Sunday, June 24, 2012

CCM kumng’oa Mukama


WABUNGE NAO WAKALIA KUTI KAVU
MKAKATI wa kumng’oa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama, anayedaiwa kushindwa kukiendesha chama umeshika kasi, Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Mbali na Mukama, baadhi ya wabunge pia wanataka wenzao waliogoma kuipitisha bajeti ya serikali nao kushughulikiwa kwa kukisaliti chama.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa baadhi ya wabunge na wanachama wanataka Mukama aachie ngazi au afukuzwe.
Duru za kisiasa kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa matumaini ya wanachama wengi wakiwamo vigogo wa chama hicho waliyokuwa nayo kwa Mukama wakati anaingia madarakani yamefifia.
Katibu mkuu huyo aliyeingia madarakani kwa mbwembwe ndani ya CCM miaka miwili iliyopita, anadaiwa kushindwa kabisa kukijenga chama kama ilivyotarajiwa na badala yake ametengeneza mpasuko mkubwa ndani ya chama.
CCM kwa sasa inakabiliwa na makundi makubwa mawili yenye wafuasi wengi, moja ni lile linaloongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, ambaye amebaki na kundi linalojinadi kama wapinga ufisadi na kundi jingine ni lile linaloongozwa na hasimu wake kisiasa, Edward Lowassa, linalopingana na dhana ya kujivua gamba.
Mukama pia anadaiwa kushindwa kukiimarisha chama na kuruhusu wanachama wengi kukihama chama hicho kwa kile kilichoelezwa kutoridhishwa na mwenendo wa mambo ndani ya CCM.
Kiongozi huyo anabebeshwa lawama kuwa ameshindwa kusimamia dhana ya kujivua gamba wakati yeye ndiye aliyeanzisha hoja hiyo kupitia tume aliyoiongoza kufanya utafiti kubaini sababu za CCM kupata kura chache za urais na kupokwa majimbo mengi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
“Unajua, Mukama ndiye aliyekuja na matokeo ya utafiti kwenye Kamati Kuu na Halmashauri Kuu. Alibainisha sababu kadhaa za chama kushindwa, lakini sababu kubwa tume yake ilibaini ni pamoja na chama kukosa mvuto kutokana na baadhi ya makada wake, Edward Lowassa, Andrew Chenge na Rostam Aziz kuhusishwa na ufisadi. Akaja na mapendekezo kwamba makada hao wavuliwe nyadhifa zao.
“Leo ameshindwa kusimamia kile alichokiamini, badala yake chama kimekuwa kikipiga vita ya maneno tu, mara kutoa siku 90, mara tumeongeza, mara haijulikani. Matokeo yake tumezalisha makundi yanayokitafuna chama,” alisema kada mmoja ambaye ni mjumbe wa NEC.
Kada huyo anasema kuwa baadhi ya makada wanaotuhumiwa kwa ufisadi waliandaliwa barua za kutakiwa kuachia nyadhifa zao lakini hilo lilishindikana kutokana na utendaji mbovu wa Mukama.
Makada wengine wanamlinganisha Katibu Mkuu Mukama na mtangulizi wake, mzee Yusuf Makamba, kwamba licha ya kuwa na elimu ndogo ya darasani, amemzidi Mukama kiutendaji.
Dalili za CCM kumchoka Mukama zimejionyesha hivi karibuni katika moja ya vikao vya wabunge wa CCM ambapo baadhi walifikia hatua ya kusema katibu mkuu wao amechoka kimawazo, bora aachie ngazi sasa.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho kilichoongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, mjini Dodoma zilisema wabunge walikuja juu wakati walipokuwa wakijadili hali ya kisiasa ndani ya chama chao na kuwekeana msimamo wa kuiunga mkono Bajeti ya mwaka 2012/2013.
Mmoja wa viongozi waandamizi wa CCM, aliliambia gazeti hili kuwa katibu mkuu sasa hashirikishwi katika baadhi ya mambo baada ya kubaini kuwa hana uwezo wa kukiimarisha chama.
“Angalia katika mikutano yote inayofanywa na chama kwa sasa hata ule wa Jangwani ulikuwa na watu wengi, Mukama hakuwepo. Ingawa alikuwa nje ya nchi, lakini hata kama angekuwapo, asingepata nafasi ya kuhutubia kwani hana uwezo wa kuongea hadharani.
Kada mwingine wa CCM alimshmabulia Mukama kwa madai kuwa amekuwa akiropoka vitu ambavyo wakati mwingine hana utafiti navyo.
“ Mfano ni wakati wa kumuaga marehemu Bob Makani. Alitoa historia ya ajabu kuhusu waasisi wa CHADEMA, matokeo yake, Freeman Mbowe, alimuumbua pale alipotoa ufafanuzi kupinga kauli yake,” alisema.
Wabunge walioipinga bajeti kukiona
Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa kuna mpango wa kutaka kuwawajibisha baadhi ya wabunge waliokiuka msimamo wa pamoja wa wabunge wa CCM juu ya kuipitisha bajeti.
Bajeti hiyo ya serikali iliyopitishwa Ijumaa wiki hii kwa kura 225 za ndiyo huku kura 72 zikiikataa, kwa kupiga kura za hapana, zaidi ya wabunge 54 hawakuhudhuria mkutano huo.
Kuna taarifa kuwa wabunge waliogoma kuhudhuria kikao hicho bila taarifa na wengine waliokataa kuipitisha bajeti hiyo huenda wakakumbana na mkono wa chama ambacho katika siku za hivi karibuni kimekuwa kikihaha kujinusuru kutoka katika minyukano ya makundi yanayohasimiana.
Inasemekana baadhi ya wabunge wanataka wenzao wajadiliwe na ikiwezekana wawajibishwe ili kujenga nidhamu chamani pamoja na kudumisha uwajibikaji wa pamoja.
Wabunge hao wanatarajiwa kujadiliwa na kikao cha wabunge wa CCM ambacho kinatarajiwa kufanyika mapema wiki ijayo mara baada ya kuwasilishwa kwa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Wabunge wanaoonekana kuwasaliti wenzao ni Luhaga Mpina (Kisesa), Deo Filikunjombe (Ludewa) na Kangi Lugola (Mwibara).

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment