Saturday, April 28, 2012

Tundu Lissu aibwaga CCM


MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dodoma imetupilia mbali madai ya kupinga matokeo ya ubunge wa jimbo la Singida Mashariki na kutangaza kuwa Tindu Lissu alishinda kihalali katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 30, 2010.
Katika kesi hiyo ya madai iliyoanza kusikilizwa tangu Machi 12, mwaka huu, walalamikaji wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) walitarajia kuleta mashahidi 51 lakini kwa sababu zisizofahamika ni mashahidi 24 tu na vielelezo saba viliwasilishwa kama ushahidi mahakamani hapo.
Katika kesi yao ya msingi walalamikaji walikuwa wakipinga ushindi wa mlalamikiwa namba moja ambaye ni Tundu Antiphas Lissu kuwa mbunge kwa madai kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa sheria za uchaguzi.
Walidai kuwa ukiukwaji huo uliufanya uchaguzi huo kutokuwa huru, wa wazi na haki na hivyo kumfanya mgombea wa CCM asiweze kupata ushindi katika uchaguzi huo.
Lissu ambaye alishinda kwa kupata kura 13,787 na kumzidi mgombea wa CCM Jonathan Njau kwa kura 1,626 alileta mashahidi wanne tu akiwemo yeye mwenyewe.
Akisoma hukumo hiyo, Jaji Moses Mzuna, alizitaja hoja zilizowasilishwa katika mahakama hiyo kuwa ni pamoja na mlalamikiwa kuandaa barua zilizodai kuwa ziliandaliwa na vyama vya siasa vya kambi ya upinzani ambavyo havikuwa na wagombea katika uchaguzi huo.
Hoja zingine ni kuwa na mawakala nje na ndani ya chumba cha kupigia kura zaidi ya sheria inavyoagiza, kutoa hongo ya usafiri na chakula kwa mawakala wa vyama vyote isipokuwa CCM, askari katika baadhi ya vituo waliacha shughuli zao na kwenda kufanya kampeni.
Hata hivyo Jaji Mzuna ambaye alikuwa akisoma hukumu hiyo huku akitoa mifano ya kesi mbalimbali zilizotolewa hukumu na Mahakama Kuu aliweka bayana kwamba mashahidi wote walifika kutoa ushahidi walionekana kujichanganya wakati wa maelezo yao.
Alisisitiza pia kwamba waleta maombi katika kesi hiyo walishindwa kuwaleta mashahidi muhimu ambao wangeweza kutoa ukweli juu ya hali halisi ya kesi hiyo licha ya kufahamika, jambo lililotafsiriwa kuwa huenda walifanya hivyo kwa kuhofia kuharibiwa kesi yao.
“Wao ndiyo waliopaswa kuthibitisha bila kuacha shaka yoyote juu ya dai lao hilo la msingi, kwani walitakiwa kuwaleta waliobaini tuhuma hizo zikitendeka kwani ni jukumu la mleta maombi kuthibitisha,” alifafanua.
Jaji huyo alisema kesi hiyo ilijikita zaidi kwenye kushuku na hivyo walalamikaji kujikuta wakishindwa kuithibitishia mahakama hiyo kikamilifu.
“Jambo la kushangaza ni kwamba mashahidi walioitwa mahakamani hapa walikuwa ni sawa na watu wanaovaa koti kwa kubadili nje ndani na ndani nje huku mawakili wa waombaji wakijigeuza kinyonga kila walipokuwa wakitoa maelezo yao.
Kabla ya kutoa hukumu hiyo Jaji Mzuna alisema ni vema mahakama zisibariki pale inapobaini kuna kila dalili za kuwanyima haki wananchi wa jimbo husika.
Aliamuru walalamikaji kumlipa Lissu gharama alizotumia katika kesi hiyo kwa mujibu wa taratibu za kisheria kuhusu madai ya gharama za kesi hiyo.
Aangua kilio
Lussu na mkewe katika hali isiyokuwa ya kawaida waliangua kilio mara baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo, huku akisema kuwa amesikitishwa na waliomshtaki kwa kile alichosema walijua hawana ushahidi wowote zaidi ya kutunga na kuhisi.
“Nakubaliana na matokeo ya hukumu hii na ni kweli kabisa haki imechukua mkondo wake, kwani waleta maombi hawakuwa na ushahidi wowote zaidi ya kutunga, kuhisi, kufundishana uwongo lakini mengi zaidi nitaongea na wananchi kule kijijini kwatu Ikungi muda mfupi baadaye,” alisema Lissu.
Hukumu hiyo ilipokelewa kwa shangwe kubwa na mamia ya watu, kiasi cha kulazimisha kuwekwa kwa vipaza sauti ili watu waliokosa nafasi ndani kuweza kusikiliza.
Ulinzi mkali wa polisi
Tangu asubuhi jana, askari polisi wengi na wale wa usalama wa taifa walitanda kila kona ya eneo la mahakama hii, kinyume kabisa na hali inavyokuwa siku zote.
Ulinzi huo uliandamana na ukaguzi mkali ambapo kila aliyeingia ndani ya jengo la mahakamana alikaguliwa, huku askari wakilazimika kuwazuia wananchi waliozidi kufurika katika mahakama hiyo kila muda ulivyosonga mbele.
Hata hivyo, haikuweza kuelezwa sababu za msingi za kuimarisha ulinzi huo, ambapo ofisa mmoja wa jeshi la polisi aliyehojiwa kwa sharti la kutotaja jina alisema ni wajibu wao kulinda amani katika matukio mazito kama hilo.

No comments:

Post a Comment