Sunday, September 1, 2013

Dk. Slaa alivyoibadili Ukonga

Na Julias Kanyala
VIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa sasa wanapita katika maeneo mbalimbali nchini kuwaelewesha wananchi umuhimu wa kujadili kwa kina yaliyomo katika rasimu ya Katiba mpya.
Viongozi wakuu wa kitaifa wa chama hicho ndio wako mstari wa mbele katika kufanikisha suala hilo muhimu kwa ustawi wa taifa letu. Viongozi hao ni pamoja na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa.
Agosti 24, mwaka huu, Dk. Slaa alipata nafasi ya kuhutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Jimbo la Ukonga, uliohusu Mabaraza ya Wazi ya Katiba Mpya, uliofanyika katika Uwanja wa Kampala, Gongo la Mboto, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.
Katika mkutano huo Dk. Slaa anabainisha kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji mstaafu, Joseph Warioba, inawatakia mema Watanzania hivyo iungwe mkono.
Kuhusu Chama Cha Mapinduzi (CCM), anasema kuwa chama hicho hakitaki mabadiliko hapa nchini ndiyo maana kinabeza na kimejipanga kukwamisha baadhi ya mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba mpya.
Anasema viongozi na makada wa CCM wamekuwa wakiibeza rasimu hiyo iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuhofia kuwa itakiondoa madarakani chama chao.
Dk. Slaa anasema katika mapendekezo ya tume hiyo imeweka wazi kuwa serikali itakayoingia madarakani italazimika kuchukua hatua kuzuia dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa na upendeleo.
“CCM haitaki maneno hayo yawemo kwenye rasimu ya Katiba, wanajua wanavyotumia vitendo hivyo kuendelea kukalia madaraka,” anasema.
Dk. Slaa anasema Katiba mpya si ya Rais Jakaya Kikwete wala CCM bali ni ya wananchi. “Katiba ni ya wananchi, si ya Rais Kikwete wala CCM, wanaobeza rasimu hiyo wanapaswa waheshimu maoni ya wananchi kwani yaliyomo humo yote ni mawazo yaliyokusanywa kutoka kwa wananchi,” anasema.
Dk. Slaa anasema CHADEMA inaunga mkono mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba mpya yaliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba bila hofu yoyote, tofauti na CCM inayohofia utawala wake kuanguka kutokana na vipengele vingi vya rasimu ya Katiba kuminya yaliyokuwa yakikinufaisha chama hicho.
Anasema kuwa suala la Katiba mpya halikuwa ajenda ya CCM ndiyo maana viongozi wake walikuwa wakitoa matamko kupinga mchakato wake. Akiendelea kutaja baadhi ya yaliyomo katika rasimu hiyo, anasema kuwa moja wapo kuhusu suala la uchumi ni kuitaka serikali ihakikishe inachukua hatua za kuwaletea wananchi maisha bora na kuondoa umaskini lakini 

Bonyeza Read More Kuendelea

CCM hawataki wananchi waondolewe umaskini ili waendelee kuwatawala kwa urahisi, na kusisitiza kwamba CHADEMA yenyewe inakubaliana na mawazo hayo.
Anabainisha kuwa tume hiyo inapendekeza Katiba iseme kuwa rais atakayeahidi jambo akiingia madarakani asipotekeleza ashitakiwe lakini CCM wanakataa, CHADEMA wao wanakubaliana na pendekezo hilo.
Dk. Slaa anasema chama chao kinaunga mkono hoja ya serikali tatu, kwakuwa ndiyo suluhu la matatizo ya muungano. Anatoa mifano ya Sudan na Sudan Kusini, Eritrea na Ethiopia, kuwa muungano wa nchi hizo ulilazimishwa na matokeo yake ulisambaratika.
Akizungumza kuhusu Tume Huru ya Uchaguzi, anasema CHADEMA inakubaliana na pendekezo hilo, pia nchi kuwa na Tume ya Maadili ya Uongozi na yawe bayana lakini CCM hawakubaliani na hoja hiyo.
Kuhusu suala la udini, anasema uhuru wa miaka 50 unaosifiwa, ulipatikana kwa kuzingatia ibara ya 19 ya Katiba iliyopo inayotambua uwepo wa dini mbalimbali.
“Serikali haina dini, Watanzania ndio wenye dini. Ni wajibu wa serikali kuwalinda, wafanye ibada bila bughudha. Tumuunge mkono kupinga udini na kudumisha amani ili tuishi kama ndugu,” anasema Dk. Slaa.
Katika mkutano huo, Dk. Slaa alionesha mshangao kuwa wananchi wanatakiwa kujadili rasimu ya Katiba mpya wakati hata ile ya zamani hawaifahamu, hivyo itakuwa vigumu kulinganisha na kujua utofauti.
Anawaeleza wananchi waliokuwa wamefurika uwanjani hapo kuwa lengo la CHADEMA ni kuwapa ufafanuzi ili wanapojadili wajue wanajadili kitu gani.
Anasisitiza kuwa lazima wananchi waelewe kuwa hadi leo taifa linayumba kwa sababu ndani ya Katiba tuliyonayo haina malengo madhubuti ya kumkomboa Mtanzania. Anatanabaisha kuwa kuna mambo mengi ya msingi hayamo katika Katiba tuliyonayo na hayamo pia katika Katiba mpya.
Anatolea mfano wa wawekezaji wanaokuja kuwekeza hapa nchini kuwa wao ndio wanakuwa na nafasi ya kuipa nchi masharti badala ya wao kuwekewa masharti kama ilivyo katika nchi nyingine.
Katika mkutano huo CHADEMA Jimbo la Ukonga waliwagawia wananchi waliohudhuria rasimu za katiba mpya, hivyo ilikuwa rahisi kuchangia maoni yao bila usumbufu.
Tanzania Daima Jumapili ilipata nafasi ya kuwahoji baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kuhusu kugawiwa rasimu za Katiba mpya na uongozi wa Jimbo la Ukonga, ambapo walikiri kuwa walifurahishwa na utaratibu huo.
Naye Katibu wa CHADEMA wa Jimbo la Ukonga, Jumaa Mwipopo, ambao ndio walikuwa wenyeji wa mkutano huo, anasema kuwa waliomba kutoka katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba rasimu za Katiba 8,000 pamoja na vitabu vya Sheria za Mabaraza ya Katiba 1,000 ili kuwagawia wakazi wa jimbo hilo, ikiwa ni maandalizi ya ujio wa Dk. Slaa katika mkutano huo.
Anasema lengo kuu ni kuwawezesha wakazi wa Jimbo hilo kutambua upungufu uliomo katika rasimu ya Katiba mpya na kutoa maoni yao.
Akitoa maoni yake kuhusu rasimu hiyo ya Katiba mpya, Mwipopo anapendekeza Katiba mpya iwe na kipengele kinachoruhusu kupata matibabu ya dharura. Akilinganisha na Katiba ya nchi ya Kenya, anasema wao wameweka kipengele hicho katika katiba yao mpya, ambapo watu wanaokwenda hospitali wanakwenda bila kuwa na fomu zinazoitwa PF 3 kutoka polisi, tofauti na hapa kwetu ambapo mtu analazimika kuwa nayo hata kama yu mahututi, vinginevyo hawezi kutibiwa, lakini wao Kenya mgonjwa anatibiwa kwanza ndipo PF 3 inafuata baadaye.
Akizungumzia kusuala la haki za Kiuchumi na kijamii anasema: “Kwa mfano Katiba mpya ya Kenya Ibara ya 43, kuna kitu kinaitwa ‘Economic and Social Right’. Haki za kiuchumi na kijamii, ambapo kila mtu ana haki ya kuwa na afya bora, haki ya uzazi, haki ya watoto, haki ya kupata makazi na mazingira bora na haki ya kupata maji safi na salama.
“Mambo haya ni muhimu tuyaingize sisi pia katika Katiba yetu ijayo. Kwa kuwa hayamo katika Katiba tunayoitumia sasa, ndiyo maana hadi leo serikali yetu suala la maji safi na salama halipewi kipaumbele kwa Watanzania.”

No comments:

Post a Comment