Sunday, April 22, 2012

Mbowe, Slaa warusha makombora


MWENYEKITI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, wameipiga kijembe serikali ya CCM na wabunge wake.
Viongozi hao kwa nyakati tofauti na maeneo tofauti wamesema ufisadi utaendelea kulitikisa taifa kwa sababu ya mawaziri kurundikiwa madaraka sambamba na woga wa wabunge wa chama tawala kuwawajibisha mafisadi.
Mbowe anena
Akiwa bungeni jana Mbowe alisema ufisadi utaendelea kuitikisa nchi kutokana na mawaziri kurundikiwa madaraka na ili kuondokana na hali hiyo ni vema mfumo wa uendeshaji wa serikali ukabadilishwa. Alisema hilo lisipofanyika kila mara mawaziri watakuwa wanabadilishwa na ufisadi unabaki pale pale.
“Tusipo badilisha mfumo, mambo yatakuwa ni yaleyale, tutaendelea kuwalaumu mawaziri, serikali na wakurugenzi, lakini tatizo halitakwisha.
“Haiwezekani waziri mmoja anakabidhiwa kuongoza suala la madini na mafuta nchi nzima au suala la kilimo nchi nzima, mtu atakayeweza ni lazima awe na supernatural powers. Ukifanyika uzembe kwa waziri mmoja, nchi nzima inaingia gizani,” alisema na kushauri mamlaka kugawanywa katika majimbo na kusema kwa kufanya hivyo watakuwa wamepunguza mamlaka kwa mawaziri.
“Watu wanadhani serikali ya majimbo ni ya ubaguzi, yakiwa majimbo 7 au 8, hakika tatizo la ukabila halitakuwapo na pia tutakuwa tumepunguza mamlaka ya mawaziri. Hakuna mkoa utakaokosa rasilimali…tusitafute temporary solution.
“Ni lazima mawaziri wawajibike, lakini wakati tunaandika Katiba mpya nawaomba Watanzania kwa ujumla suala hili la serikali ya majimbo waliangalie kwa upana zaidi ili tuweze kutoka tukitaka tutoke hapa tulipo,” alisema.
DK. Slaa alia na wabunge wa CCM
Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mnadani, wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, Dk. Slaa alisema kama wabunge wa CCM wasingekuwa wanafiki Watanzania wasingekuwa masikini.
Alisema wabunge hao wameshindwa kuwawajibisha mafisadi ambao wamekuwa wakifanya ubadhirifu wa rasilimali za taifa bila kuwajibishwa.
Alibainisha kuwa unafiki wa wabunge hao umeonekana juzi baada ya kutakiwa kutia saini azimio la kuwataka wamuwajibishe waziri mkuu kwa kushindwa kuzuia ubadhirifu unaofanywa na mawaziri walio chini yake.
Dk. Slaa alisema Rais Kikwete naye kashindwa kuwawajibisha mafisadi ndiyo maana nchi inamuelemea na maisha ya Watanzania yanazidi kuwa magumu kadiri siku zinavyosonga mbele.
“Watanzania wanapaswa kujuta kwa kumchagua Rais Kikwete na CCM, nchi inamuelemea, mfumuko wa bei umeongezeka, maisha ya Mtanzania sasa ni hoi bin taaban. Haya ni majuto,” alisema.
Katika hatua nyingine, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wilayani Sengerema, John Tungu, alirejesha kadi ya chama hicho na kujiunga na CHADEMA.
Mnyika amshauri JK
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), alimtaka Rais Jakaya Kikwete kutumia mamlaka yake ya kikatiba kuwawajibisha watumishi ambao wanabainika kuwa mafisadi.
Alisema Watanzania wengi wanaendelea kuwa maskini kutokana na viongozi serikalini kutokuwa makini katika suala zima la uwajibikaji.
Alisema kutokana na viongozi kutokuwa wawajibikaji wamesababisha kuwepo kwa mfumko wa bei hususan katika masuala ya chakula.
“Kujiuzulu ni jambo moja, lakini kuwajibishwa ni jambo jingine hivyo kuna ulazima kama mawaziri ambao wanahusika hawatawajibishwa mambo yatakuwa ni yale yale, tukakuwa tunapiga kelele bungeni lakini hakuna kinachofanyika.
“Kwa mamlaka aliyonayo rais kutokana na Katiba anatakiwa kuwawajibisha watendaji ambao wanatuhumiwa na kubainika kuwa mafisadi ili kuweza kujenga heshima ya nchi na kuwatendea haki wananchi,” alisema Mnyika.

CHANZO - Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment