Saturday, June 30, 2012

Polisi Tanzania itakamata madaktari wanaogoma



Jeshi la polisi nchini Tanzania limesema Ijumaa kuwa litaanza kuwakamata madaktari wanaoshiriki katika mgomo wa madaktari nchini humo kwa sababu wanakiuka amri ya mahakama.
Serikali ya Tanzania kupitia kwa mwanasheria mkuu wa serikali iliweka pingamizi siku moja kabla ya madaktari hao kuanza mgomo Juni 23 kuzuia mgomo huo. Lakini hata hivyo mgomo huo umekuwa ukiendelea kwa zaidi ya wiki moja sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari Ijumaa jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo Paul Chagonja alisema jeshi la polisi lina kila sababu ya kuwakamata madaktari wanaogoma. Alisema kama madaktari hawakukubaliana na pingamizi ya serikali walikuwa na haki ya kukata rufaa sio kuendelea na mgomo.
Katika habari nyingine madaktari wanasema Dr. Steven Ulimboka ambaye alitekwa na kupigwa na watu wasiojulikana mapema wiki hii anahitaji kufanyiwa vipimo zaidi nje ya nchi.
Wakati huo huo, madaktari bingwa wa serikali za umma Ijumaa walitangaza kujiunga na mgomo kupinga kupigwa kwa Dr. Ulimboka. Jeshi la polisi limeunda tume watu watano kufanya uchunguzi wa mkasa wa Dr. Ulimboka lakini tume hiyo imepingwa na wengi ikiwa ni pamoja na madaktari wenyewe.


Chanzo - Voice of America

No comments:

Post a Comment