CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimewataka wakazi wa jiji la Dar es Salaam na viunga vyake kuhudhuria mkutano wa hadhara utakaofanyika kwenye viwanja vya Jangwani kesho.
Kabla ya mkutano huo kutakuwa na maandamano ya amani yatakayofanywa na wafuasi wa chama hicho kutoka majimbo yote ya jiji hili.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Wilfred Lwakatare ambaye ni Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho ililitaka jeshi la polisi kuacha kufanya kazi kwa ramli badala yake kulinda mali na usalama wa raia kwa madai kwamba hawana askari wa kutosha kuwalinda waandamanaji hao.
“Ni vigumu kwa mtu yeyote makini kuweza kukubaliana na hoja za Jeshi la Polisi kuwa hawataki wananchi watembee kwa amani kutoka maeneo mbalimbali kwenda eneo la mkutano eti tu kwa sababu kunaweza kuibuka vitendo vya ukabaji, uporaji katika matembezi hayo! Huku ni kufanya kazi kwa mtindo wa kupiga ramri!
“Pamoja na madai ya jeshi hilo kuwa hakuna askari wa kutosha kulinda kile wanachokiita maandamano, kutokana na mantiki hiyo hapo juu, hatutashangaa wakipatikana askari wengi wa kuanzisha vurugu, kupiga watu, kutesa na kuua, kama ambavyo imetokea katika maeneo mengine kwa kisingizio cha kuzuia maandamano,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maandamano yanayoingiliwa na polisi kisha kuzuka vurumai ni yaliyotokea Arusha, Songea Ikwiriri, ambako jeshi hilo limekiri lilikuwa chanzo cha vurugu hata wananchi kupoteza maisha.
“Tunawaomba ndugu zetu wa jeshi la polisi watoe ushirikiano kwa wananchi. Wasifanye kazi kwa ubaguzi wa aina yoyote ile katika makundi mbalimbali ndani ya jamii wala maelekezo ya kisiasa, hasa kutoka kwa chama tawala, CCM,” ilifafanua taarifa hiyo.
CHANZO - Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment