Monday, April 30, 2012

CCM yahofia kung’oka

SASA YATAKA MAWAZIRI WASHTAKIWE

HALI ya upepo mbaya wa kisiasa imedhihirika kukitisha Chama cha Mapinduzi ambacho katika namna isiyokuwa ya kawaida, kimeitaka serikali kuwatimua sio tu mawaziri bali hata makatibu wakuu na wakurugenzi wa wizara zilizotuhumiwa na Bunge kufuja fedha za umma.
Mbali na kuharakisha kuwafukuza, chama hicho pia kimeitaka serikali kuwatimua makatibu wakuu na wakurugenzi wa wizara zote zilizotuhumiwa kuhusika na ubadhirifu na kisha kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya dola kwa hatua za kisheria.
Hatua hiyo isiyokuwa ya kawaida imechukuliwa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi (NEC) wa CCM, Nape Nnauye, ambaye amekiri kwamba hali ya kisiasa kwa upande wa chama hicho ni mbaya.
Akizungumza katika maandamano ya Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao walivamia ofisi za chama hicho jijini Dar es Salaam jana, Nape alisema ili kurudisha imani ya wananchi lazima mawaziri waliotajwa katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), wawajibishwe, na kisha kufikishwa katika vyombo vya dola kwa hatua zaidi za kisheria.
Nnauye alisema haitakuwa jambo la busara kuwatimua mawaziri na kuwaacha makatibu wakuu na wakurugenzi ambao ndiyo watendaji wakuu katika wizara.
“Hatua ya kwanza kwa mawaziri hao ni kuwawajibisha kwa kuwavua madaraka ya uwaziri na hatua nyingine itafuata kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuwachunguza na kuwafikisha mahakamani.
Alisema kuwa suala la kuwahamisha halitakuwepo kama ambavyo imezoeleka, bali ni kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili kuleta heshima katika serikali ya Chama cha Mapinduzi.
“Tunajua wananchi wanasubiri kwa hamu juu ya kuvunja kwa baraza la mawaziri hivyo lazima ifanyike kwa haraka kutokana na mazingira yaliyopo sasa,” alisema Nnauye.
Wanafunzi hao waliandamana wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali wa kuwataka mawaziri waliotuhumiwa wanashtakiwa kama sehemu ya kujivua gamba ndani ya CCM.
Mweyekiti wa shirikisho hilo Assenga Abbakari alisema kama makada wa chama hakuna kurudi nyuma katika hilo na kudai kuwa ni vema wote wakakamatwa na kufilisiwa ili kuwa mfano kwa mawaziri na watendaji wengine wenye tabia ya kutafuna mali ya umma.


CHANZO - Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment