Saturday, June 23, 2012

Tucta: Wafanyakazi kugoma nchi nzima

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi  Tanzania (Tucta), limetishia kuitisha mgomo wa wafanyakazi kwa nchi nzima kushinikiza serikali kupunguza kodi ya pato kwenye mshahara  (Paye) na kupandisha kima cha chini hadi  kufikia Sh. 200,000.

Naibu Katibu Mkuu wa Tucta, Hezrone Kaaya, alitangaza azama hiyo jana mjini Dodoma mbele ya wanahabari na kusema wanachosubiri ni kusikia kauli ya serikali kwenye bajeti ya Wizara ya Fedha iwapo imezingatia mapendekezo yao hayo.

Alisema wafanyakazi waliiomba serikali kuwapunguzia kodi ya pato la mshahara (Paye), kupandisha kima cha chini cha mshahara hadi kufikia 200,000 kwa mwezi kwa sekta ya umma na kurekebisha pensheni. 

Katika masuala hayo serikali imezingatia moja la kuweka uwiano wa pensheni baada ya kuunda mamlaka ya kusimamia mifuko ya pensheni (Ssra).

“Tucta na vyama shiriki tulitaka makato ya Paye  yashuke kutoka asilimia 15  hadi asilimia 9 , tulitoa mapendekezo ya namna ya kufidia pengo hilo  miaka miwili iliyopita. Kodi hiyo imeshuka kwa asilimia moja tu tena mwaka jana,” alisema Kaaya.

Alisistiza zaidi kuwa, “ Tucta tunaweka wazi kuwa  kama serikali haitazingatia maoni yetu yaliyotokana na majadiliano tusilaumiwe kwa hatua tutakazozichukua  kwa kutumia silaha yetu ya umoja. Serikali itambue kuwa  Tucta hatupendi kuharibu ….”.

Aliongeza kuwa wafanyakazi wataikaba koo serikali  kwenye nyongeza ya mishahara na kodi ya mapato ya –Paye na kusisitiza “ Tucta tunahitaji mambo haya mawili yafanyiwe marekebisho katika bajeti ya mwaka 2012/13 vinginevyo utaibuka mgogoro mkubwa ambao serikali haitaweza kuuzima kirahisi.”

Alisema iwapo serikali haitazingatia maoni yao  wanaanza vikao na maamuzi ya kuitisha mgomo nchi nzima yatafuata na safari hii hawatarudi nyuma kama ilivyotokea mwaka 2010.

Alisema Tucta itajiunga na walimu pamoja na madaktari kuendesha mgomo huo wa kitaifa na serikali isije kuwalaumu iwapo itapuuza  mapendekezo ya wafanyakazi.

Waliulaumu hatua ya kuondoa kodi kwa makampuni kadhaa  pia kwenye  boda boda zinazomilikiwa na vigogo lakini kuwabandikia mzigo mkubwa wa kodi wafanyakazi  hatua ambayo alisema haitakubalika wala kuvumilika tena.


NIPASHE

No comments:

Post a Comment