Sunday, May 19, 2013

Mdee amlipua Chenge


ASEMA HAKUITENDEA NCHI HAKI KWENYE MIKATABA
MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA) amemlipua Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani, Andrew Chenge, akisema kuwa alishiriki kwenye mikataba ya madini, lakini hakuitendea haki nchi yake.
Halima alitoa madai hayo jana mjini hapa katika semina kwa wabunge kuhusu rasimu ya sera ya gesi asili iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini na kufanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa.
Mbali na Mdee pia baadhi ya wabunge nao walizungumza wazi kuwa viongozi walioishauri nchi kuingia katika mikataba ya kifisadi ndiyo hao hao wanaisukuma ifanye haraka kuingia tena kwenye mikataba ya gesi asili hata kabla ya kuwepo kwa sera, sheria na kanuni.
Mdee alisema kuwa serikali imepuuza vurugu za kugombea rasilimali hiyo zilizotokea Mtwara na Lindi, na hivyo akataka umakini uwepo kwenye sera na sheria mpya ya gesi ili nchi isirudi kwenye mikataba mibovu kama ile ya madini ya migodi ya Geita, Bulyankhulu na mingine.
“Mheshimiwa Chenge alishiriki kuishauri serikali kwenye mikataba ya madini, lakini hakuitendea haki nchi yetu,” alisema Mdee.
Hoja ya Mdee ilikolezwa na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keisy (CCM) ambaye licha ya kutomtaja Chenge kwa jina, lakini alionekana kumlenga yeye kwani wakati huo ndiye alikuwa mwanasheria mkuu wa serikali.
Alisema wataalamu walioiingiza nchi kwenye mikataba mibovu wakatwe vichwa na kuitaja baadhi ya mikataba hiyo kuwa ni ile ya ununuzi wa rada na ubinafsishaji wa Shirika la Ndege la Taifa (ATC).
Chenge ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Bariadi Magharibi naye alipata nafasi ya kuchangia katika rasimu hiyo ambapo alisema kuwa wabunge wanaweza kukataa nchi isichimbe gesi kwa kumsingizia hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyetaka wapatikane wataalamu wetu kwanza.
Alisema watu wamekuwa wakimsingizia Nyerere kuwa alizuia rasilimali zisichimbwe na kufafanua kuwa wabunge wapende au wasipende lazima nchi iingie kwenye mikataba hiyo haraka.
“Watanzania tusiogope, sisi ndio viongozi wa sasa. Tuangalie penye kasoro na tusahihishe. Lakini napenda kuwahakikishia kuwa hatujawahi kufanya mambo gizani,” alisema.
Kauli yake ilionekana kupingwa na baadhi ya wabunge ambapo Mbunge wa Dole, Slyvester Mabumba alipoinuka kuchangia alianza kuomba radhi kuwa asieleweke vibaya kwa atakachokisema.
“Walioiingiza nchi kwenye mikataba mibovu ya Richmond na IPTL yawezekana wamo humu ndani, hivyo kama wizara wanakiri kuwa bado hatuna wataalamu wa kutosha tunaharakia nini?” alisema na kuhoji.
Madgalena Sakaya wa Viti Maaalumu (CUF) alipingana na kauli ya Chenge ya kuitaka Tanzania ifanye haraka kuingia mikataba ya utafutaji na uchimbaji gesi asilia akisema kuwa wananchi wameishaumwa na nyoka.

Bonyeza Read More Kuendelea



Alisema kuwa sera na sheria ya gesi asilia lazima iseme kuhusu utunzaji wa mazingira kwani ile ya mafuta ilikuwa kimya na hivyo kuwapa mwanya wawekezaji kuharibu mazingira watakavyo.
“Serikali hii siyo ya kwanza wala ya mwisho, sasa kutaka kila kitu kifanyiwe kazi leo inaonesha kuwa hakuna nia njema. Viko vizazi vitakuja na ujuzi mwingine, haraka hii ya nini ya kutaka kumaliza kila kitu,” alisema.
Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje aliunga mkono kauli ya Mdee akisema kuwa lazima kuwe na uwazi kwenye mikataba ya gesi itakayosainiwa ili kuepuka kujirudia kwa makosa yale yale.
“Mwizi aliyekuibia jana, leo hawezi kuwa mshauri wa ulinzi wa nyumba yako. Wale walioishauri serikali kuingia kwenye mikataba mibovu ndio hao wanashauri tena tuingine kwenye mikataba ya gesi haraka,” alisema.
Wabunge wengine waliopata fursa ya kuchangia nao waliunga mkono wenzao wakisema kuwa rasilimali zinazopatikana eneo lolote nchini ni za Watanzania wote na hivyo kupendekeza wananchi wapewe elimu ya kutosha pamoja kuwekewa mazingira ya kunufaika na uwekezaji.
Walipendekeza kuwa sera inapaswa kuwawezesha Watanzania kuwa na hisa kwenge gesi hiyo, lakini wakataka ioneshe muda maalumu wa kukamamilika wa sera, sheria na kanuni.
Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangala (CCM) alitaka sera, sheria na kanuni za gasi asilia viwepo kwanza ndipo mikataba ifungwe ili kuepusha migogoro.
Mapema akifungua semina hiyo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema kuwa wale wanaopotosha kuwa wizara imegawa vitalu wana ajenda yao ya siri ya kuikwamisha nchi kiuchumi.
Alifafanua kuwa kilichofanyika ni kutangaza vitalu hivyo ili wawekezaji waombe na kwamba Oktoba 25 mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete atafungua rasmi mpango huo wa kujitangaza.
“Mei 9, 2014 tunafungua hizo tenda kwa wale waliochukua nyaraka zetu na kesho yake tarehe 10 ndipo tunaanza kuvigawa hivyo vitalu. Wakati huo sera na sheria mpya ya gesi itakuwa imeshapitishwa na kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili,” alisema.
Alisema kuwa uchumi ni umeme na kwamba hakuna njia ya mkato, lazima kuzalisha umeme wa gesi wapende ama wasipende.

No comments:

Post a Comment