HALI ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Nchini, Dk. Steven Ulimboka, juzi usiku ilibadilika na kuwa tete kiasi cha kuwatia wasiwasi madaktari wanaomtibu.
Baadhi ya madaktari wanaomhudumia mwenyekiti huyo wameiambia Tanzania Daima jana kuwa Dk. Ulimboka hali yake ilibadilika ghafla juzi usiku na hivyo kulazimika kumfanyia uchunguzi mpya na kumwongezea uangalizi.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya jengo la Kitengo cha Mifupa (MOI) cha Hospitali ya Taifa Muhimbili kiongozi wa jopo la madaktari wanaomtibu Ulimboka, Profesa Joseph Kihamba, alisema uchunguzi mpya umebaini matatizo mengine makubwa ya kiafya.
Alisema vipimo vimebaini kuwa kiongozi huyo ameumizwa zaidi sehemu za shingo, taya na mbavu, hivyo, kukiri kwamba huyo ameumizwa sehemu kubwa ya mwili.
“Kuna vipimo vinahitajika; ninachoweza kusema ni kwamba tumegundua ameumia sana kwenye shingo, taya, ubongo wake, mbavu… kwa kifupi naweza kusema amejeruhiwa sehemu kubwa ya mwili wake,” alisema Profesa Kihamba.
Kutokana na mabadiliko hayo, sasa madaktari wameanzisha mchakato wa kukusanya fedha za kumsafirisha nje ya nchi kutokana na kukosekana kwa kipimo maalumu ambacho kitaweza kugundua madhara mengine.
Maktari bingwa nao wagoma
Mgomo huo sasa umechukua sura nyingine baada ya madaktari bingwa kutangaza kujiunga nao huku wakiwataka madaktari wengine kote nchini kushiriki.
Akitoa tamko la madaktari hao waliokuwepo kwenye kikao kwa zaidi ya saa nane ndani ya majengo ya MOI, Dk. Catherine Mng’ong’o alisema uamuzi wa kikao hicho unatokana na ukatili aliofanyiwa Dk. Ulimboka.
Kwa mujibu wa Dk. Mg’ong’o mgomo huo wa mabingwa utahusisha hospitali za MOI, Muhimbili, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na MUHAS zote za jijini Dar es Salaam.
Kabla ya kutoa tamko hilo alisema madaktari wote nchini wamefadhaishwa na kupata hofu kuhusu usalama wa maisha yao hivyo kuitaka serikali iweke bayana mustakabali wa wataalam wa sekta hiyo muhimu.
“Madaktari tumefadhaishwa, tumesikitishwa pia tumepata hofu kuhusu usalama wa maisha yetu; tunaiomba serikali itamke mustakabali wa usalama wetu.
“Tunalaani ukatili aliofanyiwa Dk. Ulimboka ambaye hali yake inazidi kuwa mbaya… tunalaani juhudi zinazofanywa na wadhalimu wanaoitendea mabaya sekta ya afya kwa kutudhuru,” alisema Dk. Mg’ong’o.
Aidha mabingwa hao wameiomba serikali kuwarejesha kazini madaktari waliosimamishwa kazi na kunyimwa mshahara wao wa mwezi wa sita kwa sababu kufanya hivyo ni kuwadhalilisha wataalam hao.
“Hakuna mahali waliposema hoja za mgomo sio za msingi sasa kwa nini wawasimamishe kazi na kuwanyima mshahara wao wakati suala hili liko mahakamani,” alisema kwa niaba ya timu ya madaktari bingwa huku akisisitiza kwamba huduma kwenye hospitali zilizotajwa zimesitishwa.
Polisi watishia kukamata madaktari
Jeshi la polisi nchini limetishia kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria madaktari watakaoendelea kukaidi amri halali ya mahakama ya kusitisha mgomo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Kamishina wa Operesheni nchini, Paul Chagonja, kwa wandishi wa habari, akisema hawatakuwa tayari kuona yeyote akitendewewa kinyume na matakwa ya sheria hivyo aliwataka madaktari kuheshimu viapo vyao vya kazi vinavyosisitiza kwamba udaktari ni wito.
Alisema ikiwa madaktari hawakuridhishwa na mwenendo wa mahakama wangefuata sheria kwa kukata rufaa mahakama za juu kuliko kuchukua uamuzi wa kibabe wa kugoma na kusababisha wagonjwa kukosa huduma za afya na kusababisha wengine kupoteza maisha.
Akizungumzia kuhusu Jeshi la Polisi kuhusishwa katika tukio la kutekwa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, alikana chombo hicho cha usalama kuhusishwa kwa namna yoyote na tukio hilo kwa sababu wanatambua suluhu ya mgomo kamwe hauwezi kutatuliwa kwa kumuondoa daktari huyo bali njia pekee ni ya mazungumzo.
Aliwaonya wale wanaosambaza uvumi wa kulihusisha jeshi la polisi na tukio la kujeruhi kwake anayachukulia kama maneno ya kuwakatisha tamaa ili washindwe kufanya uchunguzi wao kikamilifu.
Chagonja pia aliwataka wananchi na madaktari kuwa na imani na jopo la wapelelezi walioteuliwa kufuatilia suala hilo, na kwamba watafanya uchunguzi kwa kina na kwa haki.
Kumetokea sintofahamu baina ya polisi na watu wa kada mbalimbali kutokana na kuwepo kwa tuhuma zinazolihusisha jeshi hilo na tukio la kutekwa, kupigwa na kujeruhiwa vibaya kwa Dk. Ulimboka.
Aidha, kutokana na hali hiyo, watu wengi wamependekeza kuundwa kwa chombo huru kitakachofanya uchunguzi wa haki kwa sababu tayari jeshi hilo, limekwishachafuka kwa kuhusishwa na tuhuma hizo.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment