Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimedai Tume ya Mabadiliko ya Katiba haijapokea makasha yaliyojaa taarifa za michango ya wananchi kuhusu rasimu ya katiba, yaliyokusanywa na chama hicho kutoka mikoa mbalimbali, kwa maelezo kuwa hakuna sehemu ya kuyaweka.
Tume hiyo ilikataa kupokea maboksi zaidi ya 36 yaliyofikishwa kwenye ofisi zake zilizoko Mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam, kwa madai ya kukosa eneo la kuyahifadhi, kwa mujibu wa , Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa.
Hata hivyo waliwasilisha mihtasari ya maoni hayo iliyokusanywa kwenye vitabu viwili vilivyokabidhiwa maofisa wa tume hiyo.
Akizungumza na wanahabari jana jijini baada ya kuwasilisha maoni ya mapendekezo ya wananchi kwenye ofisi hiyo,alisema wameshangazwa na utaratibu wa tume hiyo kushindwa kuyapokea makasha hayo kwa madai kuwa hakuna sehemu ya kuyahifadhi.
Dk. Slaa alisema huko ni kuonyesha jinsi gani tume hiyo haijajipanga katika kupokea maoni waliyoyawasilisha kwani hawana mpango wa kupokea vidhibiti vilivyokusanywa baada ya kuzunguka nchi nzima.
Chadema ilirudisha shehena hiyo ya makasha yalikuwa yamepakiwa kwenye gari aina ya Pick Up yenye nembo ya M4C-vuguvugu la harakati za mabadiliko.
Dk. Slaa alisema wamewasilisha maoni ya wananchi milioni 3.5 yakiwa na hoja mpya 66 lakini pia yakiunga mkono kuwapo serikali tatu.
Akizungumzia maoni ya serikali tatu alisema wananchi wamependekeza pamoja na kuelezea sababu za kuwa na muungano wa sura hiyo na kueleza kuwa anamshangaa mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombale-Mwiru kupinga suala hilo . Alisema kuwa huenda inatokana na umri wake kwani wazee hufika kipindi wakachoka kama ilivyo kwa Kingunge.
Aliongezea "hayo anayoyasema kuwepo kwa serikali mbili kuna mafanikio ni yapi ama kujengwa kwa shule na zahanati hatuwezi kulazamisha Muungano kuna nchi ambazo zinapigana vita kwa ajili ya kulazimishana Muungano.”
Akizungumzia jinsi walivyokusanya maoni alisema njia sita zilitumika ikiwamo mabaraza ya wazi kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha marekebisho ya sheria, mabaraza ndani ya kata, kwenye majimbo pamoja na njia ya mtandao yanatumiwa.
Alisema licha ya kukusanya maoni hayo, tume ina usiri na kuitaka kufanya kazi kwa uwazi na siyo kuwazui waandishi wa habari kuingia na kusikiliza maoni yao waliyokuwa wakiyawasilisha. Alisema kitendo hicho kinaonyesha dhairi kuwa kuna kitu wanataka kukificha ama tume yenyewe haijajipanga kupokea maoni kwa watu walio makini.
"Nimeshangazwa na tume sijaelewa ni kwa nini wafanye kazi zao kwa siri badala ya uwazi waandishi wa habari ni chombo cha umma kwanini wazuiliwe kuingia ndani kusikiliza kile tulichokuwa tunakieleza hii katiba ijulikane siyo ya Chadema , CCM wala Jaji Joseph Warioba ni ya wananchi," alisema
No comments:
Post a Comment