Saturday, August 31, 2013

Msingwa ahoji CCM kutolipa kodi

MBUNGE wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (CHADEMA), amehoji sera ya Chama cha Mapinduzi ya kutokusanya kodi wakati yenyewe hailipi katika maeneo yao ya viwanja, majengo na vibanda vya biashara.
Msigwa alihoji jambo hilo bungeni mjini jana alipokuwa akiuliza swali la nyongeza.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuye Salum, alisema si sera ya CCM kushindwa kukusanya kodi ya majengo, bali majengo mengi hayalipiwi kodi.
“Majengo mengi hayalipiwi kodi, ila baada ya kumaliza kufanya kazi ya kuthaminisha majengo, watu wote watalipa kodi hata jengo lako Msigwa na najua hilo nimelisema kutokana na itikadi yako tu na si vinginevyo,” alisema.
Pamoja na hayo, alikiri kuwepo kwa majengo mengi katika maeneo mbalimbali nchini ambayo hayalipiwi kodi na kuwa baada ya kazi ya kufanyiwa tathmini watahakikisha yanalipiwa kodi.
Awali, Mbunge wa Tumbe, Rashid Ali Abdallah (CUF), alitaka kujua kuna aina ngapi za kodi, ushuru, na kuwa watu wangapi wanategemewa kulipa kodi na wangapi kwa kuzingatia idadi ya watu milioni 43.9 Tanzania Bara.
Akijibu swali hilo, naibu waziri huyo alisema Tanzania kuna kodi na ushuru wa aina mbili, ambazo ni kodi zinazosimamiwa na serikali kuu na zile zinazosimamiwa na serikali za mitaa.
Alisema Serikali Kuu inatoa kodi na ushuru katika kodi ya ongezeko la thamani, kodi ya ushuru wa magari, ushuru wa viwanja vya ndege, ushuru wa bandari na tozo ya maendeleo ya ufundi na elimu.
Mkuya alisema kwa upande wa serikali za mitaa, hutoza ada mbalimbali kwa mujibu wa sheria ya fedha ya serikali za mitaa.
Aliongeza kuwa si wafanyabiashara wote wanaotakiwa kulipa kodi, bali ni wale wenye kipato cha zaidi ya sh milioni 4 kwa mwaka na ni lazima apate usajili wa mlipa kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Hadi kufikia Julai, mwaka huu, idadi ya walipakodi waliosajiliwa walikuwa ni 1,199,942, walipakodi ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni 21,659 na jumla ya waajiri 92,510 wanawasilisha kodi za watumishi (PAYE),” alisema Mkuya.

No comments:

Post a Comment