Wabunge wanne wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamesema hawatakwenda kuhojiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kuhusiana na kadhia ya kutajwa na Bunge kuwa ni vinara wa vurugu bungeni, wakitaja sababu kadhaa, mojawapo ikiwa ni kutotambua uhalali wa kamati hiyo kwa madai kwamba, haipo kisheria.
Wabunge wanne wa Chadema waliotiwa hatiani na kamati hiyo kuhusiana na vurugu zilizotokea bungeni Februari 4, mwaka huu, ni pamoja Joshua Nassari (Arumeru Mashariki), Tundu Lissu (Singida Mashariki), John Mnyika (Ubungo) na Pauline Gekul (Viti Maalum).
Msimamo wa wabunge hao ulitangazwa na Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, alipozungumza na NIPASHE, saa chache baada ya kukutana na kamati hiyo na kugoma kuhojiwa nayo jana.
Lissu, ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) alisema aligoma kuhojiwa kutokana na kamati hiyo kumpa tuhuma jana ikiwa ni siku rasmi ya mahojiano, kinyume cha kanuni za Bunge, ambazo zinataka mbunge anapotuhumiwa apewe siku tatu za kujiandaa kabla ya kwenda kuhojiwa.
“Kwa hiyo, nimewaeleza kuwa mahojiano hayataanza mpaka kwanza nitakapojiandaa,” alisema Lissu, aliyetajwa na Bunge katika orodha ya wabunge wanne wa Chadema kwamba, ni vinara wa vurugu bungeni.
Alisema alikutana na kamati hiyo jana saa 4 asubuhi, lakini baada ya dakika 15 aliondoka baada ya kuitolea hoja kadhaa kuhusu utaratibu huo.
Lissu alisema sababu nyingine ya kukataa kuhojiwa, ni kwa vile kamati hiyo ilikaa Februaria 5 kujadili jambo hilo na Februari 8, mwaka huu, ikatoa hukumu yake mbele ya Bunge kwamba, katika uchunguzi wao wabunge wanne au watano walisababisha vurugu bungeni.
Hivyo, akasema kamati hiyo, ambayo kwa sasa inafanya shughuli zake kimahakama, haiwezi kukaa tena kwa jambo hilo.
“Mahakama ikishakamilisha hukumu, mamlaka yake yanaisha. Jambo hilo limeshaisha, haina mamlaka ya kusikiliza. Ni makosa kutushitaki tena sababu tulishashitakiwa na kuadhibiwa kwa kuitwa vinara wa vurugu na watovu wa nidhamu,” alisema Lissu.
Alisema hoja hiyo inatiwa nguvu na kifungu cha 280 cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai.
Lissu alisema kifungu hicho kinamlinda kwa kuwa tayari alishaachiwa huru na ‘mahakama’, hivyo hawezi kushitakiwa tena kwa kosa hilo hilo moja.
“Nilishaitwa kinara wa vurugu, nilishaadhibiwa,” alisema Lissu.
Alisema sababu nyingine ya kukataa kuhojiwa, ni kwamba, kamati hiyo ilikiuka Katiba ya nchi ilipokaa Februari 5,6 na 7, kwani haikuwapelekea hati ya mashtaka, pia haikuwapa fursa ya kujitetea.
Badala yake, alisema kamati hiyo iliwahukumu bila kuwaonyesha makosa yao ni yepi, kinyume cha Ibara ya 12 (6) na (7) ya Katiba ya nchi, ambayo inazuia haki na wajibu wa mtu kuamuliwa bila mwenyewe kusikilizwa kwa ukamilifu.
“Sisi haki na wajibu wetu vimeamuliwa (na kamati hiyo) bila kutupa haki ya kusikilizwa kabisa. Hivyo, kamati hii ni ya uvunjaji wa katiba,” alisema Lissu.
Alisema sababu nyingine ya kukataa kuhojiwa, ni ukiukwaji wa sheria ya haki, kinga na madaraka ya Bunge, uliofanywa na Bunge kutokana na kuwaita kwa kutumia ujumbe wa polisi, badala ya hati ya wito ya Bunge.
POLISI IMETUMIKA
Lissu alisema ujumbe huo ulitumwa na Bunge kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP, ambaye naye akausambaza kwa makamanda wa polisi wote wa mikoa.
“Hapo kuna ukiukwaji wa sheria. Kwani huo siyo wito kwa wabunge, bali ni police massage (ujumbe wa polisi). Kanuni za Bunge zinasema mbunge atapelekewa summons (hati ya wito). Utaratibu wa kutuita haukufuatwa,” alisema Lissu na kuongeza:
“Summons anakabidhiwa mbunge. Wana namba zetu za simu, tunapoishi wanapajua. Hawakuwa na sababu ya kututumia police massage.”
Alisema kinyume cha utaratibu huo wa kanuni za Bunge, wamekuta kuna barua iliyoandikwa na Katibu wa Bunge, ambayo siyo hati ya wito.
Lissu alisema sheria inataka hati ya wito kwa mbunge iandikwe na Katibu wa Bunge kwa maelekezo ya Spika, hivyo hawajui barua hiyo iliandikwa na nani, badala yake wanachoamini ni kwamba, haijaelekezwa na Spika.
Alisema sababu nyingine ya kukataa kuhojiwa, ni kwamba wanaamini kamati hiyo kisheria haipo kwa kuwa ilishavunjwa na kanuni za Bunge.
Lissu alisema kwa mujibu wa kanuni hizo, katika Mkutano wa 10 wa Bunge, kamati zote za kudumu za Bunge zinatakiwa zivunjwe.
KAMATI IMEKUFA
“Kwa hiyo, uenyekiti wa Ngwilizi kwenye kamati hiyo, haupo, ujumbe wa Vita Kawawa haupo, ujumbe wa Ndesamburo haupo na wajumbe wengine wote wa kamati ujumbe wao haupo. Uliisha tangu tarehe 8/2/2013,” alisema Lissu na kuongeza:
Alisema kutokana na kanuni za Bunge, Spika hana mamlaka ya kuvunja kamati moja peke yake, bali anatakiwa kuzivunja zote.
“Sasa hii kamati ya Ngwilizi inatoka wapi, kwa kanuni ipi, kwa sheria ipi?,” alihoji Lissu.
Alisema Februari 8, Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliunda na kutaja kamati mpya 18 na siku hiyo hiyo akasema agawe fomu kwa wabunge ili wajiunge kwenye kamati hizo, ikiwamo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
“Kwa hiyo, kamati ya Brigedia Ngwilizi ilishaisha. Wasubiri spika aunde upya,” alisema Lissu.
Alisema pia kanuni ya 113 (10) inazungumzia nafasi ya mwenyekiti na uenyekiti wa kamati ya Bunge kwamba, unakoma katika Mkutano wa 10.
Hivyo, akasema uhai wa Ngwilizi kama mwenyekiti wa kamati hiyo uliisha tangu Mkutano wa 10 wa Bunge ulipoahirishwa Februari 8, mwaka huu.
“Kwa hiyo, hatuna kamati, hatuna mashtaka, bali ni ukiukwaji wa kanuni uleule, ambao umekuwa ukifanywa na Bunge hili. Kwa sababu hizo, hatuwezi kuendelea kwenda kwenye chombo, ambacho hakipo kisheria,” alisema Lissu.
MBOWE AJA JUU
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amesema suala hapa si wabunge wa Chadema, bali wawakilishi wa wananchi, hivyo hawatakwenda kuhojiwa kwenye kamati hiyo na kwamba, kama ni kuwafukuza ubunge, wako tayari na Spika ajaribu kufanya hivyo.
Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, alisema kanuni ya Bunge namba 113 (7) inazungumzia ukomo wa uhai wa kamati za Bunge, kwamba unaishia Mkutano wa 10 wa Bunge, ambao unakuwa nusu ya kwanza ya uhai wa Bunge lenyewe.
Hivyo, akasema kamati hiyo inayowaita wabunge wa Chadema uhai wake uliisha siku Bunge la 10 lilipoahirishwa Februari 8, mwaka huu.
“Hivyo, kwa mujibu wa kanuni za Bunge kamati hiyo haipo na mwenyekiti wake alishamaliza muda wake,” alisema Mbowe.
Alisema wabunge wa Chadema wameitwa kwa sababu ya vurugu zilizotokea bungeni Februari 4, mwaka huu, wakati wanajua kuwa kamati hiyo hiyo tayari ilishalifanyia kazi jambo hilo.
Zaidi hivyo, alisema kamati hiyo ilitengeneza tuhuma, ikaendesha mashtaka, ikatoa hukumu, ikiwataja hata wahusika kuwa ni Lissu, Mnyika, Paulina Gekul (Viti Maalum) na Nassar.
Kutokana na hilo, aliwataka kutambua kuwa kamati hiyo inapokaa huwa ni sawa na mahakama, ambayo kwa kawaida kisheria na kikanuni, mahakama/kamati hiyo inapokuwa imeshaamua jambo haiwezi tena kukaa na kulifanyia kazi jambo hilo hilo.
“Mbele ya Watanzania wote, Tanzania nzima na dunia nzima ikasikia. Kamati ile iliwahukumu wabunge wa Chadema bila hata kuwasikiliza. Dunia nzima inajua hivyo. Sasa wanataka kusikiliza nini tena? Wakosaji wanajulikana. Walihukumiwa bila hata kufuata taratibu,” alisema Mbowe.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Brigedia Jenerali (mstaafu), Hassan Ngwilizi, akizungumza na NIPASHE alisema hawezi kuzungumzia chochote juu ya hilo bali atafutwe Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah.
Kwa upande wake Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai akizungumza na NIPASHE alisema ni kweli kuna wabunge ambao wangetarajiwa kuhojiwa na Kamati hiyo lakini hawezi kulizungumzia kwa mapana sana kwa kuwa siyo msemaji wa kamati hiyo.
Alisema katika Kikao kilichopita cha Bunge kiliipa jukumu Kamati hiyo kuchunguza vurugu zilizotokea bungeni hapo, na kueleza kuwa Kamati hiyo ilianza kufanya kazi ya kuchunguza wakati vikao vya bunge vikiendelea mjini Dodoma.
Alisema baada ya kukamilisha kufanya kazi ya kuchunguza vurugu zilizotokea bungeni hapo, Kamati hiyo ili kabidhi orodha ya baadhi ya wabunge waliowabaini kuwa ni chanzo cha vurugu hizo na ikawataja katika kikao cha bunge kilichopita.
Aliongeza kuwa baada ya Kamati kumaliza kazi ya kuchunguza na kuwataja wahusika hao kikabaki kipengele cha kutoa adhabu kwa wahusika waliobainika kuwa chanzo cha vurugu.
Ndugai alisema bunge baada ya kupata majina hayo ikaona ni vyema wabunge hao wahojiwe na kujitetea mbele ya kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kabla ya adhabu kutolewa dhidi yao.
Alisema kuna uwezekano mkubwa kwa wabunge hao kuanza kuhojiwa na Kamati hiyo kwa sasa kwa kuwa vikao vya bunge vinakaribia kuanza na adhabu inatakiwa kutolewa katika vikao vitakavyoanza hivi karibuni.
Mwisho.
MAANDAMANO DHIDI YA KAWAMBWA
Wakati huo huo, Mbowe ametangaza tamko la Musoma kwamba Machi 25, mwaka huu, katika majiji manne; Arusha, Mwanza, Mbeya na Dar es Salaam, yatafanyika maandamano makubwa yakihusisha kila raia mwema mwenye kuitakia elimu mema nchi hii, kuandamana ili Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, na Naibu wake, Philip Mulugo, wang’oke madarakan kutokana na matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana.
Katika matokeo yaliyotangazwa mwaka huu na Kawambwa Februari 8 mwaka huu, yalionyesha kuwa watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6 wamepata sifuri, huku 23,520 tu ambao ni sawa na asilimia 5.16 ndiyo waliofaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia 26.02 wamepata daraja la nne.
Dk. Kawambwa alisema watahiniwa walikuwa 456,137, wa shule wakiwa 397,136 huku wa kujitegemea wakiwa 68,806.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, watahiniwa waliopata daraja la kwanza ni 1,641, wavulana wakiwa 1,073 na wasichana 568, daraja la pili ni 6,453, wavulana wakiwa 4,456 na wasichana 1,997.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment