CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji mstaafu, Joseph Warioba, inawatakia mema Watanzania hivyo iungwe mkono.
Chama hicho kimesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), hakitaki mabadiliko hapa nchini ndiyo maana kinabeza na kimejipanga kukwamisha baadhi ya mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba mpya.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, katika mikutano ya mabaraza ya wazi ya Katiba mpya.
Alisema viongozi na makada wa CCM wamekuwa wakiibeza rasimu hiyo iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Joseph Warioba kwa kuihofia kuwa inakiondoa madarakani chama chao.
Alisema katika mapendekezo ya tume hiyo imeweka wazi kuwa serikali itakayoingia madarakani italazimika kuchukua hatua kuzuia dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa na upendeleo.
“Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakitaki maneno hayo yawemo kwenye rasimu ya Katiba, wanajua wanavyotumia vitendo hivyo kuendelea kukalia madaraka,” alisema.
Dk. Slaa alisema Katiba mpya si ya Rais Jakaya Kikwete wala Chama Cha Mapinduzi (CCM) bali ni ya wananchi.
“Katiba ni ya wananchi, si ya Kikwete wala CCM, wanaobeza rasimu hiyo wanapaswa waheshimu maoni ya wananchi kwani yaliyomo humo yote ni mawazo yaliyokusanywa kutoka kwa wananchi,” alisema.
Dk. Slaa alisema CHADEMA inaunga mkono mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba mpya yaliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Dk. Slaa alisema CCM ina hofu na utawala wake kutokana na vipengele vingi vya rasimu ya Katiba kuminyaminya yaliyokuwa yakikinufaisha chama hicho tawala.
Alibainisha kuwa suala la Katiba mpya halikuwa ajenda ya CCM ndiyo maana viongozi wake walikuwa wakitoa matamko kupinga mchakato wake.
Dk. Slaa alisema katika uchumi tume imependekeza kuwa serikali ihakikishe inachukua hatua za kuwaletea wananchi maisha bora na kuondoa umaskini.
Alisema CCM hawataki wananchi waondolewe umaskini ili waendelee kuwatawala kwa urahisi, lakini CHADEMA inakubaliana na mawazo ya Tume ya Warioba.
Alibainisha kuwa Tume ya Warioba inapendekeza Katiba iseme kuwa rais atakayeahidi jambo ama utekelezaji wake akiingia madarakani asipotekeleza ashtakiwe lakini CCM wanakataa huku CHADEMA wakilikubali.
Dk. Slaa alisema chama chao kinaunga mkono hoja ya serikali tatu, kwakuwa ndiyo suluhu la matatizo ya muungano.
Alitoa mifano ya Sudan na Sudan Kusini, Eritrea na Ethiopia, kuwa muungano wa nchi hizo ulilazimishwa na matokeo yake ulisambaratika.
Alibainisha kuwa rasimu inataka wawekezaji walinde masilahi ya ndani si kuweka masharti hata kwa mambo tunayoyaweza.
“CHADEMA kinaunga mkono tume huru ya uchaguzi, kinakubaliana na nchi kuwa na tume ya maadili ya uongozi na yawe bayana lakini wenzetu wa CCM hawataki,” alisema.
Kuhusu suala la udini, alisema uhuru wa miaka 50 unaosifiwa ulipatikana kwa kuzingatia ibara ya 19 ya Katiba iliyopo inayotambua uwepo wa dini mbalimbali.
“Serikali haina dini, Watanzania ndio wenye dini. Ni wajibu wa serikali kuwalinda, wafanye ibada bila bughudha. Tumuunge mkono kupinga udini na kudumisha amani ili tuishi kama ndugu,” alisema Dk. Slaa.
No comments:
Post a Comment