Friday, May 25, 2012

MBUNGE WA ROMBO CHADEMA JOSEPH SELASINI APATA AJALI

Mbunge wa Rombo Mheshimiwa Joseph Selasini (CHADEMA) amepatwa na ajali ya gari leo katika eneo la Boma Ng'ombe (al maaruf Mr. Price) wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, alipokuwa safarini kutoka Arusha alikokwenda kumtoa baba yake kutoka hospitalini, kuelekea Rombo, Kilimanjaro.
Amefahamisha katika ukurasa wake wa facebook ifuatavyo:
Ajali hiyo imetokea majira ya saa moja jioni ikilihusisha gari lake aina ya Toyota, Land Cruiser lenye namba za usajili T441DRT alilokuwa akiliendesha mwenyewe.
Chanzo cha ajali hiyo kinaelezwa kuwa kimetokana na jitihada za kukwepa kungonga mwendesha pikipiki, ndipo gari lilikosa mwelekeo na kupinduka.
Ndani ya gari walikuwemo watu sita, ambapo watatu wamepoteza uhai akiwemo Mama Mzazi, Grace Shao na shangaziye Mbunge huyo. Waatatu waliosalia akiwemo Baba Mzazi na mtu mwingine walikuwa wamejifunga mikanda na kusalimika.
Hali ya Mhe. Silasini  inaelezwa kuwa "ni nzuri" (SI mahututi) amejeruhiwa mkono. Yeye pamoja na majeruhi wengine walioumia vibaya, walifikishwa katika hospitali ya wilaya ya Hai. Mipango ya kuwahamishia katika hospitali ya KCMC inaendelea.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi.
Bofya kifute cha pleya iliyopachikwa hapo kusikiliza taarifa iliyoripotiwa na Rodrick Mushi, kwenye kipindi cha Dira - Ripoti za matukio cha RSI. 

1 comment:

  1. Pole sana Mh J Selasini kwa msiba uliokupata na kwa ajali hiyo. Mwenyezi Mungu awalaze mahali peponi waliotangulia mbele ya haki. Amin.

    ReplyDelete