Wednesday, June 27, 2012

Kamati ya Lowassa yaivaa Wizara ya Membe

KAMATI ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imeanza ziara ya siku 14 katika balozi za Tanzania kwenye nchi za Marekani, Ulaya na Asia kukagua namna zinavyotekeleza mambo ya sera na uchumi.

Ziara ya Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ilitangazwa jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar ers Salaam wakati wajumbe 20 wa Kamati hiyo na makatibu sita wanaondoka nchini.

Hata hivyo, wakati Kamati hiyo ikienda kutembelea balozi hizo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe mwenye dhamana na balozi hizo, alisema ziara hiyo haikuja wakati sahihi, kwa kuwa Mkutano wa Bunge la Bajeti unaendelea.

Lakini, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara hiyo, Lowassa alisema ziara hiyo imekuja wakati sahihi kwa kuwa hiyo pia ni kazi ya Bunge.

Katika ziara hiyo, Kamati hiyo imegawanyika katika makundi sita yatakayotembelea balozi 14 katika nchi 14.   Wabunge hao ni yeye Lowassa, Vita Kawawa, Khalifa Suleiman Khalifa, Rachel Mashishanga na Beatrice Shelukindo ambao watatembelea balozi za Canada, Washington na New York, Marekani na London, Uingereza.

Wengine ni Mohamed Ibrahim Sanya, Mchungaji Israel Natse ambao watatembelea New Delhi, India na Kuala Lumpur, Malaysia.

Kundi jingine lina Mussa Zungu, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi, Betty Machangu na Mussa Hassan Mussa linaotembelea balozi za Japan na China.

Kundi la nne litakalotembelea Ujerumani na Sweden, linawahusisha Anna Abdallah, John Shibuda na Augustino Massele, huku wabunge wengine akiwamo Mohamed Seif Khatib, Hilda Ngoye na Anastazia Wambura watatembelea balozi za Brussels, Ubeligiji na Geneva, Uswisi.

Kundi la mwisho linalotembelea Paris Ufaransa na Rome Italia, linawahusisha wabunge John Chiligati, Engen Mwaiposa na Masoud Abdallah Salim.

Kauli ya Membe
Ziara hiyo imeonyesha kumshangaza Waziri Membe akisema kuwa hajui wanakwenda kufanya nini huko.
Akizungumza na gazeti dada la The Citizen jana katika uwanja huo, Waziri Membe aliyekuwapo katika uwanja huo, alisema ziara hiyo haikuja wakati sahihi.

“Shughuli za Kamati huko nje huwa ni kujifunza kutoka kwa wenzao kwenye mataifa tofauti, na ziara hii hilo halikufanyika….lakini nimesikia wanakwenda kutembelea balozi zetu huko nje na sio zilizoko katika bara la Afrika,” alisema Waziri Membe.

Aliongeza kuwa, “Hapo inabidi sote tujiulize kama lengo ni kuangalia utendaji wa balozi zetu mbona sasa zinakuwa za Ulaya na Asia peke yake?"

Waziri Membe alifafanua kuwa kwenda kutembelea balozi si tatizo, lakini katika kipindi hiki ambacho Bunge la Bajeti linaendelea mjini Dodoma, kwa busara ya kawaida, mbunge anatakiwa kuwa bungeni akifuatilia Bajeti.

Alisema kulingana na ratiba ya Bunge, ziara kama hiyo ilitakiwa kufanyika wakati wa vikao vya Kamati za Bunge, lakini si sasa ambapo Bunge linakutana.
  Licha ya kukanusha mara kwa mara, Waziri Membe na Lowassa wamekuwa wakitajwa kuwania Urais kupitia CCM siku za usoni, jambo ambalo limekuwa likiwataja wabunge hao kama mahasimu wa kisiasa.
 
Kilichotokea kwenye kamati
Tayari Kamati hiyo imewahi kuripotiwa kuingia katika mvutano Membe, ambapo Juni 6, mwaka huu ilimbana ikisema alichelewa kugawa vitabu vya  bajeti yake kwa wajumbe wa Kamati.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo aliliambia gazeti hili kwamba wajumbe waligomea Bajeti hiyo kutokana na kuchukizwa na kitendo hicho na kutokuonyesha madeni ya wizara yakiwamo makato ya wafanyakazi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Wizara hiyo, Assah Mwambene alipinga taarifa hizo, lakini akafafanua kilichotokea kuwa hoja ya vitabu kuchelewa iliibuka, na tayaru waziri aliwaeleza wajumbe kuwa hilo ni suala ambalo lilitokana na kamati husika.

 Alisema vitabu hivyo viliwasilishwa mwisho wa wiki, lakini kwa kuwa labda haikuwa siku za kazi, ndiyo maana havikuwafikia mapema wajumbe. 



Mwananchi

No comments:

Post a Comment