Friday, April 27, 2012

Kamati Kuu ya Chadema kukutana leo


Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), inakutana leo jijini Dar es Salaam kwa kikao chake cha kawaida.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika, kwa vyombo vya habari jana ilieleza kwamba kikao hicho kitapitia nyaraka za ajenda mbalimbali kwa ajili ya mkutano wa baraza kuu.

Katika taarifa hiyo, Mnyika alisema kikao hicho kitafuatiwa na Mkutano wa Baraza Kuu utakaofanyika Aprili 29.

Alisema pamoja na mambo mengine, Baraza Kuu litaandaa ratiba na maelekezo kamili ya uchaguzi wa kichama ambapo uchaguzi utaanza ngazi za chini za msingi na matawi za chama na mabaraza mwaka 2012 na kuendelea mpaka ngazi ya taifa ya chama na vyombo vyake mwaka 2013.

Alisema mkutano wa baraza kuu utapokea taarifa ya hali ya siasa na kufanya maamuzi muhimu kuhusu mwelekeo wa chama na taifa.

“Mkutano huo utathibitisha mikakati, mpango kazi na bajeti ya chama kwa mwaka 2012/2013 pamoja na kufanya maamuzi muhimu kuhusu hali ya siasa nchini,” alisema.

Aliongeza kuwa “Chadema inaendelea kutoa rai kwa wananchi na wanachama kuendelea kukiwezesha chama kutimiza dhima yake ya kuhakikisha uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya Tanzania.” 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment