CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Mashariki inayohusisha mikoa ya kichama ya Ilala, Temeke Kinondoni na Pwani imekosa mratibu wa kanda mwenye sifa zinazotakiwa.
Kwa mujibu wa vigezo vilivyopitishwa na Baraza Kuu juu ya nafasi ya uratibu, ilihitajika mtu huyo kuwa mwenye kukijua chama hicho na mwenye uwezo wa kukisemea, kuratibu na kusimamia shughuli zake, pia uwezo wa kimenejimenti na kisiasa.
Sifa nyingine ni kuwa muunganishi asiye na makundi, mwenye nidhamu ya kichama na kazi, kujituma, aliye tayari kujitolea na awe mwanachadema mwenye uwezo wa kufanya kazi.
Kutokana na vigezo hivyo, waombaji walioomba kuchaguliwa kwa nafasi hiyo walionekana kukosa vigezo, jambo lililosababisha chama hicho kuitangaza tena nafasi hiyo ili wanachama zaidi waweze kuiomba.
Katika taarifa iliyotolewa na mratibu wa muda wa kanda, Henry Kilewo, mwisho wa kupokea maombi ilikuwa ni Februari 22 mwaka huu, lakini hadi mwisho waliotuma maombi hawakuwa na sifa.
Hayo yalibainika baada ya viongozi wa kanda kukaa na kupitia majina ya zaidi ya waombaji 240 waliotuma maombi yao.
Kanda imechuja majina hayo na kuyabakiza 22, kisha ikaunda kamati ndogo ya kanda kuyachambua na kuyabakiza 10.
Majina hayo yaliingia kwenye nafasi ya uafisa, kutokana na vigezo kwenye nafasi ya uratibu vilivyokuwa vimepitishwa na Baraza Kuu Januari 28.
Kamati ndogo ya kanda ya Mashariki kwa kufuata vigezo hivyo haikupata mtu mwenye sifa kwenye nafasi hiyo na badala yake ikapendekeza majina hayo kumi yaingizwe katika nafasi ya ofisa wa kanda ambapo waombaji walikidhi vigezo.
Kamati hiyo imetoa tena fursa ya kidemorasia kwa wanachama watakaokidhi vigezo vya uratibu kutuma tena maombi katika ofisi za CHADEMA katika mikoa ya Temeke, Kinondoni, Ilala na Pwani hadi Machi 13 na watakaoona wanastahili kwa hiari yao wawe wamekamilisha mchakato huo.
No comments:
Post a Comment