Sunday, April 22, 2012

MAKALA - Kama CAG anaweza, kwanini TAKUKURU na DPP Washindwe?! Hawa waondolewe mara moja

Kwa vyovyote iwavyo, ufisadi ndani ya nchi hii hautaisha wala kupungua endapo Edward Hossea na TAKUKURU yake pamoja na Eliezer Felleshi kama DPP wataendelea kuwa dhaifu katika utendaji wao! Tukiacha siasa za bingwa ni nani ambazo kimsingi zinatufanya tusiangalie upande wa pili wa mafanikio ya utendaji wa uongozi uliopo, basi utaona kwamba Rais Kikwete alijitahidi sana kutengeneza mfumo wa kitaasisi unaolenga kuzuia na kupapambana na ufisadi nchini. 

Tukiangalia historia ya TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), kabla ya JK ilifahamika kama TAKURU, yaani Taasisi ya Kuzui Rushwa. Ikaonekana kwamba kuzuia rushwa peke yake haisaidii, bali wanatakiwa pia kupambana nayo….na hapo ndipo ikabadilishwa toka Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) na kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Kiukweli, TAKUKURU wamepewa meno yote yanayostahili ili waweze kufanikisha malengo yake, lakini hata hivyo wameishia kupambana na vila na vitoa rushwa vidogodogo huku mapapa wa rushwa wakiachwa waendelee kuitafuna nchi. Badala yake, Edward Hossea amekuwa akipambana na rushwa kupitia vyombo vya habari pamoja na kwenye midaharo huku matokeo ya mapambano yake yakiwa hayaonekani! Wapo wanaoshawishika kuamini kwamba kiongozi wa nchi hampi uhuru Edward Hossea katika kutekeleza shughuli zake. Jambo hili haliingii akilini hata kidogo! Je, kwanini Edward Hossea azuiwe na Ludovick Utto aachwe kutenda shughuli zake kwa uhuru?! Amini amini nawaambia, ikiwa JK aliweza kumtosa Swahiba wake Mkuu Edward Lowassa, basi hawezi kuacha kumtosa yeyote ndani ya nchi hii; labda mwanafamilia wake!

Tukirudi katika uwezeshwaji wa kitaasisi katika suala zima la kutokomeza rushwa nchini, Mkagauzi Mkuu wa Hesabu Serikali (CAG) nae akapewa meno zaidi. Katika kuhakikisha Ofisi ya CAG haiishii katika kutoa ripoti za mapungufu ya mahesabu peke yake; humo wakajumuishwa TAKUKURU pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchni, yaani DCI. Lengo hapa lilikuwa kwamba, baada ya ukaguzi kupitia CAG kufanyika na madudu kuonekana basi madudu hayo moja kwa moja yapelekwe ama TAKUKURU au kwa DCI au wote kwa pamoja kutegemeana na aina ya madudu yaliyoanishwa na CAG. Hii maana yake ni kwamba, endapo pataonekana dalili za kuwepo kwa wizi, basi moja kwa moja DCI ishughulikie suala hilo na kuwafikisha mahakamani wahusika. Na endapo pataonekana kuwepo kwa dalili za rushwa ndani ya ukaguzi huo, basi moja kwa moja iripotiwe kwa TAKUKURU! Kwa bahati mbaya sana, si DCI wala TAKUKURU ambao wameonekana kwenda pamoja na kasi hii ya CAG. Endapo TAKUKURU na DCI wangefanya kazi zao ipasavyo, hivi leo kungekuwa na kesi nyingi mahakamani au majalada mengi yangekuwa yamewafikishwa kwa DPP.
Hata hivyo, DPP ni kansa nyingine na tena hatari zaidi ndani ya nchi hii! DPP amepewa nguvu kubwa sana kisheria kuhakikisha anaendesha shughuli zake pasipo na kuhofia! Hata hivyo, hii ni moja ya taasisi nyeti kabisa ndani ya nchi hii zenye kiongozi dhaifu asiyefaa kwa Alifu wala Be! Takribani miaka mitatu sasa, Edward Hossea amekuwa akiueleza umma kwamba wamepeleka majalada ya kesi kubwa sita kwa DPP. Hata hivyo, hakuna kesi hata moja mpaka sasa ambayo imepelekwa mahakamani kutoka ndani ya hizo kesi hizo sita KUBWA! 

Mapungufu ya Rais Jakaya Kikwete!
Kwa bahati mbaya sana, pamoja na nia yake inayoonekana katika kuziwezesha taasisi tajwa hapo juu bado ana udhaifu mkubwa mmoja! JK ni aina ya mzazi anayetoa kila kitu kwa mtoto wake. Ni aina ya wazazi ambao watanunua sare safi za shule, vitabu, madaftari na kila kitu kinachohusiana na masomo. Si hivyo, atatoa hadi ni pesa ya kutosha kabisa ya matumizi (pocket money)! Akishafika hapa, anaamini kwamba ameshamaliza kwa vile mtoto wake ni mtu mzima anayefahamu nini anatakiwa kufanya! Baada ya hapo hajishughulishi kuangalia endapo mtoto anaingia darasani au hapana; na kama anaingia nini maendeleo yake darasani! Huu ni ubovu mkubwa wa Rais wetu ambae ile tu kujenga taaisisi zenye nguvu anazani tayari amemaliza kazi!

USHAURI KWA JK!
KAMA JK alizijenga taasisi hizo kwa nia ya dhati ya kupambana na ufisadi nchini basi wakati umefika wa kuwawajibisha DPP pamoja na Mkurugenzi wa TAKUKURU. Si hivyo tu, hata DCI nae ame-prove failure! Hii ndio njia pekee ya kusafisha takataka za ufisadi nchini. Edward Hossea na Feleshi hawastahili kubaki ofisni mwao hata kwa siku moja ya ziada. Hawa wanapaswa kuondolewa mara moja bila kusitasita. Wale watakaongia, waanze mara moja na ripoti iliyotolewa karibuni na CAG pamoja na Kamati za Bunge. Pale panapoonekana harufu ya rushwa, basi bosi mpya wa TAKUKURU aanze nao…na pale palipo na dalili za wizi; DCI afanye kazi yake mara moja! Wakati umefika kwa hawa watu kupewa time frame/schedule of activitie! 

USHAURI KWA WABUNGE:
KWA vile imedhihirika wazi kwamba wakiamua kuacha ushabiki wa kichama wabunge wanaweza kuleta mabadiliko, basi waendelee na uzi ule ule kwa taasisi zingine. Waweke maslahi ya chama pembeni na kuangalia maslahi ya taifa! Kelele zilizopigwa bungeni dhidi ya Mkurugenzi wa TBS, tuzisikie zikipigwa dhidi ya Edward Hosea na DPP! Hawa watu ni kansa sugu ambayo katu haitaweza kupona kwa tiba ya mionzi! Hii ni kansa inayostahili kakata kiungo kizima kabla haijsambaa mwilini na kusababisha kifo chetu! Narudia, Edward Hossea na DPP hawafai….wabunge unganeni kuhakikisha kansa hizi zinaondolewa ikiwa Rais atashindwa kufanya hivyo. Ikibidi, onyesheni nia ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na rais ikiwa atashindwa kuwaondoa watu hao! Hata kama kura hiyo haitafanikiwa kutokana na sababu zilizo wazi, basi angalau mtakuwa mmeonesha hisia zenu kwamba hampo pamoja na rais kwa uwepo wa kansa hizi mbili nchini!

USHAURI KWA MFUMO WA KIMAHAKAMA.
Nchi hii kesi zipo nyingi kwelikweli na nyingine wala hazina dalili kwamba zitakuja kwisha! Matokeo yake, kesi zenye maslahi kwa taifa bado zimeendelea lurundikana mahakamani na hivyo kuwafanya watu wasitishike sana kiasi cha kuogopa kuacha ufisadi. Endapo kesi hizi zingekuwa zinatolewa maamuzi mapema wakati bado zipo hot, huenda baadhi ya watendaji wangeogopa! Ni kweli, zipo sababu zilizo wazi na za msingi zinazotokana na uchelewashwaji huu! Hata hivyo, ni lazima idara ya mahakama ijipange kuhakikisha kesi za ufisadi zinamalizwa mapema. Ikiwa ni vigumu kuanzisha mahakama maalumu za kushughulikia ufisadi basi tuwe na NIGHT COURTS ambazo zitashughulika na kesi hizi! Hii maana yake ni kwamba, hatutahitaji majengo mapya ya mahakama wala kuajiri mahakimu wapya! Hakuna sababu za mahakamani zetu kufunga ofisi saa tisa wakati bado kuna maelfu kwa maelfu ya kesi hazijafanyiwa kazi. Lazima shughuli za mahakama hivi sasa ziendeshwe kwa shift……mchana na usiku…..saa mbili hadi saa tisa na saa kumi hadi saa nne usiku! Hii itasaidia sana kupunguza mrundikano wa kesi!

USHAURI KWA JF MEMBERS.
TUACHE ushabiki wa kisiasa pembeni na kuangalia maslahi ya taifa kwanza! Tutumie jamvi hili kupiga kelele zisizo na mwisho kuhakikisha Edward Hossea na DPP wanaondoka! Zimwagwe hapa threads za mara kwa mara kuwachana live watu hawa! Tuache kuangalia upande wa viongozi wa kisiasa peke yake kwavile huko ndiko kutakosaidia kuvijenga vyama vyetu bali tuangalie na upande wa pili wa shilingi! Tuachane na ujuha wa kutamani serikali iharibu na kuvurunda zaidi ili iwe tiketi ya mafanikio ya kisiasa kwa upinzani!! Tunaweza kutamani hivyo na bado tukakuta CCM inarudi tena madarakani hapo 2015!

MAKALA hii ni ndefu, lakini pamoja na mambo mengine imelenga kupunguza idadi ya wachangiaji mamluki ambao wengi wao ni wavivu wa kusoma!
NAWAKILISHA! 



CHANZO - JF

No comments:

Post a Comment