Sunday, May 19, 2013

BUNGENI: CHADEMA inavyomnyima usingizi Ndugai


WIKI hii yametokea mambo mengi bungeni mjini hapa lakini kubwa kabisa ni kitendo cha Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuonesha wazi kuwa huenda Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinamnyima usingizi, hivyo anajaribu kutafuta kila mbinu kukidhibiti bila mafanikio.
Pasipo kutarajia, Ndugai aliliambia Bunge kuwa wabunge wake wanaovaa kombati bungeni wajitazame upya wasije kutolewa nje kwa kukiuka kanuni.
Ndugai alitoa kauli hiyo muda mfupi kabla ya kuliahirisha Bunge, Jumatatu jioni akidai kuwa amekuwa akiandikiwa ujumbe mfupi na baadhi ya wabunge wakihoji kama kanuni zinaruhusu uvaaji wa kombati bungeni.
Kombati ni aina ya vazi ambalo huvaliwa na viongozi na wafuasi wengi wa CHADEMA likiwa na rangi tofauti ambazo hata hivyo hazifanani na alama za rangi zilizopo kwenye bendera ya chama hicho.
Kutokana na umaarufu wa vazi hilo lililoasisiwa na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, wabunge wengi wa chama hicho hususan wanaume wameshona suti kwa muundo wa vazi hilo ambazo huzivaa bungeni.
“Sasa nikumbushe tu kuwa nawaomba tukaitazame kanuni ya 149 (3)(a) kwa wanawake na (b) kwa wanaume, tutaona aina za mavazi tunayopaswa kuvaa humu ndani,” alisema Ndugai huku wabunge wa CHADEMA wakimcheka.
Alisema kuwa ziko kombati za rangi mbili, nyeusi na kaki zinavaliwa bungeni, kwamba na wengine wanataka kuja na kombati za rangi ya kijani.
Wakizungumzia kauli hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika, walisema kuwa Ndugai anafanya porojo za kisiasa bungeni.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, aliliambia Tanzania Daima Jumapili kuwa kombati ni mavazi yanayoruhusiwa na kanuni za Bunge.
“Kombati hizi ni safari suits, hivyo maelezo ya Naibu Spika ni porojo za kisiasa tu,” alisema.
Naye Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo alisema kuwa kwa mujibu wa kanuni tajwa hapo juu, vazi la wanaume linaloruhusiwa ni pamoja na suti za safari.
Alisema kuwa kombati inaangukia katika kundi hilo kutegemeana na namna ilivyotengenezwa na kwamba ni halali.
“Kombati ambazo zimekuwa zikivaliwa na wabunge wetu mfano nyeusi hazijakiuka kanuni yoyote ya Bunge. Hivyo, Ndugai alilenga kutishia au kupindisha tafsiri ya kanuni,” alisema Manyika.
Filikunjombe atoa kali bungeni
Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), ametoa mpya bungeni akidai kuwa wapiga kura wake hawajawahi kusherehekea uhuru badala yake wamekuwa wakiwatazama Watanzania wengine wakifanya hivyo kwa miaka 50.
Filikunjombe alitoa kauli hiyo wakati akichangia hoja ya bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka 2013/2014, akimshukuru Waziri wa wizara hiyo, John Magufuli, kuwa kwa mikakati yake ni dhahiri Ludewa wataona barabara za lami kwa mara ya kwanza tangu uhuru.
“Wakati Watanzania wakisherehekea miaka 50 ya uhuru, sisi Ludewa tumekuwa tunatazama tu, lakini sasa nimshukuru Waziri Magufuli kwa mipango yake itakayowezesha kupata barabara ya lami kwa mara ya kwanza.
“Naomba mkakati huu uende haraka na lami hiyo ikikamilika kwa mara ya kwanza wananchi wa Ludewa wataanza kusherehekea mwaka wa kwanza wa uhuru,” alisema Filikunjombe.

Bonyeza Read More Kuendelea




Magufuli abanwa kufafanua bil. 252/-
Kambi rasmi ya upinzani bungeni imefichua malipo ya madeni hewa mradi usio halisi ambao uligharimu fedha za serikali sh 252,975,000,000 kupitia Wizara ya Ujenzi.
Msemaji Mkuu wa kambi hiyo kwa Wizara ya Ujenzi, Said Arfi (CHADEMA) alihoji hilo wakati akiwasilisha maoni yao kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
“Katika hotuba ya kambi rasmi ya upinzani bungeni kwenye bajeti ya mwaka 2011/2012 tulihoji kuhusiana na fedha zilizokuwa zimetengwa chini ya fungu lililojulikana kama ‘Special Road Construction Project,’” alisema.
Aliongeza kuwa wamelazimika kulikumbusha Bunge kuhusiana na suala hilo kwani kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka husika wa fedha kuhusiana na kifungu hicho, alionesha kasoro hiyo.
“Malipo ya madeni ya mwaka wa nyuma yaliyolipwa kwa fedha za 2011/2012 kwa kutumia jina la mradi usio halisi ni sh 252,975,000,000. Miradi katika wizara ilipewa namba 4168 kwa ajili ya kupitisha malipo ya madeni ya miaka ya nyuma kwa miradi inayotekelezwa na Tanroads. Namba hii si halisi,” alinukuu taarifa ya CAG ukurasa wa 160, fungu la 98.
Hata hivyo wakati Bunge limekaa kama kamati kupitisha bajeti hiyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, alizidi kumbana Magufuli afafanue kuhusu matumizi ya fedha hizo, ambapo aliendelea kudai kuwa zilitumika kulipa makandarasi.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alilazimika kutumia ubabe ili kumnusuru Magufuli akisema kuwa kwa vile Zitto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, suala hilo litajadiliwa na kamati yake.
Watoto wa vigogo CCM wahojiwa
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdalah Kigoda, alibanwa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, akitakiwa kuwataja wamiliki wa Kampuni ya kufua umeme wa upepo mkoani Singida ya Power Pool East Africa.
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa wizara hiyo, Higness Kiwia (CHADEMA), alitoa kauli hiyo wakati akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kwa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara 2013/2014.
Kiwia alisema kuwa zipo habari za kuaminika zikionesha kuwa wamiliki wa mradi huo ni ndugu na jamaa wa wabunge na mawaziri wa CCM.
Alitaja majina hayo kuwa ni Maswa Kagoswe, Isaac Joseph Mwamanga, Emmanuel Kasyanju, Prosper Tesha, Leonard Tenende na Athuman Ngwilizi, akisema kuwa inadaiwa wametumia ushawishi wao serikalini kupata ubia huu ili kufaidika kifedha.
“Mheshimiwa Spika, mradi huu ambao unashirikisha Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni binafsi inayoitwa Power Pool East Africa Ltd kwenye mradi wa nishati, umeme kwa nguvu za upepo, ambao upo takriban kilometa 12 mashariki mwa Halmashauri ya Singida,” alisema.
Alisema kuwa mradi unatarajiwa kuzalisha jumla ya megawati 300, lakini utaanza kuzalisha megawati 50, na kwamba kwa mujibu wa Power System Master Plan (PSMP) mradi ulitarajiwa kuanza rasmi mwaka 2012/2013.
Kiwia alinukuu randama ya wizara hiyo ukurasa wa 55 ambayo inasema kuwa wizara inaendelea kushughulikia upatikanaji wa fedha dola za Marekani milioni 136 kutoka EXIM Bank ya China ambayo imekubali kutoa mkopo wenye masharti nafuu na tayari ridhaa ya serikali imewasilishwa EXIM Bank na Wizara ya Fedha.
“Kambi Rasmi ya Upinzani, inataka kujua Kampuni ya Power Pool East Africa iliwezaje kupata ubia huu na NDC na ni kwa nini NDC kwa kushirikiana na serikali ndiyo imeenda kutafuta fedha za mradi huu kwa kutumia ‘guarantee’ ya serikali?” alihoji.
Kiwia aliongeza kuwa wanataka kujua kama serikali ilifanya uchunguzi wa kina (vetting), juu ya wamiliki, uwezo na uhalali wa kampuni hiyo katika kuzalisha umeme kabla ya kutoa ridhaa ya serikali juu ya mkopo huo mkubwa.
Lugola adai mawaziri wanamwandama
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) alisema kuwa anajua fika kuwa kuna mkakati ulioandaliwa kwa makusudi na baadhi ya mawaziri wakilenga kumdhohofisha.
Madai hayo yalitokana na hatua ya Mbunge wa Tumbe, Rashid Ali Abdallah (CUF), kumtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda, amtake Lugola apeleke ushahidi bungeni kuthibitisha madai yake kuwa baadhi ya mawaziri wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
“Mimi nilikuwa sijaingia ukumbini wakati waziri mkuu akijibu maswali lakini nilipoingia mwenzangu alinijulisha kilichojiri ila nilibaini kuwa yule aliyeuliza swali hilo alitumwa na hao wapinzani wangu (mawaziri),” alisema.
Aliongeza kuwa kwa vile Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, hakuchukua uamuzi wowote wa kumtaka awasilishe ushahidi wake bungeni, hivyo hawezi kusema lolote juu ya hilo.
“Hizo ni mbinu mbalimbali za kupambana na wabunge makini wanaotuona tuna msimamo, lakini kamwe siwezi kuogopa lolote, nitaendeleza msimamo wangu,” alisema.
Pinda wakati akijibu swali hilo alimwomba Lugola awasilishe ushahidi wa majina ya mawaziri wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya kama anao ili wachukuliwe hatua.
Lugola wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2013/2014, alisema kuwa kwa jinsi baadhi ya mawaziri wanavyoshindwa kuchukua hatua inatia shaka kwamba huenda wanajihusisha na biashara hiyo huku akitishia kuwataja watendaji wa serikali wanaojihusisha na rushwa.
CCM wahofia anguko 2015
Ahadi nyingi zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete wakati wa Uchaguzi Mkuu 2010, zimeanza kuwatia hofu wabunge wa CCM wakisema kuwa endapo hazitakelezeka, uchaguzi ujao utakuwa janga kwa chama hicho.
Wakichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka 2013/2014 bungeni mjini hapa, wabunge wengi wa CCM walimwangukia Dk. Harrison Mwakyembe, wakimtaka ahakikishe ujenzi wa reli, viwanja vya ndege, meli na bandari vinakamilika kabla ya mwaka 2015.
Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangala, bila kumng’unya maneno alimtaka Waziri Mwakyembe kwa kushirikiana na Waziri mwenzake wa Ujenzi, Dk. John Mgufuli kuhakikisha wanaufungua Mkoa wa Tabora kwa usafiri wa reli, anga na barabara.
“Tabora imechagua wabunge wote wa CCM 2010 lakini leo haifikiki kwa usafiri wowote, iwe reli, ndege wala barabara. Na hatua hiyo imewafanya wapinzani hasa CHADEMA na CUF kutuchonganisha kwa wananchi kuwa umaskini wao umetokana na kuichagua CCM.
“Sasa Mwakyembe kwa kushirikiana na Magufuli hakikisheni mnaifungua Tabora kwa kutekeleza ahadi za rais, vinginevyo uchaguzi ujao 2015 CCM itakuwa janga,” alisema.
Alisema anaamini kuwa Waziri Mwakyembe ana akili timamu, uwezo wa kufanya hayo, kwamba akiyafanya hayo hata mwaka 2015 wanaweza kumfikiria kwenye ile nafasi (akimaanisha urais).
Naya Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani, alimtaka Mwakyembe alieleze Bunge ni kwanini miradi yote ya wizara hiyo aliyoahidi Rais Kikwete haitengewi fedha.
Alisema kuwa wananchi wanahoji kiwanja cha ndege Tanga mjini, upanuzi wa Bandari ya Tanga na ujenzi wa bandari mpya ya Korogwe, huku akioneshwa kusikitishwa na uamuzi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo wakati ile ya Tanga ikiwa haijatekelezwa.
Ngonyani maarufu kama ‘Majimarefu’ aliongeza kuwa waliokuwa wafanyakazi wa reli Tanga waliahidiwa kulipwa madai yao lakini hadi sasa bado, hivyo kuonya kuwa bila mambo hayo kufanyika hali itakuwa ngumu kwa CCM 2015.
Bunge lahofia ugaidi
Vitendo vya kigaidi ambayo vimelikumba taifa hivi karibuni, vimeanza kulitia hofu Bunge, hivyo kuchukua tahadhari za kukabiliana navyo.
Pamoja na kutokuwepo taarifa zozote za vitisho, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limewataka wabunge kukubali utaratibu wa kuegesha magari yao nje ya uzio.
Taarifa ya Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah ilisomwa bungeni juzi mara mbili na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, ikiwataka wabunge kuanzia sasa wawe wanaegesha magari yao ndani ya uzio wa Bunge kwenye maegesho rasmi.
“Waheshimiwa wabunge kuna tangazo muhimu hapa linatoka kwa Katibu wa Bunge, linasema kuwa kutokana na tishio la vitendo vya kigaidi vinavyoendelea nchini mwetu kuanzia sasa magari ya wabunge wote yawe yanaegeshwa ndani ya uzio kwenye maegesho na si nje ya uzio wa Bunge kama baadhi wanavyofanya,” alisema.
Zungu aliongeza kuwa kwa wale watakaotaka kuendelea kuegesha magari yao nje ya uzio, watapaswa kuyaegesha ng’ambo ya barabara ya Dodoma - Dar es Salaam mkabala ya ukumbi wa Bunge.

No comments:

Post a Comment