HATUA ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani hapa, James Ole Millya, kukihama na kujiunga na Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA), imekitikisa chama hicho tawala.
Licha ya kauli za baadhi ya viongozi wa CCM kubeza hatua ya Millya kujiengua CCM na kujiunga CHADEMA, duru za kisiasa ndani ya chama hicho zimeshtushwa na hatua hiyo.
Mmoja wa makada maarufu wa CCM ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alisema kuwa hatua hiyo siyo ya kubeza kwani kuna uwezekano mkubwa wa vigogo wengi kujiengua na kujiunga CHADEMA.
Kwa upande wake Millya ambaye anaelezwa kuwa na uhusiano wa karibu na Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Mstaafu, Edward Lowassa, amesema kuwa CCM haiwezi kupona kwenye uchaguzi mkuu 2015 kutokana na makundi yanayokitafuna chama hicho.
Aidha Millya amemshukia Katibu wa Itikadi na Uenezi taifa wa CCM, Nape Nnaye, pamoja na Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela, akiwataka kuacha kutapatapa kwa kutoa kauli zisizo na msingi kwa madai kuwa hakuwahi kuwa miongoni mwa waliotakiwa kujivua gamba ndani ya CCM.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano, Millya alisema anawashangaa viongozi hao kutumia kigezo cha yeye kupewa karipio ndani chama hicho kuwa ni mzigo.
Alisema kauli hiyo ya Nape na Shigela inaweza kutafsiriwa kama ni kejeli kwa Kamati Kuu ya CCM iliyokaa na kumteua Mrisho Gambo kugombea ubunge wa Afrika Mashariki kwani walipewa karipio hilo kwa pamoja.
“Mimi Millya sijawahi kuwa gamba ndani ya CCM kwani waliotakiwa kujivua gamba ni wale waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma za ufisadi, mimi sijawahi kufanya kazi serikalini wala sijawahi kufanya ufisadi wa aina yoyote na hakuna hata siku nimewahi kupewa barua au kuitwa kwenye kikao chochote kutakiwa nijivue gamba.
“Nawashauri wao kama viongozi wawe wanasema kweli waachane na siasa za kizamani za kusema uongo, wamekosa dira wanatapatapa hawajui wasemalo, kama kupewa karipio kali ndani ya chama unakuwa mzigo basi na Gambo naye ni mzigo? Kwani tulipewa naye adhabu hiyo, waseme kweli hizi ni kama kauli za sungura sizitaki mbichi hizi,” alisema Millya.
Aliwataka viongozi hao wawaeleze wananchi ni lini serikali ya CCM itawatatulia wananchi kero mbalimbali zinazowaongezea ugumu wa maisha badala ya kuwapa porojo zinazoweza kuishushia hadhi hata Kamati Kuu ya CCM iliyokaa chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, na kumpitisha Gambo kugombea ubunge wa Afrika Mashariki wakati kwa tafsiri yao naye ni mzigo.
Wanachama wa UVCCM wazungumza
Akizungumzia kuhama kwa Millya na kauli zilizotolewa na Katibu Mkuu wa UVCCM, mjumbe wa Baraza la vijana mkoa wa Arusha, Ally Bananga, alimpongeza mwenyekiti huyo kwa uamuzi aliouchukua akisema ni haki yake Kikatiba kuhama na kujiunga na chama chochote anachokitaka lakini akapinga kauli za kumpuuza zilizotolewa na viongozi wa kitaifa akiwemo Shigela.
“Kuondoka kwa Ole Millya ni pigo kwa UVCCM na chama kwa ujumla, sisi vijana wa Arusha tunamlilia na kusikitika kwa kukihama chama lakini kwa dhati nampongeza kwa kuvunja ukimya kwa kufanya kile anachokiamini ni bora kwake kisiasa,” alisema Bananga.
Hata hivyo, kada huyo alisema siyo kweli kwamba mwenyekiti huyo alikuwa mzigo na gamba ndani ya CCM kama alivyokaririwa Shigela kwani siyo mmoja wa watuhumiwa wa kosa lolote linalohusiana na ufisadi, rushwa au kufifisha taswira ya chama mbele ya umma kama ilivyoelezwa kwenye azimio la kutaka watu wajivue gamba.
“Mtu yeyote ndani ya CCM na serikali yake anayetoa kauli ya kupuuza kuondoka kwa Millya hakika atakuwa hana akili timamu kwa sababu pengo la kiongozi huyo ni kubwa na sisi vijana tunajua alivyojitoa kukijenga chama na Jumuiya mkoani Arusha na Kitaifa,” alisema Bananga.
Akielezea sababu anazodhani zimemsukuma kiongozi huyo kujiengua na kujiunga upinzani kuwa ni kutotendewa haki ndani ya chama chake licha ya juhudi kubwa alizofanya kukipigania.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Monduli, Julius Kalanga, alisema alishtushwa na kusononeshwa na taarifa za Millya kuondoka CCM na kwenda upinzani lakini anaheshimu uamuzi huo aliouita ni suala binafsi licha ya ukweli kwamba umekiathiri chama.
Hata hivyo, Kalanga alisema ataendelea kushirikiana na Millya kupigania na kutetea hoja za msingi walizozipigania kwa pamoja wakiwa CCM kwa maslahi ya vijana na taifa hili licha ya tofauti za kiitikadi zilizopo kati yao kwa sasa.
“Tofauti yetu kwa sasa na Millya ni itikadi, lakini naamini bado ana nia, malengo na kusudi la kupigania haki na maslahi ya vijana kama tulivyofanya pamoja akiwa ndani ya CCM na iwapo bado anaendelea na msimamo huo na ahidi tutashirikiana kwa maslahi na maendeleo ya vijana na taifa kwa ujumla,” alisisitiza Kalanga
CHADEMA yawatoa hofu wanachama wao
Katibu wa CHADEMA mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, alimpongeza Millya kwa uamuzi wa busara aliouchukua ambapo aliwataka wananchi wengine wenye kutaka mabadiliko kujiunga na chama hicho.
Hata hivyo alisisitiza kuwa licha ya CHADEMA kuwakaribisha wote wenye nia ya kujiunga nacho akaonya kuwa wasifanye hivyo kwa matarajio ya kupewa madaraka ya uongozi kwa sababu CHADEMA ina taratibu za watu kupata uongozi.
“CHADEMA hatugawi vyeo kama pipi na ninataka niwatoe hofu wana CHADEMA wote kuwa hakuna mwanya wowote wa mamluki kujipenyeza kukivuruga chama kama wengi wanavyodhani. Mabadiliko haya yanayoshuhudiwa sasa yameasisiwa na CHADEMA na yanaongozwa na viongozi wa chama kwa maslahi na faida ya chama,” alibainisha Golugwa.
Alisema wote watakaojiunga CHADEMA kutoka chama chochote cha siasa watapewa mafunzo na maelekezo ya kuwabadilisha fikra, mawazo, mwenendo na matendo yao ili kuachana na yale waliyokuwa wakifanya walikotoka na kuenenda kwa kufuata malengo ya CHADEMA ambayo ni ukombozi, haki na usawa kwa watu wote.
Katika kikao kilichopita, Millya na mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM ngazi ya taifa kutokea mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, walipewa onyo kali linaloambatana na adhabu ya kuwekwa katika uangalizi kwa mwaka mmoja kuanzia Agosti 3, mwaka jana.
Vijana hao sasa wako kwenye uangalizi huo hadi Agosti 3 na kwa hali hiyo, inaelezwa kwamba hawawezi kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama hicho katika uchaguzi wa mwaka huu.
Kutoka Mbeya, Angelica Sullusi anaripoti kuwa Baraza la Umoja wa Viajana wa chama hicho (UVCCM), mkoa wa Mbeya, limemvua madaraka kamanda wao wa mkoa, Dk. Steven Mwakajumilo, kwa kile kinachodaiwa kuwa misimamo yake mikali.
Habari ambazo gazeti hili limezipata na kuthibitishwa na Katibu wa UVCCM mkoa wa Mbeya, Ramadhan Kizinga, zinadai kuwa Dk. Mwakajumilo alivuliwa madaraka yake ya kuwa Kamanda wa UVCCM mkoani humo Jumamosi iliyopita na wajumbe wa baraza hilo waliokutana jijini Mbeya.
Kizinga alisema kuwa katika kikao cha baraza hilo walihudhuria wajumbe 27 na kuwa ajenda ya kumvua Dk. Mwakajumilo madaraka yake iliibuliwa na wajumbe hao ndani ya kikao na kutolewa maamuzi.
“Ajenda hiyo haikuandaliwa na Kamati ya Utekelezaji, iliibuka tu ndani ya kikao na wajumbe wakaamua kupiga kura ya kutokuwa na imani naye, kura za kumkataa zilipokuwa nyingi, wakapitisha uamuzi wa kumvua madaraka,” alisema Kizinga.
CHANZO Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment