Wednesday, June 27, 2012

Membe: Nitataja wezi wa rada


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema akiona kimya kinazidi kuhusu watuhumiwa wa rushwa katika kashfa ya rada atawataja bungeni kwa sababu kila aliyehusika ametajwa na kuwekwa picha yake katika kitabu cha ‘The Shadow World-Inside the Global Arms Trade’ kilichoandikwa na mwandishi wa Afrika Kusini, Andrew Feinstein.

Akizungumza katika mahojiano na kituo cha radio cha jijini Dar es Salaam, Membe, alisema atawataja bungeni wahusika hao kwa sababu kimya chao tangu kutoka kwa kitabu hicho kinamaanisha kwamba wanahofia kukanusha.

Alisema kitabu hicho chenye kurasa 672 kina sura nzima inayozungumzia suala la rada akitaja kwamba imeandikwa kwenye ukurasa wa 218 na 219.

“Na ukienda ukurasa wa 285 utakuta wanaeleza namna fedha zilivyoibwa,” alisema.

Kashfa ya ununuzi wa rada uliofanywa na serikali ya Tanzania kwa kampuni ya silaha ya BAE Sysyem ya Uingereza, umeitia doa serikali kwa kuwa imekuwa ikielezwa kwamba ilinunuliwa kwa bei ya kuruka huku ikiwa katika hali mbaya.

Hata hivyo, tayari serikali imekwisha kupokea paundi milioni 29 kama malipo ya fidia kwa serikali ya Tanzania na imekubaliwa kwamba fedha hizo zitatumika kununua vitabu na madawati kwa shule za msingi na sekondari nchini.

Aidha, Membe alizungumzia suala la kugombea urais akieleza kuwa hawezi kutangaza nia ya kuwania nafasi hiyo kwa sababu jambo hilo ni kubwa sana na linahitaji mtu kusikia sauti inayomwambia "kagombee".

"Kwanza ni jambo la ajabu mtu kutangaza leo kwamba unataka kugombea urais. Bado tuna miaka mitatu kufikia uchaguzi mkuu ujao. Kwa hiyo kwa kipindi hiki chote hadi wakati huo utakuwa umefanya nini?" alihoji.

Alisema kugombea urais: "Siyo suala la kukurupuka au kuona gazeti moja ama mawili yamekuandika kwamba unaweza kisha ukagombee urais. Ni lazima usikie sauti inakwambia ukagombee. Vinginevyo utaishia kwenda kwa waganga maana siku hizi waganga nao wanaingilia mambo haya. Wanakuhusisha hata kama hujaomba. Wanakwambia eti utashinda."

Aliongeza kuwa: "Suala la urais siyo la kukusanya watu na kudhani kwamba ndiyo watakupigia kura. Hata mimi hapa Benard Membe nikitaka kukusanya watu, watakuja wengi tu. Lakini siyo lazima watu uliokusanya wakupigie kura. Urais ni sera zako. Ni kutambua umasikini wa Watanzania uko wapi, unatokana na nini na ni kwa namna gani utauondoa."

"Mtu ni mbunge, hajafanya chochote katika jimbo lake dogo, lakini anasema anataka kuja kugombea urais. Kama jimboni kwako hujafanya kitu, utafanya nini ukipewa jukumu la nchi nzima?" alihoji Memba.

Membe ambaye ni Mbunge wa Mtama (CCM), alisema hawezi kusema atagombea uraia hadi atakaposikia sauti ikimwambia afanye hivyo.

Alipoulizwa kama akioteshwa atatangaza nia ya kugombea, alijibu: "Salini mniombee."

Membe pia alikanusha madai yaliyoripotiwa na gazeti moja kwamba alikisifu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakati alipowakaribisha viongozi wa chama hicho na kupata nao mlo nyumbani kwake jimboni kwake, Mtama, Lindi.

Alisema kamwe hawezi kuisifia Chadema na kwamba kilichoripotiwa ni uongo.

"Mimi nilikuwa jimboni kwangu ambako Mwenge wa Uhuru ulikuwa unakuja ... viongozi wa Chadema walikuja nyumbani kwangu nikawakaribisha. Walikuwa na njaa wakala na wakanywa; kumkaribisha mtu hakuna itikadi hakuna udini ni utamaduni wetu," alisema.

 "Hapakuwa na wakati wowote ambao niliwafagilia (kusifia). Jambo zuri ni kwamba walioandika wamedai kwamba kuna mikanda ya video ilirekodiwa katika mazungumzo yangu na viongozi wa Chadema. Itolewe hapa kila mmoja aione kama kuna sehemu niliwasifu Chadema, kwa nini inafichwa? Najua hawatamani mikanda hiyo iwekwe hadharani kwa sababu wanajua kitakachofuata ni mahakamani," alisema.

Aliwasifu wahariri ambao walimpigia simu kabla ya kuitoa habari ile ili kupata maoni kutoka upande wa pili.

Serikali ilirejeshewa na kampuni ya zana za kijeshi ya Uingereza BAE Sh. Bilioni 72.3 kutokana na ufisadi wa rada hiyo iliyonunuliwa kwa bei ya kutupa ya Sh. bilioni 70.

Miongoni mwa watu wanaotarajwa kuhusika katika sakata hilo na wamekanusha mara kadhaa ni pamoja na Mbunge wa Bariadi Mashariki (CCM), Andrew Chenge, wakati huo akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment