Siku moja baada ya Serikali kutangaza kutumia hospitali za Jeshi na madaktari wastaafu kunusuru afya za wagonjwa kufuatia mgomo wa madaktari nchini, juhudi zaidi zimechukuliwa na sasa itatumia pia hospitali binafsi.
Hospitali zilizotajwa kukubali kushirikiana na Serikali kutoa huduma za afya kwa watakaohitaji tiba ya haraka na walio katika tiba isiyoweza kusitishwa ni pamoja na TMJ, Regency, Aga Khan, Hindu Mandal, CCBRT na Hospitali ya Jeshi Lugalo.
Aidha, nguvu zimeongezwa katika hospitali za Mwananyamala, Amana na Temeke za Dar es Salaam kunakodaiwa hakuna mgomo, ili kutotoa rufaa nyingi kwa wagonjwa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kunakodaiwa kuwa na mgomo.
Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja aliliambia gazeti la HABARI LEo ofisini kwake kuwa, utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu kuhusu kutumia hospitali za Jeshi na madaktari wastaafu limeanza na sasa nguvu imeongezwa kwa kuhusisha hospitali binafsi.
“Pamoja na Lugalo kuwa tayari, tulikuwa katika mazungumzo na hospitali za binafsi ikiwa ni juhudi hizo hizo za Serikali, hospitali kadhaa zimeshakubali ambazo ni CCBRT, Aga Khan, Hindu Mandal, Regency na TMJ na tunaendelea kuzungumza na nyingine,” alisema Mwamwaja.
Pamoja na hilo, Mwamwaja alisema nguvu kubwa pia imeelekezwa katika hospitali za Mwananyamala, Temeke na Amana kuhakikisha kuwa wagonjwa wanatibiwa kikamilifu.
Akifafanua kuhusu namna ya wagonjwa watakavyotibiwa katika hospitali hizo za binafsi, Mwamwaja alisema;” Kutakuwa na fomu maalumu ambayo daktari wa Amana, Mwananyamala au Temeke atakayeona mgonjwa anahitaji tiba zaidi, atamjazia ili apokewe ama kupelekwa katika hospitali hizo”.
Pia alisema wagonjwa watakaohitaji rufaa, kwa utaratibu huo huo, watatibiwa katika Hospitali ya Jeshi la Lugalo ambayo imekuwa tayari muda mrefu ikishirikiana na hospitali nyingine chini yake.
Alisema mgomo wa awali madaktari walipelekwa Muhimbili kutoa huduma, lakini baadhi ya madaktari wenyeji mgomo wa awali walidaiwa kuwakwamisha makusudi kufanya huduma na Serikali ililiona hivyo na kuona ni bora wagonjwa wapelekwe huko ili kupata tiba vizuri zaidi.
Alisema madaktari wastaafu na wa Wizara kama alivyosema Waziri Mkuu Pinda, ndio watakaohusika Muhimbili. Pinda alieleza hayo juzi bungeni akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliyetaka kujua hatua za Serikali kukabili mgomo huo.
Habari Leo
No comments:
Post a Comment