MBUNGE wa Ukerewe, Salvatory Machemli (CHADEMA) amefikishwa mahakamani akikabiliwa na mashitaka ya uchochezi.
Machemli (39) amesomewa mashitaka hayo jana mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya, Rouben Luhasha akidaiwa kutenda kosa hilo mwaka mmoja na nusu uliopita.
Mwendesha mashitaka wa polisi, ASP Denis Rwiza alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Oktoba 23, 2011 katika Kijiji cha Nyamanga kisiwani Ukara wakati akiutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CHADEMA.
Alisema mshitakiwa huyo kwa makusudi aliwachochea wananchi kutenda kosa la shambulio kwa kuwaelekeza wachukue uamuzi mgumu wa kuwazuia, hata kushambulia maofisa wa polisi wakiwa katika kazi zao kisiwani hapo.
Katika maelezo ya kosa, inadaiwa kupitia mkutano huo wa hadhara, aliwataka wananchi wazuie, wamshambulie kwa silaha za jadi ikiwemo marungu, mapanga na fimbo ofisa wa polisi atakayekwenda kutafuta washitakiwa nyakati za usiku.
Katika maelezo yake zaidi, mwendesha mashitaka huyo wa polisi alisema kipindi hicho ulikuwepo msako wa watuhumiwa wa mauaji ya watu wanne waliouawa na wananchi Desemba 10, 2010 mbele ya maofisa wa polisi kwa tuhuma za ujambazi.
Mshitakiwa huyo alipewa dhamana. Upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, na imeahirishwa hadi Machi 21, mwaka huu itakapotajwa na kusikiliza maelezo ya awali.
No comments:
Post a Comment