Sunday, August 25, 2013

Mbowe ashauri mambo muhimu kuwekwa wazi kwenye Rasimu

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewataka wananchi kutoa maoni yao kwenye rasimu ya mchakato unaoendelea wa kuundwa kwa katiba mpya huku kikishauri mahitaji yote muhimu yawekwe wazi.
Akizungumza katika mikutano ya hadhara ya kuhamasisha wananchi kutoa maoni yao iliyofanyika wilayani Mbinga, Namtumbo na Songea, mkoani Ruvuma kuhusu mchakato huo, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema maji ni moja ya mahitaji muhimu ya kila mwanadamu hivyo ni jukumu la serikali kuhakikisha kila mwananchi anapata maji safi na salama kwa ajili ya ustawi wa maisha yao ya kila siku.
Amesema kumekuwapo na kasumba miongoni mwa baadhi ya viongozi na wananchi kuwa huduma hiyo inatolewa kwa msukumo na utashi wa viongozi na inatafsiriwa kuwa ni hisani ikiwa kiongozi atajisikia kufanya hivyo lakini ikiwekwa kwenye katiba itamtaka kila kiongozi kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama na kilio kisichoisha cha ukosefu wa maji katika maeneo mbalimbali nchini kitapungua kama siyo kutoweka kabisa.
Akizungumzia suala la elimu na lugha ya kufundishia kuanzia ngazi ya elimu ya msingi na kuendelea, alisema katiba inapaswa kutamka wazi kuwa lugha ya Kiingereza ndiyo lugha ya kufundishia na umuhimu wa lugha ya taifa ambayo ni Kiswahili upewe kipaumbele badala ya kuendelea na mfumo uliopo ambao umekuwa ni wa huria zaidi na kusababisha kuwapo kwa matabaka katika sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa huku akishauri lugha za asili zisipuuzwe kwa ajili ya kulinda na kudumisha utamaduni wa Watanzania.

No comments:

Post a Comment