Saturday, April 28, 2012

LWAKATARE - Kauli ya Dr Slaa si ya kwake ni ya Chama


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimelitahadharisha Jeshi la Polisi kutofanya hila yoyote ya kuhamisha mantiki ya msingi iliyotolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa.
Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho jana, Wilfred Lwakatare, ilisema kauli iliyotolewa na Dk. Slaa Jijini Mwanza, ilikuwa ni msimamo wa chama na wala si ya kwake.
“Tunaona polisi wameshindwa kujibu hoja za msingi ambazo nyingine zinawahusu wao moja kwa moja… ilikuwaje tukio la wabunge wa Chadema washambuliwe na kujeruhiwa kinyama mbele ya polisi wenye silaha,” ilihoji sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa ilisema, agizo la Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, ACP Phillip Kalangi, kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo linafanya uchunguzi wa kauli alizodai ni za uchochezi na kutolewa na Dk. Slaa, ni za vitisho kwa chama hicho.
“Wao polisi wanadai wakijiridhisha Dk. Slaa alitoa kauli hizo, basi watamkamata na kumfungulia mashtaka. Hatuwezi kukubaliana na hilo kabisa,” ilisema.
Kurugenzi ya Ulinzi na Usalama ya Chadema ilisema, inashangazwa na Jeshi la Polisi badala ya kuwakamata na kuwafikisha vyombo vya sheria wale ambao wanafahamika kutenda tukio hilo kwa wabunge wao, wanaitisha mkutano na wanahabari na kutoa vitisho kwa viongozi wa chama.
Aidha, taarifa hiyo iliendelea kusema Chadema inayafuatilia kwa karibu matukio ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na uvunjwaji wa sheria uliofanywa na kuendelea kufanywa kwa makusudi na Jeshi la Polisi dhidi ya raia, na kuwafumbia macho wahusika wake.
“Uvunjaji wa haki za binadamu uliofanywa na polisi ni pamoja na mauaji wakati wa maandamano ya amani jijini Arusha, Januari 5, 2012. Pia mauaji yaliyofanyika Mbarali, Mbeya Januari 13, 2011,” Lwakatare alisema katika taarifa yake.
Pia, taarifa hiyo ilisema, jeshi hilo liliendelea na ukiukaji wake wa haki za binadamu kwa kufanya mauaji mjini Songea, Februari 22 mwaka huu, kwa kuwaua kwa kuwapiga risasi raia wasiokuwa na hatia pamoja na kuharibu mali zao.
Mauaji hayo yalitokana na maandamano ya amani ya wananchi wa mji wa Songea kuonyesha hisia zao dhidi ya uzembe wa vyombo vya dola kushindwa kudhibiti matukio ya mauaji ya mfululizo.
“Lakini kama hiyo haitoshi, Polisi walifanya vurugu huko Tandahimba Aprili 17 na 18 mwaka huu na kuharibu mali za wananchi waliokuwa wakidai haki zao katika malipo ya korosho.”
Hivyo, Chadema wanasema matukio hayo yote ni kielelezo cha uozo na uwajibikaji mbovu uliomo ndani ya Jeshi hilo ambalo badala ya kuwajibika kulinda amani na usalama wa raia na mali zao, limegeuka kuwa mlinzi wa makosa yake yenyewe na ya watawala wanaofanya dhidi ya raia wasiokuwa na hatia.
Lwakatare alisema kwenye taarifa hiyo kuwa ni karibu miaka mitano imepita tangu Chadema ilipotoa tamko juu ya vita dhidi ya ufisadi na mafisadi kwa kutoa orodha ya aibu ya mafisadi (list of shame), lakini Jeshi hilo limekaa kimya bila kutoa kauli yoyote, huku wananchi wakiendelea kuteseka kwa kuathiriwa na vitendo hivyo vya kifisadi.
“Hivyo basi Chadema haitaweza kufumbia macho vitendo hivyo vinavyofanywa na polisi kwa kujitokeza hadharani kutaka kuwalinda na kuwaficha wahalifu,” ilimaliza taarifa hiyo.

CHANZO - Nipashe

No comments:

Post a Comment