Sunday, September 1, 2013

Zitto: Utoroshaji fedha haramu ni mkubwa

MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, amesema kuwa mapato ya Bara la Afrika yanayopotea kutokana na utoroshwaji wa fedha haramu nje ya nchi ni makubwa kuliko fedha za msaada na za uwekezaji.
Aidha, amesema kuwa kiasi cha zaidi ya dola za Marekani bilioni 700 hutoroshwa nje ya bara hili kwa mwaka huku misaada kutoka nchi wahisani ikikadiriwa kufikia kiasi cha dola za Marekani bilioni 37, huku uwekezaji kutoka nje ukiwa ni dola za Marekani bilioni 40 kwa mwaka.
Zitto aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi juu ya mkutano wa 10 wa umoja wa Kamati za Mabunge za Hesabu za Serikali Kuu kutoka nchi wanachama wa SADC, (SADCOPAC) ambao unatarajiwa kufunguliwa Septemba 2, mwaka huu na Rais, Jakaya Kikwete.
Alisema kuwa ni jukumu la kamati za mahesabu ya umma kwenye kila nchi kufanya kazi yao ipasavyo ili kudhibiti utoroshwaji wa fedha haramu huku akianisha changamoto iliyopo kwenye baadhi ya nchi za Afrika ambapo hakuna kamati za mahesabu ya serikali huku nyingine zikiwemo Zambia na Swaziland kamati hizo hufanya kazi wakati wa vikao vya bunge.
“Mwaka 2011 Tanzania iliuza nje ya nchi tani 80,000 za korosho ambapo soko letu kuu ni India ambao walisema walipokea tani 120,000 zilizotoka kwetu, hii inaonesha tani 40,000 zilitoroshwa bila kulipiwa kodi wala Benki Kuu (BoT) haina taarifa nazo hivyo hawawezi kuzirudisha nchini kwa kuhofia kubainika,” alisema.
Akifafanua mbinu zinazotumika kusafirisha fedha haramu nje ya nchi, alisema kuwa Umoja wa Afrika (AU) unachangiwa na nchi zote wanachama kwa ajili ya kuuendesha lakini hakuna chombo cha kusimamia mahesabu yake, jambo alilosema kuwa ni miongoni mwa masuala watakayoyajadili ili kuweza kuyapatia ufumbuzi.
Awali Mwenyekiti wa SADCOPAC, Sipho Makama, kutoka nchini Afrika Kusini alisema kuwa mkutano huo utazikutanisha nchi zote za SADC isipokuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo kwa sasa hali yake si shwari kutokana na vita inayoendelea kati ya serikali na waasi wa M23.

No comments:

Post a Comment