dk. Cassian Mkuwa alithibitishia Tanzania Daima kufukuzwa kwa madaktari hao, na kwamba tukio hilo lilitokea jana asubuhi wakati wakiwa hospitalini hapo wakiendelea na mgomo wao.
Alisema Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dk. Ezeliel Mpuya aliwaita madaktari wote walio katika mafunzo kwa nia ya kuzungumza nao, lakini walipofika alitoa barua kwa madaktari 11 na kudai kuwa wamesimamishwa kazi kuanzia jana kutokana na mgomo.
Hata hivyo madaktari hao waliosimamishwa kazi walikataa kupokea barua hizo licha ya kutakiwa kuondoka katika eneo la hospitali.
Dk. Mkuwa akiwa mmoja kati ya waliofukuzwa alisema anashindwa kuelewa ni vigezo gani vilitumika kuwapata madaktari hao 11 na kuwasimamisha kazi kwani waliogoma ni zaidi ya madaktari 20.
“Mimi nashangaa yeye alitumia vigezo gani kutufukuza na kwanza sisi hatukuingia mkataba na yeye sasa anatufukuza kama nani?’’ aliuliza.
Aidha Dk. Mkuwa alisema tayari wameshatuma taarifa kwa Kamati Kuu ya Jumuiya hiyo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya hatua zaidi.
Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dk. Ezekiel Mpuya alisema kama madaktari wamegoma, hawana sababu ya kuwepo katika eneo hilo.
Hata hivyo, Dk Mpuya hakutaka kuzungumza zaidi kuhusiana na sakata hilo, badala yake alisema kama madaktari wenyewe wamezungumza hakuna haja ya yeye kuongeza kitu.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment