Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeweka hadharani maoni kuhusu rasimu ya katiba kiliyoyakusanya kutoka kwa wananchi nchi nzima huku kikionyesha wasiwasi wake juu ya uwezekano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuyachakachua kwasababu yamepiku yale yaliyokusanywa na CCM.
Chadema pia kimemkosoa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kufuatia kauli yake kwamba tume yake haitapokea maoni yanayokusanywa kwa Chopa wakati hakuna sheria inayokataza maoni kukusanywa kwa helikopta.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Wilbroad Slaa, alisema jana wakati akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.
Alisema njia zilizotumika ni pamoja na mikutano ya mabaraza ya katiba ya wazi, katika makao makuu ya wilaya, mabaraza ya ndani katika makao makuu ya majimbo 349, ujumbe mfupi wa simu ya mkononi, barua pepe (email) na mitandao ya kijamii kama Jamii Forum na Facebook.
Dk. Slaa alisema kwa kutumia njia hizo jumla ya watu walioshiriki kutoa maoni yao ya rasimu ya katiba mpya kwenye mabaraza ya Chadema ni 3,462,805 na mikutano iliyofanyika kwa nchi nzima ni 190.
Alisema katika mabaraza ya katiba ya kata 586 yaliyoendeshwa na madiwani wa Chadema maoni yaliyokusanywa ni 117,274, mabaraza ya katiba ya wazi 3, 200, 889, mabaraza ya katiba ya ndani 130,004, barua pepe 612, ujumbe mfupi wa simu ya mkononi 12,345 na mitandao ya kijamii.
Aliongeza kuwa kwa kutumia njia hizo ambazo ziliwarahisishia wananchi Chadema pia ilipokea maoni ya Watanzania waliopo nchi za Uingereza, Marekani, Botswana na Zambia ambayo waliyatuma kwa njia ya barua pepe.
“Kinana (Katibu Mkuu wa CCM) alijigamba kuwa maoni waliyokusanya kutoka kwa watu 2,600,000 haiwezi kufikiwa na chama chochote cha siasa tunataka watoe mchanganuo na ushahidi jinsi walivyokusanya maoni yao maana sisi tumewapiku,” alisema Dk.Slaa.
Dk.Slaa alisema wakati wa kukusanya maoni yao walikumbana na changamoto nyingi ikiwamo baadhi ya watu kulishwa maneno na CCM kutetea mfumo wa serikali mbili na kupinga serikali tatu kwa madai ni gharama lakini kila wanapobanwa maswali wanakosa hoja.
Alisema CCM lazima watambue kuwa haiwezi kuendesha nchi 'kimagumashi' kwani hivi sasa Watanzania hawakubali kudhalauliwa na vyama vya siasa kwa kuwa wana uelewa mkubwa na kwamba Chadema inakubali kwa asilimia 80 mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwenye rasimu.
Katibu Mkuu huyo alitoa mfano wa maoni yanayopendekezwa na Chadema ni mfumo wa serikali tatu ambao utakuwa ni serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment